M
|
wanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Jaji
Frederick Werema amejiuzulu nafasi yake hiyo kuanzia jana, Jumanne, kufuatia
sakata la uchotaji wa fedha kutoka akaunti ya ESCROW ambapo zaidi ya dola
milioni 120 zilihamishwa.
Mwanasheria
mkuu, pamoja na baadhi ya wanasiasa na maafisa waandamizi wa serikali
walituhumiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha kufanyika kwa
miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta.
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam, imesema Rais Jakaya Kikwete
alikubali ombi hilo la kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali.
Katika
barua yake kwa Rais Kikwete, Jaji Werema alisema ameomba kujiuzulu kwa sababu
ushauri wake kuhusiana na suala ya Akaunti ya Tegeta Escrow haukueleweka na umechafua
hali ya hewa.
Rais
Kikwete amemshukuru Jaji Werema kwa utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na
uadilifu.
Itakumbukwa
kwamba sakata la Akaunti ya Escrow liliibuliwa bungeni na mmoja wa wabunge wa
bunge la Tanzania, David Kafulila na kusababisha mjadala mkali na kuamua Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kupewa jukumu la kuchunguza kashfa
hiyo.
Baada
ya uchunguzi kuwasilishwa katika mkutano wa bunge uliomalizika mwishoni mwa
mwezi Novemba, kamati hiyo ilikuja na maazimio manane kuhusu taarifa ya ukaguzi
maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya Escrow ya Tegeta
pamoja na umiliki wa kampuni ya IPTL.
Miongoni
mwa maazimio ya bunge yaliwataja baadhi ya wanasiasa, mwanasheria mkuu, maafisa
waandamizi wa serikali, majaji, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini,
mawakili wa kujitegemea na watu binafsi kuhusika katika kashfa hii na hivyo
kuagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua za kisheria wahusika na wengine
kuondolewa katika nyadhifa zao za kuteuliwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni