Jumanne, 23 Desemba 2014

TAASISI ZA MAGEREZA NA POLISI WADAIWA SUGU, MAJI WILAYANI ROMBO



Z
aidi ya asilimia 70 ya maji yanayozalishwa na kampuni ya Maji ya Kili Water wilayani Rombo hupotea kila mwaka huku kampuni hiyo ikikabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundo mbinu na wizi wa maji.
Pamoja na upotevu wa asilimia hizo, bado kampuni hiyo inakabiliwa na changamoto ya kuzidai taasisi za magereza na jeshi la polisi wilayani humo zaidi ya shilingi milioni 25 pamoja na jumuiya ya watumia maji ya Mwika Kaskazini na Mwika Kusini zaidi ya shilingi milioni 145.


Katika  taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni ya Maji ya Kili Water  Theodory Silayo,  aliyoiwasilisha katika mkutano mkuu wa mwaka wa  18, pamoja na mambo mengine alieleza changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni uchakavu wa miundombinu na madeni makubwa kwa taasisi za magereza na polisi wilayani humo.

Silayo alisema kuwa upotevu huo wa maji unatokana na uchakavu wa miundo mbinu ambayo imekuwa ikiharibika mara kwa mara na kupelekea hasara kubwa katika ukarabati na wakati mwingine kupelekea kuwapo kwa mgao wa maji ambao haukwepeki.

 “Ndugu wana hisa, kampuni yetu inakabiliwa na changamoto nyingi sana, kubwa kati ya hizo ni ya wadaiwa sugu, ikifuatiwa na upotevu wa maji ambapo ni asilimia 70 kwa mwaka pamoja na uchakavu wa miundo mbinu ambayo inapelekea kuwapo kwa mgao kwa baadhi ya maeneo…nyingine mnaifahamu ambayo ni ya wadaiwa sugu ambao ni mwika kaskazini na kusini bila kuwasahau magereza na jeshi la polisi,” alisema Silayo

Naye  Meneja biashara wa Kampuni hiyo,  Barth Willa alisema kampuni hiyo imejiwekea  mikakati mbalimbali  kwa kipindi cha mwaka ujao ikiwa ni pamoja na kukarabati miundo mbinu iliyochakaa ambapo wametenga zaidi ya shilingi milioni 115 na watatoa zawadi kwa wasamaria wema watakaotoa taarifa za za kufanikisha kuwakamata wezi wanaojiunganishia maji pasipo utaratibu ikiwemo na wale wanaoiba maji nyuma ya dira waliyofungiwa.

Awali akifungua mkutano huo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Rombo, Mohamed Maje, aliwataka viongozi wa vijiji na vitongoji kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji linazingatiwa, ili kuendelea kuwepo kwa maji katika vyanzao hivyo.

Maje alisema kuwa hatosita kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wale watakaokwenda kinyume na misingi ya sheria, miongozo na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya viongozi wazembe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni