Jumanne, 30 Desemba 2014

ASANTE MABALOZI KWA KUZURU MLIMA KILIMANJARO 2014



Desemba 16, mwaka huu Mabalozi 20 wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbali mbali duniani walianza safari ya kuupanda mlima Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu kuliko yote barani Afrika kupitia lango kuu la Marangu ambako pia yapo makao makuu ya Hifahdi ya Taifa ya mlima huo(KINAPA) huku wakibeba ujumbe mzito wa Diplomasia ya uchumi kileleni .

 BALOZI BATILDA BURIAN (KUSHOTO), RADHIA MSUYA (KULIA), CHARLES SANGA WAKIWA NA WAFANYAKAZI KAMPUNI YA ZARA TOURS NJE YA HOTEL YA PARKVIEW INN MUDA MFUPI KABLA YA SAFARI YA KUPANDA MLIMA KILIMANJARO.


Mabalozi waliopanda mlima huo na nchi zao kwenye mabano ni Dk. Batilda Buriani (Kenya), Ptrick Tsere (Malawi), Joseph Sokoine (Ulaya na Marekani), Mbaruku Nassor  Mbaruku (Falme za Kiarabu), Dk.Aziz Mlima (Malaysia), Dk. Ladislaus Komba (Uganda) na Adad Rajabu (Zimbabwe).
Wengine ni Celestine Mushi, ambaye ni Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa, Charles Sanga aliyepata kuwa Balozi wa Tanzania nchini China ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shamim Nyanduga (Msumbiji), Grace Mujuma (Zambia), Ramadhan Mwinyi (UN), John Kijazi (India) na Mbelwa Kairuki (Asia na Australia).
Waliofanikiwa kufika kilele cha uhuru ni balozi Joseph Sokoine,Daniel Ole Njoolay,Mbarouk Nassor Mbarouk,Dkt.Aziz Mlima,Dkt.Ladslaus Komba,Celestine Mushi,Adadi Rajabu,Dkt.Bernard Achilwa na balozi mwanamama pekee aliyekifikia kilele hicho Dkt.Batilda Burian.
Balozi Charles Sanga ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Bodi ya Utalii nchini(TTB) yeye alikwea na kufikia kituo cha Gilmans huku balozi Grace Mwijuma na Shamim Nyanduga wakiishia eneo  la Hans meyer Cave umbali mfupi kutoka kituo cha Kibo.
Mabalozi Radhia Msuya ambaye ndiye aliyefanikisha zoezi la kuwakusanya mabolozi hao na kuwashawishi kupanda mlima pamoja na mabalozi Patrick Tsere,Ramadhan Mwinyi,John Kijazi na Mbelwa Kairuki wao waliishia kituo cha Horombo.
Mabalozi hao waliagwa rasmi katika lango kuu la Marangu na waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe na kumkabidhi bendera ya taifa kiongozi wa msafara huo Balozi Adadi Rajabu .
Waziri Membe hakuishia kuwaaga mabalozi hao tu na kuwakabidhi bendera ya Taifa bali aliungana nao katika safari hiyo hadi eneo la nusu njia maarufu kwa jina la Kisambioni akitumia muda wa saa moja na nusu ambako alipata chakula cha mchana na mabaozi hao katika eneo hilo na kisha kurejea Dar es salaam.
Niwapongeze mabalozi wote waliothubutu kupanda mlima huo na wale walioishia njiani nao wameonyesha kuwa wanaweza na wasikate tama na wajiandae kwa safari nyingine kwani ni ukweli ulio wazi kuwa kazi ya kuupanda mlima Kilimanjaro si lelemama,ni safari inayohitaji maandalizi ya nguvu ikiwamo mazoezi ya kutosha.
Lengo la mabalozi hao kuupanda mlima Kilimanjaro kwanza ni pamoja na kujifunza zaidi juu ya mlima huo na pia kufahamu vyema vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya mlima huo  ili kuwawezesha kuutangaza vyema katika maeneo yao ya kazi.
Lakini jambo jingine kubwa ni kujionea maajabu yaliyomo ndani ya mlima huo na kuondokana na dhana potofu inayoedezwa na wenzetu Kenya kwamba mlima Kilimanjaro upo nchini mwao hatua ambayo imewawezesha kuvuna mamilioni ya fedha za kigeni kupitia propaganda hiyo chafu.

Kampuni nyingi za wakala wa utalii nchini Kenya zimeweza kuwahadaa watalii kwa vipeperushi vyao vinavyosema 'njoo Kenya uone mlima Kilimanjaro',kampeni iliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa kwani hata mitandao ya simu za kiganjani zimepenyeza hadi upande wa Tanzania na unapoingia wiaya ya Rombo unakaribishwa na ujumbe wa mitandao hiyo.

Hili pia lilishuhudiwa na mabalozi wetu ambao walijikuta simu zao za kiganjani zikiingiliwa na mawasiliano ya mitandao ya kenya na hawakisita kulizumgumzia muda mfupi baada ya kushuka kutoka kileleni kwenye chakula cha mchana kilichoandaliwa na TANAPA.

Kwa faida ya wasomaji wa blog hii ni kwamba Hifadhi hii ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro  ilianzishwa rasmi mwaka 1973 kwa tangazo la serikali namba 50 machi 16,1973  na shughuli za utalii zilifunguliwa rasmi mwaka 1977 na mwaka 1989 hifadhi hiyo ilitangazwa kuwa eneo la urithi wa dunia.

Madhumuni ya kuanzishwa kwa hifadhi hii ni kuuhifadhi mlima Kilimanjaro pamoja na maeneo yanayouzunguka mlima huo ambayo ni pamoja na vilele vitatu kikiwamo cha Shira,Mawenzi na Kibo.

Kilele cha Shira chenye urefu wa mita 3,692 kutoka usawa wa bahari ni Volkano iliyokufa(extrict volcano) wakati kilele cha Mawenzi chenye urefu wa mita 5,149 na  Kibo chenye urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa habari  ni Volkano iliyolala(dormant volcano).

Hivyo basi hili ni tukio kubwa na mhimu sana kwa mabozi wetu kupanda mlima huo na hivyo kuwa mabalozi wazuri katika uuutangaza mlima wetu .

Kitendo kilichoonyeshwa na mabalozi hao kuupanda mlima kilimanjaro kwa lengo la kujifunza na kuhamasisha watalii huko waliko kuja nchini kupanda mlima huo ni kitendo cha kizalendo na cha kuungwa mkono kwa nguvu zote.

Pia kitendo hicho kiwaamshe mabalozi wengine ambao hawakuweza kuja nchini kupanda mlima huo nao wafanye hivyo ili kuwe na nguvu ya pamoja katika kuutangaza utalii wetu nje ya nchi. 

Ni wazi kwamba kama mwamko  huu ulioonyeshwa na mabolozi wetu kuja kupanda mlima Kilimanjaro na kutembelea baadhi ya vivutio katika hifadhi zetu zingine za taifa utaleta hamasa kubwa kwa watanzania wengine kuwa na moyo wa kupenda kuupanda mlima huu.

Kwa sasa baadhi ya watalii kutoka mataifa ya magharibi wamesitisha baadhi ya safari zao  kutembelea vivutio vya utalii katika nchi za Afrika ikiwamo Tanzania kwa hofu ya kuambukizwa ugonjwa wa Ebola.

Wazungu hawa waamamini ugonjwa wa ebola upo katika bara zima la afrika wakati ukweli ni kwamba ugonjwa huo upo katika baadhi ya nchi za Afrika magharibi na si nchi zote za ukanda huo.

Wenzetu wanaamini ya kwamba Afrika ni sawa na mkoa mmoja hivyo tukio linapotokeo sehemu moja ya nchi mojawapo za afrika wanachukulia ni afrika nzima huu ni upuuzi ambao sharti upingwe kwa nguvu zote.

Kazi ya kupambana na upuuzi huu  yafaa ifanywe na mabolozi wetu walioko nje ya nchi na watakaoupinga kwa vielelezo ili kuwaondolea kasumba hiyo hawa wenzetu wazungu wanaochukulia matatizo ya nchi moja kuwa ni matatizo ya bara zima la Afrika.

Kwa kufanya hivyo tutawawezesha kuondokana na kasumba hiyo ya kuona matatizo ya nchi moja kuwa ni matatizo ya nchi zote za Afrika na huo ndiyo ukweli wa mambo,hongereni mabalozi wetu na asanteni kwa uzalendo wenu.

MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA






ZINAZOFANANA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni