Kiongozi wa kundi la
kigaidi la Al-Shabaab nchini Somalia, Zakariyah Ismail Ahmend Hersi, amekamatwa
na polisi baada ya kujisalimisha jana Jumamosi.
Afisa
mmoja wa idara ya ujasusi amesema Hersi alijisalimisha kwa polisi katika mkoa
wa Gedo, baada ya kile kinachoonekana ni uwezekano wa kuzuka mzozo ndani ya
kundi hilo.
Huenda
Hersi anatofautiana na wapiganaji watiifu kwa kiongozi wa Al-Shabaab, hayati
Abdi Godane, aliyeuawa katika shambulio la anga lililofanywa na Marekani
mwanzoni mwa mwaka huu.
Kwa
mujibu wa shirika la habari la AFP, afisa wa kijeshi wa ukanda huo, Jama Muse,
amesema Hersi alikuwa anasimamia masuala ya kijasusi na fedha na pia alikuwa ni
mmoja kati ya makamanda waandamizi wa Al-Shabaab.
Ingawa jeshi la Somalia
lilimuweka katika orodha ya mawakala wa Al-Shabaab, haijafahamika wazi iwapo
Hersi bado alikuwa ana nguvu ndani ya kundi hilo la kigaidi katika miezi
michache iliyopita. Inawezekana kuwa Hersi alikuwa miongoni mwa kundi la
makamanda waliotofautiana na Godane kabla ya kifo chake.
CHANZO: DW
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni