Mvua
iliyonyesha kwa saa mbili katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam
jana, imeleta kero kwa wasafiri wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu na
kusababisha baadhi ya barabara kushindwa kupitika kutokana na kujaa maji.
Mvua
hiyo iliyoanza saa nne asubuhi hadi saa sita mchana, ilisababisha baadhi ya
barabara kutopitika ikiwamo ile ya Samora karibu na Jengo la Wizara ya Nishati
na Madini, baadhi ya maeneo ya Upanga na Msasani.
Aidha,
watumiaji wa Barabara za Azikiwe, Bibi Titi na Morogoro katikati ya jiji
walikuwa na wakati mgumu kupita, wengi walionekana wakiwa wamevua viatu au
kutafuta njia mbadala kukwepa maji hayo ambayo yalionekana kuchanganyika na
majitaka yaliyotokana na baadhi ya chemba kujaa.
Eneo
linalojengwa njia za mabasi ya haraka katika eneo la Akiba, lilifunikwa na maji
na kusababisha usumbufu kwa vyombo vya moto na watembea kwa miguu.
Maeneo
ya Kariakoo, Barabara ya Uhuru na Msimbazi, yalijaa maji kama ilivyokuwa
Barabara ya Umoja wa Mataifa na kuelekea Hospitali ya Taifa Muhimbili ambazo
zilikuwa hazipitiki kutokana na mvua hizo na kusababisha msongamano mkubwa wa
magari.
Wakazi
wa mabondeni walianza kuingiwa na hofu ya kukumbwa na mafuriko wakati hali ya
hewa ilipokuwa inabadilika huku mvua ikiongezeka kwa kasi. Katika bonde la
Msimbazi, Kigogo na Jangwani wakazi walionekana wenye hofu baada ya mvua
kuongezeka.
Mkurugenzi
wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alikataa kusema lolote na kusukuma mpira
kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mgurumi.
Hata
hivyo, Mgurumi alipopigiwa simu yake ya kiganjani ilikuwa inaita bila kupokewa.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Agnes Kijazi alisema hayo ni
matokeo ya taarifa ya hali ya hewa waliyoitoa Oktoba, Novemba na Desemba ambayo
yalibainisha kuwa kutakuwa na vipindi virefu vya jua katika msimu wa mvua
pamoja na mvua kubwa. Alisema mvua zilizonyesha jana, zinanyesha mwisho wa
msimu wa mvua kama ilivyotabiriwa kabla.
Kijazi
alisema kesho (leo) wanatarajia pia mvua kubwa kutokana na kuwapo kwa
mkandamizo mkubwa wa hewa katika pwani ya Madagascar.
“Kesho
(leo) tutatoa taarifa nyingine ya hali ya hewa kwa kipindi cha miezi mitatu
mingine, hivyo wananchi watumie taarifa hiyo katika mipango yao mbalimbali,”
alisema mkurugenzi huyo.
CHANZO: MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni