Mali zenye thamani ya
zaidi ya shilingi milioni 100 zimeteketea kwa moto yakiwemo maduka sita na basi
dogo la abiria lililokuwa gereji kwa ajili ya matengenezo katika tukio
lililotokea mjini Moshi hapa mkoani Kilimanjaro.
Mashuhuda wa tukio
hilo lililotokea katika mtaa wa Bakwata-Sido katika Manispaa ya Moshi walisema
moto ulianza majira ya saa 6:30 usiku wa kuamkia leo, ukianzia katika kibanda
cha kuchaji betri za magari.
“Kuna kibanda cha
kuchaji betri za magari katika gereji ya vijana ambako betri zilikuwa
zikichajiwa humo ambako shoti ya umeme ilitokea na kulikuwa na oil zilizokuwa
zimetapakaa chini hivyo cheche za moto ziliruka na kusababisha mlipuko huu,”
alisema shuhuda mmoja.
Mmiliki wa mojawapo
ya maduka aliyetambulisha kwa jina la Justo Elias Mboho alisema taarifa za kulipuka
kwa maduka katika mtaa ulio na shughuli nyingi za ufundi magari na uuzaji wa
mitungi ya gesi alizipata usiku na kwamba kila kitu kimeteketea kwa moto.
“Sikuwa na jinsi
nilipoambiwa kwamba mali zote zimeteketea kwa moto hivyo nikaona hakuna haja ya
usiku huo kuja katika eneo la tukio hadi asubuhi ambako kila kitu kimeteketea…
mali zenye thamani ya shilingi milioni 5 katika duka langu zimeteketea zote,”
alisema Mboho.
Aidha mmiliki
mwingine aliyejifahamika kwa jina la Living Mrema alisema duka lake lilikuwa na
vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 20 viliteketea kwa moto na
kuongeza kwamba kwa ujumla wa maduka yote sita zaidi ya shilingi milioni 90
zimeteketea kwa moto.
Katika tukio hilo
mashuhuda waliongeza kusema gari la zimamoto la Manispaa ya Moshi liliishiwa
maji hivyo kuomba msaada wa zimamoto ya Kiwanda cha Sukari (TPC) ambao walifika
na kuambulia kuzima moto tu kutokana na umbali hadi eneo la tukio.
Kwa upande wake
Diwani wa Kata ya Korongoni, Said Mwamba alilitupia lawama Jeshi la Polisi
mkoani Kilimanjaro, kikosi cha Zimamoto-Kilimanjaro na Manispaa ya Moshi
kutokana na uzembe wa matukio kadhaa ya moto.
“Niliamshwa usiku na
vijana kwamba moto unawake katika mtaa wa Bakwata-Sido, nikapiga simu jeshi la
polisi simu zilikuwa zikiita bila kupokelewa na nyingine kuzimwa kinyume na
maadili ya kazi yenyewe, zimamoto nao waliishiwa maji huku Manispaa
nilishawaambia mapema kwamba uuzwaji wa gesi katika eneo hili ambalo ni makazi
ya watu ni hatari,” alisema Diwani Mwamba
Diwani huyo aliongeza
kuwa chanzo ni mrundikano wa vifaa vya gereji ya karibu (Vijana Garage)
bila kufanyiwa usafi na kuwekwa kwa utaratibu hali ambayo ingeweza kuleta
maafa zaidi katika eneo hilo.
Jeshi la Polisi
mkoani Kilimanjaro limethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku uchunguzi zaidi
ukiendelea.
CHANZO: JAIZMELALEO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni