Ijumaa, 24 Novemba 2017

EU YAITAKA TANZANIA IJITATHIMN MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA



Umoja wa Ulaya (EU) umeitaka serikali ya Tanzania kuimarisha taasisi za uwajibikaji na uwazi kwa kupanua wigo wa Asasi za Kiraia kufanya kazi na jamii ili ifanikiwe katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwaletea wananchi maendeleo.  

Tamko hilo la EU linakuja siku chache baada ya serikali kuiondoa Tanzania kwenye Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa  (OGP) na kuziagiza Halmashauri za miji kutoshirikiana na Asasi za kiraia mpaka zipate idhini ya Wizara Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). 

Wito huo umetolewa  jijini Dar es Salaam na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Roeland van de Geer wakati akizindua Mradi wa Kutete Haki ya Demokrasia, Uwazi na Uwajibikaji katika jamii, 

Amesema changamoto kubwa inayoikabili Tanzania ni rushwa ambayo imedhoofisha juhudi za serikali kuwaletea wananchi maendeleo. 

“Rushwa inaharibu rasilimali za wananchi na jamii, zaidi kuvunja haki zao za msingi na uhuru. Gharama za kiuchumi ni kubwa lakini gharama za rasilimali watu na jamii ni kubwa zaidi”, amesema Balozi Geer na kuongeza kuwa,

“Rushwa ni adui wa maendeleo na mafanikio. Ni chanzo kikubwa cha umaskini na kikwazo kuushinda. Dawa ni uwazi”. 

Ili kuhakikisha rushwa inatokomezwa katika jamii, ameshauri kuundwa kwa taasisi imara zinazojiendesha kwa uwazi na kuwajibika kwa wananchi ambao ndio wadau muhimu wa shughuli za maendeleo. 

“Kupambana na rushwa ni mapambano yanayohitaji taasisi imara na wananchi makini katika ngazi zote. Lakini rushwa haitokei Tanzania peke yake.  

Rushwa ipo kila sehemu lakini tofauti ni kwamba taasisi zao zina uwezo na utashi wa kupambana nayo”, amesema Balozi.

Ameongeza kuwa rushwa bado ni changamoto katika Umoja wa Ulaya ambapo kila mwaka inaigharimu Euros bilioni 120 kwa mwaka. 

Amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuzijengea uwezo Asasi za Kiraia na wananchi hasa kwenye masula ya demokrasia, uwazi na uwajibikaji wa viongozi katika jamii ili kujenga jamii inayoheshimu misingi ya demokrasia.
 
Uwazi na Uwajibikaji katika Serikali za Mitaa
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa ‘Tuungane Kutete Haki’, Daniel El-Noshokaty amesema ili mapambano ya rushwa yafanikiwe inahitajika nguvu ya pamoja katika ngazi ya serikali ya mitaa ambako uwakilishi wa wananchi unapatikana.

“Rushwa ni kikwazo katika njia ya maendeleo ambayo Tanzania inapita; mapambano yake yanatakiwa kuanzia kwenye mizizi ya taifa. Kwa kufanya hivyo, nchi itakuwa na nafasi nzuri ya kutokomeza rushwa katika ngazi ya juu. Kwa Pamoja Tanzania inaweza ikasimama na kupambana na rushwa”, amesema El-Noshokaty. 

Kulingana na Shirika la Transparency International (2016) inaiweka Tanzania katika nafasi ya 116 katika ya nchi 176 zenye viwango kikubwa cha rushwa duniani. Na sababu kubwa ni kutokuwa na mifumo imara ya kitaasisi inayofanya kazi kwa uhuru na uwazi. 

Licha ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Magufuli kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa, bado rushwa inajitokeza kwa sura tofauti na kuathiri kwa sehemu kubwa upatikanaji wa huduma za kijamii, kudhoofisha mfumo wa utawala na kuzuia mazingira mazuri ya kufanya biashara. 

Ufunguzi huo wa Mradi wa ‘Tuungane Kutetea Haki” ulihudhuliwa na wadau mbalimbalimbali kutoka Asasi za kiraia na viongozi wa serikali, ambapo wote wamesisitiza uwepo wa uwazi katika shughuli za maendeleo na viongozi kuwa tayari kuwajibika kwa wananchi ili kujenga jamii inayoheshimu misingi ya demokrasia.

Mabadiliko ya Sera na Sheria kuchochea Uwazi

 
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa InterStar Consults, Lawrence Kilimwiko amesema Serikali za Mitaa zinaongozwa kwa msukumo wa kisiasa na utashi wa baadhi ya viongozi toka Serikali Kuu ambao wanatumia rasilimali za nchi kwa manufaa binafsi.

Ameitaka jamii kupaza sauti na kudai uwajibikaji na uwazi kwa kupigania mabadiliko ya kisheria na sera ambazo zimekuwa kikwazo kwa maendeleo ya nchi.  

Mradi wa ‘Tuungane Kutetea Haki’ unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya, Konrad-Adenauer-Stiftung (KAS) kwa kushirikiana na taasisi za Actions for Democracy and Local Governance (ADLG) na Civic Education Teachers Association (CETA) ambao utagharimu bilioni 2.5 katika miaka miwili ya utkelezaji wake.

Mradi huo una lengo kupunguza mianya ya rushwa kwa kukuza ushirikiano baina ya Asasi za Kiraia (AZAKI) na Serikali za Mitaa kwa kupanua wigo wa siasa, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ngazi ya Halmashauri. 

Unatekelezwa katika mikoa ya Geita, Simiyu, Ruvuma, Lindi, Mara, Kagera na Pwani ambaopo utafanya kazi sambamba na vyombo vya habari zikiwemo redio za kijamii katika maeneo husika.

BREAKING NEWS,ALIYEKUWA MKUU WA MKOA WA K'NJARO LEONIDAS GAMA AMEFARIKI DUNIA

Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro(2011-2015) pichani na mbunge wa Jimbo la Songea mjini enzi za uhai wake

Pichani aliyekuwa mkuu wa mkoa wa kilimanjaro na mbunge wa Jimbo la Songea mjini,Leonidas Gama(enzi za uhai wake)Gama amefariki dunia usiku wa kuamkia leo akiwa katika Hospital ya Pelamiho

Jumatano, 22 Novemba 2017

JENGO LA BENKI YA USHIRIKA KILIMANJARO(KCBL)ILIYOPO MJINI MOSHI


BENKI YA KCBL YATUMIA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI KUKOPESHA WAKULIMA WA KAHAWA



Na Charles Ndagulla,Moshi

MIKOPO yenye riba kubwa na masharti magumu katika upatikanaji wa mikopo kwenye mabenki mengi hapa nchini imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa wakulima wengi hasa wadogo wadogo hali ambayo imechangia wengi wao kuishi maisha ya dhiki.

Hii inatokana na mabenki mengi kujiendesha kibiashara zaidi kwa kutoza riba kubwa pamoja na masharti magumu katika upatikanaji wa mikopo kwa wakulima ambao wengi hawana mali zinazoweza kuwekwa kama dhamana ya mkopo.

Benki ya ushirika mkoani Kilimanjaro(KCBL)iliyopo mjini moshi imeweza kuliona hilo na kujikita katika utoaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima wadogo wadogo lengo ni kuwawezesha kuboresha maisha yao.

Mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wakulima kukusanya mazao hususani zao la  kahawa kupitia mfumo wa stakabadhi ya mazao  ghalani ambao unatajwa kama mfumo bora na rafiki kwa wakulima wa zao la kahawa .

Benki hii ya ushirika ilisajiliwa kama chama cha ushirika mwaka 1994 kabla ya mwaka 1995 kupata  leseni ya kutoa huduma za kibenki ambako mwaka uliofuata yaani 1996 huduma za kibenki zilianza rasmi.

Meneja Mkuu wa Benki hiyo,Joseph Kingazi anasema mpaka sasa benki hiyo inao wanahisa 245 ambao ni vyama vya ushirika wa mazao (AMCOS),vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo(SACCOS) pamoja na watu binafsi wapatao 307.

Anasema wazo la kuanzishwa kwa benki hiyo kulitokana na mawazo yaliyotolewa na vyama vya ushirika wa mazao(AMCOS)mkoani Kilimanjaro ili kuweza kupata mikopo yenye riba na masharti nafuu katika kukusanya mazao yao.

“Lengo kuu la kuanzishwa kwa benki hii ilikuwa kuwasidia wakulima wadogo wadogo kuweza kupata mikopo yenye riba na masharti nafuu tofauti na mabenki mengine katika ukusanyaji wa mazao hususani zao la kahawa kupitia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani”,anasema kingazi.


Meneja huyo anataja mafanikio sita ambayo benki hiyo imepata tangu kuanzishwa kwake miaka 20 iliyopita ikiwa ni pamoja na kuwafikia wateja zaidi ya 762,177 katika mkoa wa Kilimanjaro na mikoa mingine iliyo jirani na mkoa huo .

Mafanikio menigne ni kuwa benki ya ushirika ya kwanza nchini inayomilikiwa na wazalendo kwa aslimia 100 huku ikitoa mikopo kwa wakulima wa zao la kahawa  yenye thamani ya ya shilingi Bilioni 28 hadi kufikia msimu wa kilimo wa 2016/17.

“KCBL imekuwa mwanzilishi wa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani toka mwaka 1999 na kwa sasa mfumo huu umeweza kuenea na kutumika sehemu mbali mbali hapa nchini  hasa kwenye mazao ya pamba,korosho na mazao mengine”,anasema.

Kwa mujibu wa meneja huyo,uwepo wa benki hiyo umekuwa kimbilio kwa wakulima wengi hatua ambayo imekuwa chachu kwa wakulima hao kuboresha maisha yao huku wanahisa na wateja wa kawaida wakipewa mafunzo mbalimbali kupitia kwa wataalam wa benki hiyo.

Anasema tangu kuanza kwa mfumo wa stakabadhi ya mazo ghalani,KCBL imeweza kumsaidia mkulima kutoka kukopwa mazao yake na kupata malipo kwa wakati huku mfumo huo ukivisaidia vyama vya msingi vya ushirika kujitegemea katika kununua mazao.

“Mfumo huo pia umevisaidia vyama vya msingi vya ushirika kujitengenezea mfuko wake wa ndani kwa ajili ya kununua mazao msimu bubu unapoanza tofauti na miaka ya  nyuma kabla ya mfumo haujaanza”,anasema.

Kwa upande wa wakulima meneja huyo anasema kuwa mfumo huo umechangia kuwahamasisha wakulima kulima kahawa kwa wingi kutokana kutokana na kupata malipo kwa wakati pale anapoleka mazao yake chamani.

Ametaja faida nyingine wanayopata wakulima kutokana na mfumo hiuo wa stakabadhi ya mazao ghalani kuwa ni pamoja na kupanda kwa bei ya kahawa kila msimu,kupanda kwa ubora wa mazao .

“Pia mkulima amefaidika kutokana na kupata faida  kwenye fedha za kigeni (Foreign Exchange Gain) pamoja na kupata  riba nafuu ikilinganishwa na wateja wengine”.anasema.

Anasema mikakati yao ya baadaye katika kuhakikisha wakulima wa zao la kahawa wananufaika na mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ni pamoja na kuuboresha mfumo huo ili wakulima waweze kuutumia vizuri.

Mikakati mingine ni kutoa elimu na semina kwa wakulima kwenye kilimo cha kisasa cha kahawa,elimu juu ya tabia yakujiwekea akiba pamoja na kutoa mafunzo kwa watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika .

Kupitia mfumo huo wa stakabadhi ya mazao ghalani,KCBL imeweza kutoa mikopo kwa ajili ya makusanyo ya kahawa na zaidi ya aslimia 75 ya kahawa yote  ya mkoa wa Kilimanjaro imefadhiliwa na benki hiyo.

Mpaka sasa benki hiyo inatoa huduma zake katika wilaya zote saba za mkoa wa Kilimanjaro ambazo ni Same,Mwanga,Rombo,Moshi Vijijini,Hai Siha na Moshi mjini na mkoa wa Arusha.

“Tunatoa huduma zaidi vijijini kupitia vyama vya msingi vya ushirika na kumfikia mtu/mkulima wa chini kabisa,pia tumefungua kituo cha huduma kwa wateja katika wilaya ya Rombo eneo la Tarakea Kibaoni”,anasema.

Licha ya baadhi ya  benki kuyumba katika utoaji wa mikopo kutokana na serikali kupitisha uamuzi wa kuzihamishia akaunti zote za serikali benki kuu,KCBL haijaguswa na hali hiyo kutokana na kutokuwa na fungu lolote toka serikalini.

Kwa mujibu wa meneja huyo wa benki ya ushirika,benki yake imekuwa ikitegemea akiba za wateja wao katika kufanya biashara ya pesa na kuwatoa hofu wateja wao kuwa benki hiyo haina tatizo katika suala zima la utoaji mikopo.

Kukua kwa tekinolojia ya mawasiliano kumerahisisha benki nyingi kutumia miamala ya fedha kwa ATM na Simu baking na KCBL haijapitwa na mfumo huo kwani kupitia Umoja Switch mtandao huo unazo zadi ya  ATMs 200 kwa nchi nzima kupitia huduma ya ushirika Card.

Mfumo huo na ule wa miamala ya kibenki kupitia simu ya kiganjani kwa mteja mwenye akaunti katika benki hiyo ambayo kujiunga kwake ni bure,ni mfumo unaomwondolea usumbufu mteja kusafiri umbali mrefu kwenda benki.

Meneja huyo anaeleza kuwa changamoto inayowakabili ni mtaji mdogo unaochangiwa na kupanuka  kwa shughuli za kibenki pamoja na gharama kubwa za TEKNOHAMA.

Kijazi anasema mipango yao ya baadaye ni kuongeza kiwango cha faida kutoka kwenye uwekezaji mbalimbali,kuongeza wanahisa wapya na kuongeza wateja wapya ndnai na nje ya mkoa wa Kilimanjaro kupitia vituo vya huduma kwa wateja vya benki hiyo.

“Mipango yetu mingine ni kwenda na teknolojia ya kisasa katika utoaji wa huduma zetu  pamoja na kufungua matawi kwenye baadhi ya wilaya zetu na mikoa jirani kama Arusha,Manyara na Tanga”,anasema meneja huyo.

Kwa upande wake meneja mikopo wa KCBL,Janeth Minja anasema hali ya urejesheji wa mikopo ni nzuri kutokana na wakopaji wengi kurejesha kwa wakati huku benki hiyo ikifanya ufuatiliaji kwa baadhi ya wakopaji ambao hawarejeshi kwa wakati.

Meneja huyo anasema kuwa pamoja na urejeshaji wa mikopo kuwa mzuri ipo changamoto kwa baadhi ya wkopaji kutorejesha mikopo yao kwa wakati na baadhi yao  hukimbilia mahamakani kuweka zuio la kuuzwa kwa mali wanazoweka kama dhamana ya mikopo.

Anasema mkakati wa benki hiyo ni pamoja na kufanya jitihada za kuwafuatilia kwa karibu wateja ambao mikopo yao hailipwi ili kuhakikisha wanalipa kwa wakati na kuondokana na usumbufu kwa kukamatwa kwadhamana zao na kuuzwa.

Minja anafafanua kuwa malengo yao ya muda wa kati na muda mrefu ni kuongeza kiasi cha ukopeshaji  katika sekta mbali mbali ikiwamo kilimo,biashara ndogo na kubwa,ujenzi na sekta ya utalii.



Jumanne, 21 Novemba 2017

TRA YAZIFUNGA AKAUTI ZA MAMLAKA YA MAJI MOSHI MJINI MUWSA




RUNGU la mamlaka ya mapato Tanzania(TRA) kufunga akaunti za walipakodi wakorofi  na kukamata mali zao limeikumba  Mamlaka ya Maji safi na maji taka Moshi Mjini(MUWSA) ambako akaunti za mamlaka hiyo zinadaiwa kufungwa.

Kufungwa kwa akaunti za mamlaka hiyo kulikodhibitishwa na mkurugenzi wake Joyce Msiru  ni kutokana na madai kwamba mamlaka hiyo inadaiwa shilingi Bilioni 2.6 ikiwani malimbikizo ya kodi mbali mbali.

Hata hivyo mkurugenzi  huyo wa MUWSA Joyce Msiru anapinga deni hilo akidai baadhi ya kodi zilizoanishwa na TRA hawawezi kuzilipa kutokana na wao(mamlaka) kutojiendesha kibiashara huku akidaia TRA imesisitiza lazima madeni hayo yalipwe.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TRA,kiasi hicho cha deni ni kutokana na ukaguzi uliafanywa kati ya mwaka 2013 hadi mwaka jana ambsalo linahusisha kodi mbali mbali ikiwmao VAT,Corporation tax,Skillls Development Levy na nyinginezo.

Mkurugenzi huyo amesema mamlaka yake haiwezi kulipa kodi ya Coporation tax inayofikia shilingi Milioni 847 kutokana na kile alichodai mamlaka yake haifanyi biashara badala yake inategema mapato kutokana na Ankara za maji kutoka kwa wateja.

“Mfano hiyo kodi ya coporation tax wanayotudai hiyo ni kodi inayolipwa na makampuni au taasisi zinazojiendesha kibiashara lakini sisi MUWSA income yetu inatokana na Ankara za maji zinazolipwa na wateja,sasa hapo sisi tunahusikaje?”,alihoji.

Kuhusu shilingi Milioni 948 ambazo  TRA inaidai MUWSA kama kodi ya ongezeko la thamani(VAT) mkurugenzi hiyo amedai kuwa kuna mkanganyiko mkubwa katika kutafsiri sheria kutokana na kwamba kwenye maji sheria imesamehe VAT lakini kwenye huduma ya majitaka sheria imekaa kimya.

Kodi nyingine ambayo mamlaka hiyo wanadai hawastahili kulipa na ambayo TRA wamesisitiza lazime ilipweni ya Skills Development Levy ambako wanadaiwa shilingi milioni 569.

Akizungumzia kodi hiyo,mkurugenzi huyo anadai kuwa mwaka 2012 TRA waliirejeshea mamlaka hiyo kiasi cha shilingi milioni 39 baada ya kutozwa na mamlaka hiyo katika mwaka 1999 na 2002 na kuhoji iweje kodi hiyo  irejeshwe tena kwa mamlaka yake.

Kutokana na mvutano huo ,mkurugenzi huyo amedai kuwa kwa sasa sakata hilo limepelekwa kwa katibu mkuu wa wizara ya maji,profesa Kitila Mkumbo kwa ajili ya kulitafutia ufumbuzi huku taarifa zikipasha kuwa sakata hilo sasa limeziunganisha wizara mbili,wizara ya maji na wizara ya fedha.

Mbali na kupelekwa huko,mkurugenzi huyo ameliambia Jamhuri kuwa imeundwa timu  itakayoshughulikia madai ya mamlaka za maji kote nchini ambako inadaiwa kuwa zimekuwa zikitozwa kodi na TRA kadri wanavyoona.

“Lengo letu tunataka kuwe na mfumo unaoeleweka wa utozwaji kodi kwa mamlaka zote nchini tofauti na sasa ambako utasikia mamlaka hii wanatozwa kodi fulani,sasa huu mkanganyiko tunataka tuumalize”,alisema.

Kutokana na kufungwa kwa akaunti za mamlaka hiyo,wafanyakazi kadhaa wa mamlaka hiyo walijawa na hofu ya kukosa mishahara yao ya mwezi oktoba lakini taarifa zilizopatikana baadaye na kudhibitishwa na mkurugenzi huyo,TRA imeregeza kamba na kuzifungua huku ikitishiak uzifunga tena kama hakitaeleweka.

WADAIWA SUGU MUWSA NAO KUKIONA CHA MOTO

Wakati Mamlaka hiyo ikitikiswa kwa akaunti zake kufungwa na TRA na baadaye kufunguliwa kwa masharti,mkurugenzi huyo amesema kuwa,mamlaka yake bado inasaka dawa ya kuondoka na wadaiwa sugu wa mamlaka hiyo.

Amesema hadi sasa wanazidai taasisi za serikali ikiwamo ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro,Chuo cha taaluma ya polisi(MPA) na Magereza mkoa zaidi ya shilingi Bilioni 1.7.

Amesema pamoja na kuzikatia huduma ya maji taasisi hizo na baadaye kuzirejeshea huduma hiyo,hakuna dalili zozote za kulikwa kwa malimbikizo hayo ya Ankara za maji kutokana na wakuu wa taasisi hizo kudai hawana pesa.

“Tunaona suluhisho la yote haya ni kuwafungia mita za maji ili  kubaini kiwango cha matumizi yao na sasa tupo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato huo na tunaamini tukifanya hivyo tutakuwa tumekata mzizi wa fitina”,alisema.

Mara kwa mara mamlaka hiyo imekuwa ikichukua hatua za kusitisha huduma ya maji safi kwa taasisi hizo za serikali kutokana na ukubwa wa malimbikizo ya madeni hayo lakini huishia kuendelea kutoa huduma kutokana na unyeti wa taasisi hizo.



BREAKING NEWS,JENGO LA CLOUDS FM LASHIKA MOTO MCHANA HUU



Jengo la kituo cha Radio na Luninga cha  Clouds Fm Jijini Dar es salaam limeshika moto mchana huu wa leo.
 
Taarifa kutoka eneo la tukio zinapasha kuwa,sehemu kubwa ya jengo la kituo hicho  cha Chouds Media Group linaungua moto huku  juhudi za kuuzima moto huo bado zinaendelea.

  Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana

Kutokana na mkasa huo,matangazo ya radio pamoja na Televisheni yamesitishwa kwa muda hadi hapo hali ya mambo itakapokuwa imetengemaa

Taarifa zaidi zinaendelea kuja........