Na Charles Ndagulla,Moshi
MIKOPO yenye riba kubwa na masharti
magumu katika upatikanaji wa mikopo kwenye mabenki mengi hapa nchini imekuwa ni
kikwazo kikubwa kwa wakulima wengi hasa wadogo wadogo hali ambayo imechangia
wengi wao kuishi maisha ya dhiki.
Hii inatokana na mabenki mengi
kujiendesha kibiashara zaidi kwa kutoza riba kubwa pamoja na masharti magumu
katika upatikanaji wa mikopo kwa wakulima ambao wengi hawana mali zinazoweza
kuwekwa kama dhamana ya mkopo.
Benki ya ushirika mkoani
Kilimanjaro(KCBL)iliyopo mjini moshi imeweza kuliona hilo na kujikita katika
utoaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima wadogo wadogo lengo ni
kuwawezesha kuboresha maisha yao.
Mikopo hiyo inalenga kuwawezesha
wakulima kukusanya mazao hususani zao la kahawa kupitia mfumo wa
stakabadhi ya mazao ghalani ambao unatajwa kama mfumo bora na rafiki kwa
wakulima wa zao la kahawa .
Benki hii ya ushirika ilisajiliwa
kama chama cha ushirika mwaka 1994 kabla ya mwaka 1995 kupata leseni ya
kutoa huduma za kibenki ambako mwaka uliofuata yaani 1996 huduma za kibenki
zilianza rasmi.
Meneja Mkuu wa Benki hiyo,Joseph
Kingazi anasema mpaka sasa benki hiyo inao wanahisa 245 ambao ni vyama vya
ushirika wa mazao (AMCOS),vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo(SACCOS) pamoja
na watu binafsi wapatao 307.
Anasema wazo la kuanzishwa kwa benki
hiyo kulitokana na mawazo yaliyotolewa na vyama vya ushirika wa
mazao(AMCOS)mkoani Kilimanjaro ili kuweza kupata mikopo yenye riba na masharti
nafuu katika kukusanya mazao yao.
“Lengo kuu la kuanzishwa kwa benki
hii ilikuwa kuwasidia wakulima wadogo wadogo kuweza kupata mikopo yenye riba na
masharti nafuu tofauti na mabenki mengine katika ukusanyaji wa mazao hususani
zao la kahawa kupitia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani”,anasema kingazi.
Meneja huyo anataja mafanikio sita
ambayo benki hiyo imepata tangu kuanzishwa kwake miaka 20 iliyopita ikiwa ni
pamoja na kuwafikia wateja zaidi ya 762,177 katika mkoa wa Kilimanjaro na mikoa
mingine iliyo jirani na mkoa huo .
Mafanikio menigne ni kuwa benki ya
ushirika ya kwanza nchini inayomilikiwa na wazalendo kwa aslimia 100 huku
ikitoa mikopo kwa wakulima wa zao la kahawa yenye thamani ya ya shilingi
Bilioni 28 hadi kufikia msimu wa kilimo wa 2016/17.
“KCBL imekuwa mwanzilishi wa mfumo
wa stakabadhi ya mazao ghalani toka mwaka 1999 na kwa sasa mfumo huu umeweza
kuenea na kutumika sehemu mbali mbali hapa nchini hasa kwenye mazao ya
pamba,korosho na mazao mengine”,anasema.
Kwa mujibu wa meneja huyo,uwepo wa
benki hiyo umekuwa kimbilio kwa wakulima wengi hatua ambayo imekuwa chachu kwa
wakulima hao kuboresha maisha yao huku wanahisa na wateja wa kawaida wakipewa
mafunzo mbalimbali kupitia kwa wataalam wa benki hiyo.
Anasema tangu kuanza kwa mfumo wa
stakabadhi ya mazo ghalani,KCBL imeweza kumsaidia mkulima kutoka kukopwa mazao
yake na kupata malipo kwa wakati huku mfumo huo ukivisaidia vyama vya msingi
vya ushirika kujitegemea katika kununua mazao.
“Mfumo huo pia umevisaidia vyama vya
msingi vya ushirika kujitengenezea mfuko wake wa ndani kwa ajili ya kununua
mazao msimu bubu unapoanza tofauti na miaka ya nyuma kabla ya mfumo
haujaanza”,anasema.
Kwa upande wa wakulima meneja huyo
anasema kuwa mfumo huo umechangia kuwahamasisha wakulima kulima kahawa kwa
wingi kutokana kutokana na kupata malipo kwa wakati pale anapoleka mazao yake
chamani.
Ametaja faida nyingine wanayopata
wakulima kutokana na mfumo hiuo wa stakabadhi ya mazao ghalani kuwa ni pamoja
na kupanda kwa bei ya kahawa kila msimu,kupanda kwa ubora wa mazao .
“Pia mkulima amefaidika kutokana na
kupata faida kwenye fedha za kigeni (Foreign Exchange Gain) pamoja na
kupata riba nafuu ikilinganishwa na wateja wengine”.anasema.
Anasema mikakati yao ya baadaye
katika kuhakikisha wakulima wa zao la kahawa wananufaika na mfumo wa stakabadhi
ya mazao ghalani ni pamoja na kuuboresha mfumo huo ili wakulima waweze kuutumia
vizuri.
Mikakati mingine ni kutoa elimu na
semina kwa wakulima kwenye kilimo cha kisasa cha kahawa,elimu juu ya tabia
yakujiwekea akiba pamoja na kutoa mafunzo kwa watendaji wa vyama vya msingi vya
ushirika .
Kupitia mfumo huo wa stakabadhi ya
mazao ghalani,KCBL imeweza kutoa mikopo kwa ajili ya makusanyo ya kahawa na
zaidi ya aslimia 75 ya kahawa yote ya mkoa wa Kilimanjaro imefadhiliwa na
benki hiyo.
Mpaka sasa benki hiyo inatoa huduma
zake katika wilaya zote saba za mkoa wa Kilimanjaro ambazo ni
Same,Mwanga,Rombo,Moshi Vijijini,Hai Siha na Moshi mjini na mkoa wa Arusha.
“Tunatoa huduma zaidi vijijini
kupitia vyama vya msingi vya ushirika na kumfikia mtu/mkulima wa chini
kabisa,pia tumefungua kituo cha huduma kwa wateja katika wilaya ya Rombo eneo
la Tarakea Kibaoni”,anasema.
Licha ya baadhi ya benki
kuyumba katika utoaji wa mikopo kutokana na serikali kupitisha uamuzi wa
kuzihamishia akaunti zote za serikali benki kuu,KCBL haijaguswa na hali hiyo
kutokana na kutokuwa na fungu lolote toka serikalini.
Kwa mujibu wa meneja huyo wa benki
ya ushirika,benki yake imekuwa ikitegemea akiba za wateja wao katika kufanya
biashara ya pesa na kuwatoa hofu wateja wao kuwa benki hiyo haina tatizo katika
suala zima la utoaji mikopo.
Kukua kwa tekinolojia ya mawasiliano
kumerahisisha benki nyingi kutumia miamala ya fedha kwa ATM na Simu baking na KCBL
haijapitwa na mfumo huo kwani kupitia Umoja Switch mtandao huo unazo zadi
ya ATMs 200 kwa nchi nzima kupitia huduma ya ushirika Card.
Mfumo huo na ule wa miamala ya
kibenki kupitia simu ya kiganjani kwa mteja mwenye akaunti katika benki hiyo
ambayo kujiunga kwake ni bure,ni mfumo unaomwondolea usumbufu mteja kusafiri
umbali mrefu kwenda benki.
Meneja huyo anaeleza kuwa changamoto
inayowakabili ni mtaji mdogo unaochangiwa na kupanuka kwa shughuli za
kibenki pamoja na gharama kubwa za TEKNOHAMA.
Kijazi anasema mipango yao ya
baadaye ni kuongeza kiwango cha faida kutoka kwenye uwekezaji
mbalimbali,kuongeza wanahisa wapya na kuongeza wateja wapya ndnai na nje ya
mkoa wa Kilimanjaro kupitia vituo vya huduma kwa wateja vya benki hiyo.
“Mipango yetu mingine ni kwenda na
teknolojia ya kisasa katika utoaji wa huduma zetu pamoja na kufungua
matawi kwenye baadhi ya wilaya zetu na mikoa jirani kama Arusha,Manyara na
Tanga”,anasema meneja huyo.
Kwa upande wake meneja mikopo wa
KCBL,Janeth Minja anasema hali ya urejesheji wa mikopo ni nzuri kutokana na
wakopaji wengi kurejesha kwa wakati huku benki hiyo ikifanya ufuatiliaji kwa
baadhi ya wakopaji ambao hawarejeshi kwa wakati.
Meneja huyo anasema kuwa pamoja na
urejeshaji wa mikopo kuwa mzuri ipo changamoto kwa baadhi ya wkopaji
kutorejesha mikopo yao kwa wakati na baadhi yao hukimbilia mahamakani
kuweka zuio la kuuzwa kwa mali wanazoweka kama dhamana ya mikopo.
Anasema mkakati wa benki hiyo ni
pamoja na kufanya jitihada za kuwafuatilia kwa karibu wateja ambao mikopo yao
hailipwi ili kuhakikisha wanalipa kwa wakati na kuondokana na usumbufu kwa
kukamatwa kwadhamana zao na kuuzwa.
Minja anafafanua kuwa malengo yao ya
muda wa kati na muda mrefu ni kuongeza kiasi cha ukopeshaji katika sekta
mbali mbali ikiwamo kilimo,biashara ndogo na kubwa,ujenzi na sekta ya utalii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni