Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani ndiyo hifadhi kongwe
kuliko hifadhi asilia zote nchini, Hifadhi hii ilitangazwa rasmi kwenye gazeti
la Serikali mwaka 1997. Hifadhi hii ipo katika Wilaya za Muheza na Korogwe umbali
wa kilomita 64 kutoka Jijini Tanga.
Amani yenye ukubwa wa hekta 8,380 ni moja kati ya maeneo ya
mfano yaliyohifadhiwa vizuri nchini kwa kutumia mfumo wa Uhifadhi Shirikishi
baina ya Serikali na wananchi wanaoishi na kuzunguka katika hifadhi hiyo.
Akizungumza na Ndagullablog, Afisa Misitu Mkuu wa Hifadhi hiyo,
Angyelile Sousa alisema, Serikali kupitia Wakala wake wa Huduma za Misitu (TFS)
imewekeana Makubaliano ya kuhifadhi Msitu huo na vijiji 21 vinavyozunguka
hifadhi hiyo. Vijiji vinne kati ya hivyo ambavyo ni Shebomeza, Mlesa, Chemka na
Mikwinini vimo ndani ya Hifadhi hiyo Asilia.
Sousa alisema katika mfumo huo kila kijiji kimeunda kamati
ya uhifadhi wa mazingira ambazo zinashirikiana kwa karibu na uongozi wa hifadhi
hiyo kwenye shughuli za uhifadhi ikiwemo ulinzi wa rasilimali zilizomo.
Alisema kuwa makubaliano hayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa na
manufaa makubwa kwa kuwa wananchi wa vijiji hivyo wameelimishwa na kuuelewa
umuhimu wa hifadhi hiyo ambayo ina faida kubwa kwao, kwa Serikali na kwa wananchi
wote wa Mkoa wa Tanga.
Aliongeza kuwa mfumo huo umesaidia kuimarisha uhifadhi
katika Msitu huo ambapo matukio ya moto yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa ikiwa
na pamoja na shughuli za uharibifu wa mazingira kwa ujumla.
Akielezea faida za hifadhi hiyo alisema, Amani ni chanzo
kikuu cha Maji yanayotumika katika Jiji la Tanga ambapo vyanzo vyake vinapeleka
maji katika mto Zigi unaopeleka maji hayo Jijini humo. Vijiji vyote 21
vinavyozunguka hifadhi hiyo pia vinanufaika na maji hayo.
Alisema kuwa faida nyingine inayopatikana katika hifadhi
hiyo ikiwa ni sehemu ya makubaliano kwenye uhifadhi shirikishi ni mchango wa
asilimia 20 ya mapato yanayotokana na utalii ambayo yanatolewa kwa vijiji 21
vinavyopakana na hifadhi hiyo kwa ajili ya kusaidia katika shughuli za
maendeleo za vijiji hivyo.
“Katika sehemu ya makubaliano hayo wananchi wa vijiji jirani
wanaruhusiwa kuokota kuni kavu zinazopatikana katika hifadhi hiyo, matunda,
mbogamboga pamoja na dawa za miti shamba. Wananchi hao wanaruhusiwa kuingia hifadhini
kwa umbali wa mita 100 kutoka maeneo yao ya vijiji kwa ajili ya shughuli hizo”
alisema Sousa.
Aliongeza kuwa watu binafsi pia wananufaika na hifadhi hiyo
kwa kuwekeza katika mahoteli yanayowapatia kipato. Wananchi pia wanaotembeza
watalii katika hifadhi hiyo wananufaika na ajira ambapo huchukua asilimia 60 ya
mapato ya kutembeza watalii (Tour
Guiding Fees), asilimia 20 ikibaki hifadhini na
asilimia 20 nyingine ikienda kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.
Akizungumzia vivutio mbalimbali vilivyomo katika hifadhi
hiyo, Sousa alisema kuna vivutio vingi vya utalii vilivyohifadhiwa vizuri
ikiwemo Misitu ya Asili na Wanyama mbalimbali kama vile Kima wa Bluu (Blue Monkey), Mbega
Weupe na Weusi (Black and White Collabus), Nyoka, vinyonga pembe tatu (Three Hornes Chamelleon), vipepeo na ndege wa aina mbali mbali ambao baadhi yao
husafiri umbali mrefu kutoka barani ulaya kwa ajili ya kukimbia baridi kali na
kuzaliana katika hifadhi hiyo.
“Vivutio vingine vilivyopo katika hifadhi hii ni Maporomoko ya
Maji (Water Falls) ambayo ni Derema, Chemka, Ndola na Pacha. Pia kuna vivutio
vya Vilele vya Milima (viewpoints) kama Kiganga, Ngua, Makanya, Mbomole na Kilimahewa.
Ukiwa katika vilele hivyo unaweza kuona Mji wa Korogwe na Jiji la Tanga kwa
juu” alisema.
Mbali na vivutio hivyo, alisema kivutio kingine ambacho ni
cha kipekee katika hifadhi hiyo ni aina ya Ua linaloitwa “Saintpaulia” ambalo
lina rangi ya Zambarau “Violeth Color”, Ua hilo pia linatumika kama nembo ya hifadhi hiyo. Upekee
wa Ua hilo ni kwamba likipandwa sehemu nyingine yeyote duniani hubadilika rangi
yake ya asili, Tafiti mbalimbali zimefanywa ikiwemo kujaribiwa kupandwa nchini
Ujerumani na kutoa majibu hayo hayo.
Pamoja na vivutio hivyo kivutio kingine katika hifadhi hiyo
ni mashine ya kusagia unga iliyokuwa ikitumia nishati ya nguvu ya kusukumwa na
maji miaka 1986 katika kijiji cha Kisiwani na mtambo wa kuzalisha umeme kwa
kutumia nishati hiyo hiyo iliyotumiwa na Wakoloni wa Kijerumani katika Kijiji
cha Chemka.
Akizungumzia aina za utalii katika hifadhi hiyo alisema, upo
Utalii wa Picha (Photography), Utalii wa Kutizama Ndege (Bird Watching),
Utalii wa Kuangalia viumbe hai Usiku (Night
Watching), Utalii wa Kiutafiti (Reseach Tourism),
Utalii wa kiutamaduni (Cultural
Tourism) na Utalii wa Kutembea na Kupanda
Milima.
“Kwa upande wa gharama za kutembelea hifadhi ya Amani kama
kiingilio kwa Mtalii mmoja kutoka nje ya nchi ni Dola 10 za Kimarekani na
Mtanzania ni Shilingi10,000. Kwa upande wa gharama za watembeza watalii wa nje
ni dola 15 za Kimarekani” alisema.
Nae Afisa Misitu wa Hifadhi hiyo, Isack Bob Matunda
akizungumzia idadi ya watalii waliotembelea hifadhi hiyo na mapato
yaliyopatikana alisema “Mwaka wa fedha 2015/16 jumla ya watalii 545
walitembelea hifadhi hii na jumla ya mapato yote yaliyopatikana ni shilingi
milioni 50. Aidha, mwaka huu wa fedha 2016/17 mwezi Julai-Agosti jumla ya
watalii 121 wameshatembelea hifadhi hii na mapato ambayo yameshapatikana ni
shilingi milioni 7.3”.
Akielezea changamoto za uhifadhi, Afisa Misitu Mkuu wa
Hifadhi hiyo, Angyelile Sousa alisema zipo changamoto kidogo ikiwemo uchimbaji
wa madini kwenye vyanzo vya maji, uharibifu mdogo wa misitu ikiwa ni pamoja na
uchomaji moto katika ukanda wa chini na miundombinu mibovu ya barabara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni