Jumatatu, 20 Novemba 2017

MATUMIZI YA KAHAWA NI TIBA ASILI KWA MWILI WA BINADAMU



 
Habari njema ni kuwa kahawa ina mchango mkubwa katika kuzuia magonjwa ya moyo ikiwemo shambulio la moyo na kuziba kwa mishipa ya damu iliyopo kwenye ubongo. 

Kutokana na mtindo wa maisha na ulaji wa vyakula usiozingatia lishe bora, idadi ya watu wanaokumbana na magonjwa ya moyo na kiharusi inaongezeka. 

Ili kukabiliana na hatari ya kushambuliwa kwa moyo; kiungo muhimu kwa uhai wa binadamu wataalamu wa afya wanashauri watu kunywa kahawa angalau vikombe 2 hadi 6 kwa siku ili kujiweka katika nafasi ya kuruhusu mzunguko wa damu na hewa ya oksijeni mwilini. 

Kwa muda mrefu wataalamu wa afya wamekuwa wakifanya tafiti kubaini sababu na njia za kuzuia shambulio la moyo na kupata kiharusi, lakini baadhi ya watafiti waliamua kuafanya uchambuzi na mchanganuo wa tafiti zilizofanywa ili kubaini njia ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu katika kupambana na magonjwa ya moyo. 

Watafiti kutoka Chuo Kikuu Cha Colorado Kitengo Cha Afya wamechanganua data za utafiti wa moyo uliowahusisha wakazi 15,000 wa Framingham nchini Marekani ambao walikuwa wanaangalia mahusiano yaliyopo ya ulaji wa vyakula na utendaji wa moyo tangu mwaka 1940. 

Walijikita zaidi kuangalia sababu zisizojulikana za kupata  kiharusi na shambulio la moyo ambalo hupelekea moyo kushindwa kufanya kazi. 

 Wamebaini  kuwa unywaji wa kahawa unahusishwa kupunguza hatari ya kupata shambulio la moyo na kiharusi (stroke). Kila kikombe cha kahawa kinachotumiwa kila siku kinapunguza matatizo hayo kwa asilimia 5 hadi 7  ikiwa mtu atakunywa hadi vikombe sita kwa siku. 

Utafiti wa awali ambao uliwasilishwa katika Taasisi ya Moyo ya Aneheim iliyopo California Marekani ni muendelezo wa tafiti mbalimbali ambazo zinaelezea faida ya kahawa kwa moyo wa binadamu. 








 Kahawa iliyoiva ikiwa tayari kwa mavuno,inatajwa kama tiba asili kwa mwili wa binadamu.



Walitumia njia ya kitaalamu inayojulikana kama mashine ya kujifunzia (machine learning) ambayo inafuatilia takwimu za muda mrefu juu ya matatizo ya moyo na vyakula ambavyo watu walikuwa wanatumia na athari za kiafya zinazohusiana na moyo. Njia hii ni sahihi kwa sababu inaangazia namna watu walivyokuwa wanaishi ikilinganishwa na maisha ya watu wa sasa. 

“Katika hali halisi ya dunia, tulikuwa na uwezo wa kutabili magonjwa ya shambulio la moyo na kiharusi kwa uhakika wa 100% muda mrefu kabla ya tukio kutokea”, anasema Mwandishi Laura Stevens akihojiwa na jarida la TIME. 

“Changamoto iliyopo hapa ni kuwepo kwa sababu nyingi hatarishi, kuzijaribu zote kwa kutumia njia za asili tungetumia muda mrefu na haiwezekani”, amesema Laura. 

Katika uchambuzi huo wa tafiti wamebaini kuwa kahawa ina mchango mkubwa wa kupunguza hatari ya kupata kiharusi na shambulio la moyo.  Kahawa inasaidia kutanua mishipa ya damu inayoingia na kutoka kwenye moyo n aubongo ili kusafirisha damu vizuri bila kizuizi.

 Karibu wanywaji wote wa kahawa (97%) waliowekwa kwenye majaribio walitumia kikombe 1 hadi 6 kwa siku na watafiti hao hawana uhakika kama faida hizo zinaweza kuendelea ikiwa kiwango cha matumizi kitaongezeka. 

 Na wamegundua kuwa hata kama mtu alikunywa au hakunywa kahawa iliwasaidia kubashiri sababu hatarishi za kupata kiharusi na shambulio la moyo.

Pia uchambuzi  ulitumia sampuli ya wanywaji wa kahawa wakihusianisha na sababu hatarishi umri wa kuishi, shinikizo la damu na mafuta katika mwili wa binadamu, majaribio hayo yalionyesha kuwa kahawa inaweza kupunguza hatari hiyo kwa 4%.

Watafiti hao walithibitisha matokeo ya utafiti kwa kupitia na kuchambua tafiti nyingine mbili zinazohusu Utendaji wa mishipa ya damu inayoingia kwenye moyo na  kuziba kwa mirija ya damu iliyopo kwenye moyo. 

 Hata hivyo, imebainika kuwa kahawa ina faida nyingi kwa afya ya binadamu ikiwa itatumiwa kwa kiwango kizuri. Utafiti huo umebainisha wazi kuwa mashine ya kujifunzia inaweza kuwasaidia watafiti kutambua sababu nyingine hatarishi zinazosababisha na kuzuia magonjwa ya moyo.

Stevens anasema timu yake inakusudia kutumia uchambuzi huo kugundua muunganiko wa kafeini inayopatikana kwenye kahawa kama ina uhusiano wa afya ya moyo iliyoangaliwa kwenye utafiti. 

“lengo letu la msingi ni kutambua kama matumizi ya kahawa ni sehemu inayotumiwa na kliniki katika kutathmini njia ya kuzuia vihatarishi vya magonjwa ya moyo” amesema, “na kama mabadiliko ya matumizi ya kahawa au kafeini yanaweza kuwa njia ya kubadilisha vihatarishi”.
 
Dalili mojawapo ya shambulio la moyo ni maumivu ya kifua

 Shambulio la Moyo ni nini?
 
Shambulio la moyo ni kufa kwa sehemu ya misuli ya moyo ambayo husababishwa na damu kuganda katika mishipa inayosafirisha damu kwenye moyo. Ikiwa baadhi ya misuli ya moyo itakufa, mtu husikia maumivu ya kifua na mapigo ya moyo kutokuwa ya kwaida. 

Sababu zinazosababisha Shambulio la Moyo
 
Hatari ya mtu kupata shambulio la moyo huongezeka ikiwa mwanaume amevuka umri wa miaka 45 na mwanamke amevuka miaka 55. Pia kupungua kwa hewa ya oksijeni katika mzunguko wa damu, uvutaji wa sigara na unene uliopitiliza ni sababu zinazo changia shambulio la moyo.
  
Ugonjwa wa Kisukari na mafuta mengi mwilini ambayo ni matokeo ya ulaji wa vyakula vyenye mafuta, upasuaji wa moyo na shinikizo kubwa la damu. Watu wenye virusi vya UKIMWI na msongo wa mawazo unaotokana kazi. 

Mara nyingi shambulio la moyo linapotokea, linasababishwa mjumuiko wa sababu mbalimbali kuliko sababu moja.  
         
Baadhi ya dalili ni kuchoka na kuishiwa nguvu, maumivu ya kifua ambayo hushuka hadi kwenye mkono na sehemu ya nyuma ya mgongo, hofu, kutapika, kukosa pumzi na kutokwa na jasho.           




Maoni 2 :

  1. Shambulio la moyo nimeeelewa sana eneo hilo mwandishi, wengi wanajikuta kuwa na maumivu makali ya kifua na wanabaki kukinyamazia hadi kinaleta maradhi ambayo inakuwa ngumu kutibika. Hata mchezaji wa zamani wa Rwanda na Vital'O Hamad Ndikumana naye alikuwa na maumivu makali ya kifua hadi kifo chake cha ghafla. Asante kwa ujumbe

    JibuFuta
  2. Picha unaweza kuifanya ikiwa kubwa badala ya kuiweka saizi ndogo kama ulivyoweka. Wakati unaposti kwenye Editorial kule una iclick picha husika kuna maneno yatatokea small, large, x-large na original size sasa chaguo zuri ni X-Large. Asante Ndagulla blog.

    JibuFuta