Uamuzi wa mahakama ya juu wa
kuidhinishwa kwa ushindi wa rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Oktoba 26
umezua maandamano ya ghasia katika maeneo yanayodaiwa kuwa ngome za upinzani
nchini Kenuya.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation
wafuasi wa kiongozi wa muungano wa Nasa Raila Odinga waliandamana ili kuonyesha
kutoridhishwa kwao na uamuzi huo.
Maandamano hayo yalibadilika na kuwa
ya ghasia katika maeneo kadhaa ya Nyanza, nyumbani kwa Odinga , katika maeneo
ya Kibira na Mathare mjini Nairobi.
Mjini Kisumu, gari moja la kibinafsi
lilichomwa katika eneo la Kondele muda mfupi baada ya ghasia kuzuka katika mji
huo wa ziwa Victoria kufuatia uamuzi huo wa mahakama.
kulingana na gazeti hilo vijana
walifunga barabara zinazoelekea mjini Kisumu kwa kuchoma magurudumu ya gari na
mawe.
Waliwazuia watu watatu waliokuwa
katika gari hilo la kibinafsi , wakawapiga na kuwaibia kabla ya kuliharibu gari
hilo na kulichoma.
Watatu hao walikimbilia katika kituo
cha polisi cha kondele wakihofia maisha yao.
Raila Odinga: Hatutambui ushindi wa Uhuru Kenyatta
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amezungumzia kuhusu uamuzi uliotolewa na mahakama ya juu wa kuidhinisha uchaguzi wa Uhuru Kenyatta.Kulingna na gazeti la daily Nation, Bwana Odinga kupitia taarifa iliotolewa na mshauri wake Salim Lone, amesema kuwa serikali ya Jubilee sio halali akiongezea kwamba uamuzi huo wa mahakama ya juu ulifanywa kupitia shinikizo.
''Sisi watu wa Nasa tayari, tulikuwa tumeamua kabla ya uamuzi wa mahakama kwamba hatuitambui serikali ya Uhuru Kenyatta'', alisema.
''Uamuzi huo haujabadilishwa na uamuzi wa mahakama ya juu ambao haukutushangaza. Ni uamuzi uliotolewa chini ya shinikizo kubwa ,hatushutumu mahakama tunaihurumia''.
Ushindi wa rais Uhuru Kenyatta mnamo mwezi Oktoba 26 uliidhinishwa na mahakama hiyo kupitia uamuzi wa pamoja wa majaji sita wa mahakama ya juu.
Kulingana na gazeti hilo bwana Lone amedai kwamba mahakama ilikutana chini ya shinikizo kubwa, baada ya kushindwa kukutana kutokana na wasiwasi mkubwa wa kiusalama kufuatia kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa dereva wa naibu jaji mkuu kabla ya kusikizwa kwa kesi ya uchaguzi wa tarehe 26 Oktoba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni