TAASISI ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), imewafikisha mahakamani Daktari wa Hospitali
ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi Dkt. Deogratias Godfrey Urio pamoja na
Muuguzi wa Hospitali hiyo, Naomi Shayo kwa kosa la kuomba na kupokea Rushwa ya
shilingi 150,000.
Washitakiwa hao
walifikishwa mahakamani hapo jana Ijumaa mbele ya hakimu mkazi ,Pamela
Meena na kusomewa mashitaka na wakili na
mwendesha mashitaka wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro,Barry Galinoma akisaidiwa na Caroline Lugenge.
Katika shauri
hilo la jinai namba 2/2017 ,washitakiwa hao
wanashitakiwa chini ya kifungu cha 15
kifungu kidogo cha kwanza A na kifungu kidogo cha pili cha sheria namba 11 ya kupambana na rushwa ya
mwaka 2007.
Kwa mujibu wa
hati ya mashitaka iliyosomwa na mawakili hao wa Takukuru,washitakiwi hao wanadaiwa
kuwa kati ya Novemba 10 na 15 mwaka huu kwa pamoja wakiwa watumishi wa Serikali
katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi walidai rushwa kiasi
cha shilingi 150,000.
Wanadaiwa kuomba
kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Stanley
Samson ili waweze kumfanyia upasuaji wa uvimbe katika kizazi ndugu yake aitwaye
Lightness Samson, huku wakitambua kuwa ni kinyume na sheria.
Galinoma alidai
kuwa, kosa la pili linamhusu mshitakiwa wa kwanza ambaye ni Dkt. Deogratias
Godfrey Urio ambapo alitenda kosa hili kinyume na kifungu cha 15 kifungu kidogo cha kwanza A na kifungu
kidogo cha pili cha sheria ya
kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Ilidaiwa
mahakama hapo kuwa mshitakiwa wa kwanza Daktari Urio akiwa katika baa ya Mombasa High way iliyopo Mji Mdogo wa Himo akiwa kama
mwajiriwa wa Katibu Tawala mkoa wa Kilimanjaro, na kama Daktari wa Hospitali ya
Mawenzi alipokea kiasi cha shilingi 150,000/- kama rushwa kutoka kwa Stanley
Samson kwa ajili ya kumfanyia upasuaji wa uvimbe katika kizazi ndugu yake
aitwaye Lightness Samson.
Baada ya
kusomewa mashitaka yao,washitakiwa wote walikana mashitaka yao, ambapo upande wa
Jamuhuri ulieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na kuomba kupangiwa
tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Washitakwia waliachiliwa kwa dhamana baada ya kutimiza
masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na watakaosaini fungu la dhamana ya shilingi
milioni moja kila mmoja,kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Desemba 18 mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni