Ijumaa, 10 Novemba 2017

MKAKATI WA KUZALISHA KAHAWA UMEKWAMA



Na Charles Ndagulla,Moshi

MWAKA 2011,serikali kuu kupitia  bodi ya kahawa nchini(TCB) iliweka mkakati wa miaka 10 wa kuendeleza tasnia ya kahawa(Coffe Industry  Development Strategy,2011-2021) kwa lengo la kuendeleza kilimo cha zao hilo nchini kwa kushirikiana na wadau mbali mbali katika sekta hiyo.

Lengo la mkakati huo ilikuwa ni  kuongeza uzalishaji,tija na ubora wa kahawa na kuboresha mapato katika mnyororo wote wa thamani hususani wakulima wa kahawa  na  kuwezesha kahawa ya Tanzania kupata bei nzuri kwenye soko la dunia.

Hata hivyo mkakati huo umekwama kutokana na changamoto kadha za uzalishaji ikiwamo tija ndogo ya uzalishaji inayochangiwa na matumizi kidogo ya pembejeo hususani mbolea .

Mkakati huo ulilenga kuongeza uzalishaji wa kahawa safi kwa mwaka  kutoka tani 50,000  hadi kufikia tani laki moja ifikapo mwaka 2021 lakini hadi kufikia msimu wa 2016/2017 uzalishaji wa kahawa ulikuwa tani 46,963.5.

Sababu nyingine zilizokwaza mkakati huo zinatajwa kuwa ni kasi ndogo ya kupokea matokoeo ya utafiti,mabadiliko ya tabianchi yanayaodaiwa kusababisha mvua zisizo na mpangilio pamoja na uwekezaji mdogo ikilinganishwa na malengo ya mkakati huo.

Uchunguzi wa jamhuri umebaini kuwa,katika misimu saba iliyopita uzalishaji wa zao la kahawa nchini umekuwa ukipanda na kushuka huku baadhi ya wakulima wakidaiwa kulipa kisogo zao hilo na kugeukia mazao mseto kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na bei ndogo.

Katika msimu wa 2010/2011 uzalishaji wa kahawa ulikuwa tani 56,790.0 lakini msimu uliofuata wa 2011/2012 uzalishaji ulishuka kwa kasi ya kutisha na kufikia tani 33,086.7 na ulipanda tena msimu wa 2012/2013 na kufikia tani 71,319.1.

Msimu wa 2013/2014 tani 48,761.9 zilizalishwa na tani hizo zilishuka tena msimu wa 2014/2015 na kufikia 42,768.0 na kupanda tena katika msimu wa 2015/2016 hadi tani 60,188.0 kabla ya kuporomoka msimu wa 2016/2017 hadi tani 46,963.0.


Kaimu mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo anasema utazalishaji wa kahawa katika msimu wa 2017/2018 unatarajiwa kushuka kutoka tani 46,963.0 hadi kufikia tani 43,000.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni