DAR ES SALAAM
Baada ya Mahakama kumkuta Msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’ na hatia ya kuua bila kukusudia na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, Wakili wa Msanii huyo, Peter Kibatala amesema wanakusudia kukata rufaa ili kumsaidia mteja wake.
Hukumu hiyo imetolewa mapema leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo Lulu amekutwa na hatia ya kumuua bila kukusudia Msanii mwenzake marehemu Steven Kanumba mwaka 2012 maeneo ya Sinza, Dar es Salaam.
Muda mfupi baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Kibatala amesema wamepokea hukumu hiyo lakini utaratibu wa kukata rufaa unafanyika ili kumnusuru mteja wake, ambapo ushahidi wa mazingira ndio umemtia hatiani mshtakiwa kwasababu yeye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu wakati tukio hilo linatokea.
“Kwa kifupi ni kwamba tutakata rufaa, wakati rufaa inaandaliwa tutaomba dhamana mchakato wake ni wa kisheria”, amesema Wakili Kibatala.
Elizabeth Michael kwa mara ya kwanza alipelekwa Mahakama ya Kisutu iliyopo Dar es salaam, akishtakiwa kuua bila kukusudia tarehe 7 mwaka 2012, wakati huo akiwa chini ya umri wa miaka 18, ambapo leo amesomewa hukumu ya kufungwa jela miaka 2.
Kabla ya kusoma hukumu hiyo, Jaji
Sam Rumanyika aliIeleza kuwa Mahakama imetoa hukumu hiyo kwa kuzingatia
ushahidi wa mazingira kwasababu hakukuwepo na ushahidi wa moja kwa moja wa
kuhusika na mauaji ya marehemu Kanumba.
"Ushahidi wa mazingira ni
ushahidi ambao mstakiwa alikubali kwamba yeye ni mtu wa mwisho kuwa na
marehemu ambapo mshtakiwa alikuwa na Uhusiano wa kimapenzi na marehemu kwa
miezi minne"
“Ushahidi wa mazingira unaweza
kutumika kama msingi pekee wa kumtia hatiani mshtakiwa tena mshtakiwa pekee,
Sasa ninapokwenda kuangalia maelezo ya mshtakiwa kama yanakidhi vigezo
nilivyosema awali". Ameeleza Jaji Rumanyika.
Aidha Jaji Rumanyika amesema
ameridhishwa na ushaidi wa mashaidi wanne wa upande wa mashtaka na amemtia
hatiani Elizabeth maarufu kama ‘Lulu’ chini ya kifungu cha Sheria cha 195 cha
sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Ushahidi wa Mazingira ni nini?
Mtaalamu wa Sheria, Gilbert Daudi
kutoka mkoa wa Kigoma anasema ushahidi wa mazingira ni ushahidi wa nyongeza
ambao unatumika sambamba na ushahidi wa moja kwa moja. Anaeleza kuwa,
“Ushahidi wa kimazingira ni
kwamba tukio limetokea sehemu fulani, mtu amekuwepo sehemu hiyo ya tukio
anahusishwa mazingira kwa sababu yeye yuko hapo kwa muda huo. Huo ushahidi wa
mazingira lazima uwepo ushahidi wa nyongeza kuweza kumtia mtu hatiani”,
Anasema ushahidi wa mazingira
huchukuliwa kama ni ushahidi wa nyongeza ambao unatumika kama mtu alikutwa eneo
la tukio lakini haimaanishi kuwa mtu huyo amefanya hilo tukio na mahakama
ikijiridhisha mtuhumiwa hutiwa hatiani na kuhukumiwa.
Akitoa maoni yake juu ya hukumu
iliyotolewa leo kwa Msanii Lulu amesema Mahakama imetenda haki kulingana na
ushahidi walioupata lakini Mawakili wa mtuhumiwa wana nafasi ya kukata
rufaa kama hawajaridhishwa na hukumu hiyo.
Anaamini kuwa Mawakili wa Lulu
wakikata rufaa wana uwezekano wa kushinda na Msanii huyo akaachiwa huru
kutokana na aina ya ushahidi uliotumika ambao kwa tafsiri ya kisheria ni
ushahidi wa nyongeza na sio wa moja kwa moja.
Chanzo:fikrapevu.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni