Umoja wa Ulaya (EU) umeitaka
serikali ya Tanzania kuimarisha taasisi za uwajibikaji na uwazi kwa kupanua
wigo wa Asasi za Kiraia kufanya kazi na jamii ili ifanikiwe katika mapambano
dhidi ya rushwa na kuwaletea wananchi maendeleo.
Tamko hilo la EU linakuja siku
chache baada ya serikali kuiondoa Tanzania kwenye Mpango wa Uendeshaji wa
Shughuli za Serikali kwa (OGP) na kuziagiza Halmashauri za miji
kutoshirikiana na Asasi za kiraia mpaka zipate idhini ya Wizara Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Wito huo umetolewa jijini Dar es
Salaam na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), Balozi Roeland van de Geer wakati akizindua Mradi wa Kutete
Haki ya Demokrasia, Uwazi na Uwajibikaji katika jamii,
Amesema changamoto kubwa
inayoikabili Tanzania ni rushwa ambayo imedhoofisha juhudi za serikali
kuwaletea wananchi maendeleo.
“Rushwa inaharibu rasilimali za
wananchi na jamii, zaidi kuvunja haki zao za msingi na uhuru. Gharama za
kiuchumi ni kubwa lakini gharama za rasilimali watu na jamii ni kubwa zaidi”,
amesema Balozi Geer na kuongeza kuwa,
“Rushwa ni adui wa maendeleo na
mafanikio. Ni chanzo kikubwa cha umaskini na kikwazo kuushinda. Dawa ni uwazi”.
Ili kuhakikisha rushwa inatokomezwa
katika jamii, ameshauri kuundwa kwa taasisi imara zinazojiendesha kwa uwazi na
kuwajibika kwa wananchi ambao ndio wadau muhimu wa shughuli za maendeleo.
“Kupambana na rushwa ni mapambano
yanayohitaji taasisi imara na wananchi makini katika ngazi zote. Lakini rushwa
haitokei Tanzania peke yake.
Rushwa ipo kila sehemu lakini tofauti ni
kwamba taasisi zao zina uwezo na utashi wa kupambana nayo”, amesema Balozi.
Ameongeza kuwa rushwa bado ni
changamoto katika Umoja wa Ulaya ambapo kila mwaka inaigharimu Euros bilioni
120 kwa mwaka.
Amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuzijengea uwezo
Asasi za Kiraia na wananchi hasa kwenye masula ya demokrasia, uwazi na
uwajibikaji wa viongozi katika jamii ili kujenga jamii inayoheshimu misingi ya
demokrasia.
Uwazi na Uwajibikaji katika Serikali
za Mitaa
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi
wa ‘Tuungane Kutete Haki’, Daniel El-Noshokaty amesema ili mapambano ya rushwa
yafanikiwe inahitajika nguvu ya pamoja katika ngazi ya serikali ya mitaa ambako
uwakilishi wa wananchi unapatikana.
“Rushwa ni kikwazo katika njia ya
maendeleo ambayo Tanzania inapita; mapambano yake yanatakiwa kuanzia kwenye
mizizi ya taifa. Kwa kufanya hivyo, nchi itakuwa na nafasi nzuri ya kutokomeza
rushwa katika ngazi ya juu. Kwa Pamoja Tanzania inaweza ikasimama na kupambana
na rushwa”, amesema El-Noshokaty.
Kulingana na Shirika la Transparency
International (2016) inaiweka Tanzania katika nafasi ya 116 katika ya nchi 176
zenye viwango kikubwa cha rushwa duniani. Na sababu kubwa ni kutokuwa na mifumo
imara ya kitaasisi inayofanya kazi kwa uhuru na uwazi.
Licha ya serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na rais John Magufuli kupiga hatua katika mapambano dhidi ya
rushwa, bado rushwa inajitokeza kwa sura tofauti na kuathiri kwa sehemu kubwa
upatikanaji wa huduma za kijamii, kudhoofisha mfumo wa utawala na kuzuia mazingira
mazuri ya kufanya biashara.
Ufunguzi huo wa Mradi wa ‘Tuungane
Kutetea Haki” ulihudhuliwa na wadau mbalimbalimbali kutoka Asasi za kiraia na
viongozi wa serikali, ambapo wote wamesisitiza uwepo wa uwazi katika shughuli
za maendeleo na viongozi kuwa tayari kuwajibika kwa wananchi ili kujenga jamii
inayoheshimu misingi ya demokrasia.
Mabadiliko ya Sera na Sheria kuchochea Uwazi
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa InterStar Consults, Lawrence Kilimwiko amesema Serikali za Mitaa zinaongozwa kwa msukumo wa kisiasa na utashi wa baadhi ya viongozi toka Serikali Kuu ambao wanatumia rasilimali za nchi kwa manufaa binafsi.
Ameitaka jamii kupaza sauti na kudai uwajibikaji na uwazi kwa kupigania mabadiliko ya kisheria na sera ambazo zimekuwa kikwazo kwa maendeleo ya nchi.
Mradi wa ‘Tuungane Kutetea Haki’ unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya, Konrad-Adenauer-Stiftung (KAS) kwa kushirikiana na taasisi za Actions for Democracy and Local Governance (ADLG) na Civic Education Teachers Association (CETA) ambao utagharimu bilioni 2.5 katika miaka miwili ya utkelezaji wake.
Mradi huo una lengo kupunguza mianya ya rushwa kwa kukuza ushirikiano baina ya Asasi za Kiraia (AZAKI) na Serikali za Mitaa kwa kupanua wigo wa siasa, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ngazi ya Halmashauri.
Unatekelezwa katika mikoa ya Geita, Simiyu, Ruvuma, Lindi, Mara, Kagera na Pwani ambaopo utafanya kazi sambamba na vyombo vya habari zikiwemo redio za kijamii katika maeneo husika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni