Jumapili, 26 Novemba 2017

MAZINGIRA:MOYO UNAOHITAJI ULINZI THABITI



Na Sitta Tumma, Mwanza
 
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinaoathirika na mabadiliko ya tabianchi, yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira.
 
Athari za mabadiriko haya yanasababisha hasara ya upotevu wa mali, maisha ya watu, mimea na viumbe vingine hai na visivyo hai, kama vile udongo.

Zaidi ya watu milioni 200 duniani kote wanaathirika na ukame, mafuriko, vimbunga, matetemeko, moto, milipuko ya mabomu na majanga mengine.

Aidha kuongezeka kwa majanga kumeongeza kasi ya watu kuathirika kiuchumi, pamoja na kuongeza idadi ya watu masikini duniani.

Kwa mtu asiyeelewa maana ya mabadiriko ya tabianchi, ni mtiririko wa mfumo wa mabadiliko ya  hali ya hewa.

Yanayochukua muda mrefu au mfupi.Husababisha hali mbaya za hewa, ama uchache wa hali inayohitajika au wingi wa hali isiyohitajika.
Husababsisha madhara kwa jamii na nchi kwa ujumla. Ndiyo!

Tatizo hili limekuwa miongoni mwa ajenda kuu za Umoja wa Mataifa (UN) na Jumuiya ya kimataifa  kwa mwaka 2014.

Dunia imejielekeza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Ili kuishinda vita hii lazima kila mtu abebe jukumu la kutunza mazingira yanayomzunguka.

Kuwepo kwa majanga haya duniani kunatokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu, zinazoathiri mfumo mzima wa hali ya hewa na mazingira.

Baadhi ya shughuli hizo ni ukataji miti ovyo, utiririshaji maji machafu, uvuvi wa kutumia sumu, ujenzi na uendeshaji viwanda vinavyochafua mazingira.

Umwagaji ovyo wa kemikali, madini na matumizi mabaya ya ardhi. Vichocheo vingine ni uchomaji moto misitu.

Mabadiriko ya tabianchi pia husababisha mafuriko, ukame na magonjwa dhidi ya wananchi na mimea!

Kwa zaidi ya miaka 50, hali ya hewa duniani imekuwa ikibadilika, kutokana na kuongezeka gesi chafu zinazozalishwa na mvuke wa maji, methane na  kaboni  dayoksaidi.
                    Uhifadhi Misitu

Kulingana na hayo, Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) imeweka mikakati ya kulinda mazingira na utunzaji wa misitu nchini.

Hifadhi ya Msitu wa Asili ya Milima ya Uluguru, iliyopo Mkoa wa Morogoro, ni moyo unaohitaji uangalizi madhubuti kwa faida ya jamii na maendeleo ya taifa.

Hifadhi hii inatakiwa kulindwa na kutunzwa na jamii yenyewe ya vijiji 62 vinavyozunguka msitu huo.

Tunapozungumzia Msitu wa Uluguru, tunagusa uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Msitu huu ni hazina ya maendeleo na hifadhi ya mazingira, si tu kwa Mkoa wa Morogoro bali ukanda wote wa Pwani na Dar es Salaam.

Juma James na Halima Musa, ni wakazi wa Mkoa wa Morogoro, wanasema uwapo wa msitu huo unawasaidia kupata hewa safi.

Mbali na hilo, wanasema unawasaidia pia kupata mvua kwa ajili ya kikimo, ingawa wanakiri hivi sasa hali ya hewa imebadirika kuliko awali.

"Lakini pia watalii wanapokuja kwenye Misitu ya Uluguru wananunua bidhaa zetu. Wengine wanalala Morogoro na kuongeza pato la wafanyabiashara.

"Mimi mwenyewe ingawa sijawahi kuingia kwenye misitu hii, lakini nafarijika sana kuona namna uoto wa asili unavyovutia," anasema Husna Ali (42) mkazi wa Morogoro.
              Panzi wa ajabu

Moja ya vivutio vya kitalii vilivyomo kwenye Hifadhi ya Uluguru, ni panzi mwenye rangi ya bendera ya Taifa la Tanzania. Ndiyo. Yupo!

Akizungumza na timu ya waandishi wa habari za mazingira, waliotembelea hivi karibuni hifadhi hii, Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Misitu ya Uluguru, Mohamed Borry, anasema panzi huyo hapatikani kokote duniani, isipokuwa kwenye msitu huo.

Timu hiyo ya wanahabari ilizuru eneo hilo, wakati wa mafunzo ya siku tano dhidi yao, yaliyoandaliwa na Muungano wa Vilab vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweeden kupitia Shirika lake la Maendeleo (SIDA).

"Yupo pia panzi mwingine yeye ana alama ya namba tisa mgongoni mwake. Huyu anaonekana Desemba 9 (siku nchi ilipopata uhuru wake-mwaka 1961).

"Uwapo wa msitu huu na viumbe hivi, inatulazimu sisi jamii tuendelee kutunza mazingira yanayotuunguka," anasema Borry na kuongeza:

"Mazingira ni uhai. Bila kutunza mazingira jamii ndiyo inayoathirika zaidi na uchafuzi huo. Kwa sababu kutakuwa na ukame, magonjwa, kukosa chakula na maji."

Mhifadhi Borry hapa anazitaja vivutio vingine vya kitalii, vilivyomo kwenye Hifadhi hiyo ya Uluguru kuwa ni vyura mwenye mguu mmoja, miwili na mitatu.
 
Kwa mujibu wa ofisa huyo, wapo pia vinyonga wenye pembe moja, mbili na tatu.
Kwamba uwapo wa viumbe hao unaonesha umuhimu wa jamii kutunza mazingira.

"Faida ya kutunza mazingira katika Msitu huu wa Uluguru, watu 151,000 wanaotoka vijiji 62 vinavyozunguka hifadhi hii watanufaika kiuchumi.

"Kwa sababu viumbe na uoto huu ni kivutio kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.

"Hivyo watalii wanapokuja wananunua bidhaa za wananchi na wenyeji kunufaika kuwapandisha milimani watalii," anasema Borry.
                  
                                                Utafiti


Utafiti wa Wakala wa Huduma ya Misitu nchini (TFS) unasema kwamba, heka 400,000 ya misitu inapotea kila mwaka kutokana na ukataji kuni, ujenzi, uchomaji misitu nakadhalika.

Vivyo hivyo, utafiti wa mwaka 2013 unasema jumla ya tani milioni moja za mkaa hutumika kila mwaka. Hii ni kutokana na ukosefu wa ajira.

Wataalamu wa masuala ya mazingira wanasema, asilimia 40 ya ardhi inayofaa kwa kilimo imeharibiwa vibaya, kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Kwamba uchafuzi huo unaofanywa na binadamu, unachangia mmomonyoko wa udongo jambo linaloathiri pia kilimo.

Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 pamoja na Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 zinazuia uharibifu wa misitu na uchomaji moto, ambapo imeainisha pia adhabu kwa waharibifu.

Pia, Sheria ya Mazingira No. 20 ya mwaka 2004, na ile ya Usimamizi wa Railimali ya Maji Na. 11 ya mwaka 2009, zinazuia pia uchafuzi wa maingira.

Kulingana na hayo, Sheria ya Maji inasema wazi kwamba, uchafuzi wa maji nikosa la jinai, na mtu au kiwanda hakitakiwi kutiririsha maji machafu bila kuwa na kibali cha Bodi ya Taifa ya Maji.

Wazir wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Januari Makamba, amekuwa akisisitiza kitu mtu nchini kutunza mazingira.

Waziri Makamba anataka kuona Sheri ya Mazingira inatekelezwa kwa vitendo, ikiwamo wachafuzi wa mazingira kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs) unaosimamiwa na UN duniani, unasisitiza kila nchi na raia wake kutunza mazingira.

Katika taarifa iliyotolewa mwaka jana na UN inasema kuwa, takribani watu milioni 700 wanaishi chini ya mstari wa umasikini duniani.

Mwandishi mkongwe wa habari za mazingira nchini, Deodatus Mfugale, yeye anaeleza kuchukizwa na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na jamii.

Mfugale anasema, uchafuzi wa mazingira una athari kubwa katika maisha ya binadamu na viumbe wengine.

Unasababisha magonjwa, vifo, ukame na kudhorota kwa afya za watu walioathiriwa na tatizo hilo.

"Binadamu ndiye anayeathirika zaidi na athari za uchafuzi wa mazingira. Kila mtu awajibike kulinda na kutunza mazingira.

"Sheria zipo, zisimamiwe kikamikifu kudhibiti uchafuzi wa mazingira Tanzania," anasema Mfugale.

Kufuatia hayo yatupasa kila mtu ayalinde na kutunza mazingira yanayomzunguka. Mazingira ni 'Moyo' unaohitaji uangalizi mzuri.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni