Mamlaka nchini Tanzania imezuia
uzinduzi wa ripoti kuhusu unyanyasaji wa wafanyikazi wanawake kutoka taifa hilo
wanaofanya kazi katika mataifa ya Uarabuni.
Shirika la Human Wrights Watch
limedai katika matokeo yake kwamba wafanyikazi wa nyumbani kutoka nchini
Tanzania walikuwa wakibakwa , kuteswa na kulipwa mishahara duni na waajiri wao
katika mataifa ya Uarabuni.
Ripoti yenye kurasa 100 inayodai
kuteswa kwa wafanyikazi wa nyumbani wa Tanzania nchini Oman na muungano wa
mataifa ya Emirata UAE ilitarajiwa kutolewa jana kwa waandishi wa habari mbele
ya waathiriwa lakini hilo halikufanyika.
Katika hatua isiokuwa ya kawaida
,afisa mmoja kutoka shirika linalofadhiliwa na serikali la Sayansi na
Teknolojia COSTEC William Kindekete alifutilia mbali mkutano huo katika mji
mkuu wa Dar es Salaam akisema kuwa wanaharakati wa shirika hilo la haki za
kibinaadamu hawakufuata sheria katika kufanya utafiti wao.
Hatahivyo matokeo ya utafiti huo wa
HRW unaonyesha kuwa takriban wanawake 50 walihojiwa wakati wa utafiti huo ambao
wanadai kwamba walilazimishwa kufanya kazi kwa kati ya saa 15 na 21 kwa siku
huku wakipokonywa pasipoti zao na waajiri wao punde tu walipowasili katika mataifa
hayo.
Ripoti hiyo ilibaini zaidi kwamba
zaidi ya nusu yao hawakulipwa huku wengine wakisema kuwa hawakulipwa kabisa.
Wawili kati ya watano walidai
kupigwa mbali na kunyanyaswa kijinsia.
Ripoti hiyo ya HRW pia inasema
kwamba balozi za Tanzania katika eneo la Ghuba hazikutoa usaidizi wowote kwa
waathiriwa wakati walipotaka usaidizi .
Juhudi za kupata majibu kutoka kwa
serikali ya Tanzania hazikufanikiwa kwa kuwa maafisa wengi hawakuwa tayari
kuzungumzia swala hilo.
Chanzo:bbcswahili.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni