Jumamosi, 11 Novemba 2017

WADUDU WATISHIA KILIMO CHA MIWA TPC MOSHI




Na Charles Ndagulla,Moshi

UZALISHAJI wa sukari katika kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo mkoani Kilimanjaro upo shakani kutokana na kuibuka kwa wadudu hatari wanaoshambulia  miwa .

Wadudu hao wanauojulikana kwa jina la kitaalamu kama White Grub,Eldana na  Yellow Sugar Cane Alphid,wanadaiwa kushambulia kwa kasi miwa pamoja na kusambaa kwenye mazao mengine ikiwamo zao la mpunga.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni  moshi na ofisa mtendaji wa kiwanda hicho anayeshughulikia masuala ya utawala,Jafari Ally katika taarifa yake kwa waziri wa Kilimo,Dk.Charles Tizeba.

Alisema white grub ni mdudu anayeshambulia mizizi ya miwa ama mazao mengine wakati Eldana ni mdudu anayepekecha muwa na kuwa wa rangi nyekundu huku white yellow sugar cane alphid ni jamii ya wadudu kama utitiri wanaopamba majani ya mmea na kuua mmea kwa kula majani na kugeuka kuwa ya njano.

Hata hivyo Jafari alilalamikia urasimu unaofanywa na Taasisi ya utafiti wa viuatilifu vya kitropiki Tanzania(TPRI) katika utoaji wa vibali vya kuagiza madawa ya kuulia wadudu hao na kumuomba waziri kuingilia kati suala hilo.

Alisema kuwa,upatikaji wa vibali kutoka TPRI unachukua zaidi ya miaka minne jambo ambalo alidai linakwamisha juhudi zao katika kukabiliana na wadudu hao na kwamba wasipodhibitiwa mapema wanaweza wakaathiri shughuli  za uzalishaji .

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni kukwama kwa vibali  kutoka mamlaka ya mapato Tanzania(TRA)vya kuingiza mtambo kwa ajili ya kuchimba visima 25 vitakavyosaidia shughuli za kilimo katika kiwanda hicho.

"“Mheshimiwa waziri,hili la usajili wa madawa nchini  kwa kweli ni changamoto kubwa sana,unachukua mpaka miaka minne na zaidi wadudu hawa ni hatari sana na wanaweza kusambaa mpaka kwenye mazao mengine”,alisema.

Akijibu changamoto hizo,Waziri Tizeba pamoja na kukiri kuwa urasimu huo haukubaliki, alisema kuchelewa kwa vibali vya kuingiza viuatilifu kutoka nje ya nchi kunatokana na baadhi ya wafanyabiashara kutokuwa waaminifu .

Alisema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakifanya udanganyifu kwa kuingiza bidhaa ambazo ni tofauti na zile zilizoombewe vibali hatua mabayo inaweza kuchangia kuchelewa kwa vibali hivyo.

Kuhusu ucheleweshwaji wa kibali kwa jli ya kuingiza mtambo wa kuchimba visima,waziri Tizeba alisema mtambo huo ni mhimu kwani uwepo wa visima vingi katika shamba hilo unaweza kupunguza mgogoro wa maji uliopo baina ya TPC  na  wananchi wa vijiji vya Mawala,Oria na Ngasini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni