Jumamosi, 11 Novemba 2017

MHISPANIA AWEKA REKODI YA KUPANDA MLIMA KILIMANJARO KWA KUTUMIA BAISKELI.



MPANDA milima mashuhuri duniani kwa kutumia Baiskeli ,Juanito Oiarzabal ameweka rekodi ya kuwa Mhispania wa kwanza kupanda Mlima Kilimanjaro huku akitumia saa 31 akiendesha baiskeli kwa siku tano hadi kufika kilele cha Uhuru.

Juanito na wenzake wawili , Eduardo Pascuaz na Ramon Abecia waliianza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kutumia Baiskeli ,wakianza safari yao kupitia lango la Kilema, aina hi ya utalii ikiwa ni bidhaa mpya katika Milima huo mrefu kuliko yote barani Afrika.

Aina hii mpya ya utalii ambayo kwa sasa imeanza kushika kasi katika Hifadhi za Taifa za Kilimanjaro,Arusha na Saadani inatokana na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuendelea kupanua wigo wa vivutio vya utalii katika Hifadhi zake 16.

Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete anaeleza hatua ya Juanito na wenzake kufika katika kilele cha Uhuru inaashiria kuanza kufunguka kwa aina hii mpya ya utalii katika Hifadhi za Taifa .

Shelutete anaeleza namna ambavyo Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limekuwa mstari wa mbele katika kubuni aina mpya ya bidhaa za utalii ili kushindana na nchi nyingine duniani katika uuzaji wa safari kwa watalii.

Kwa upande wake Juanito Oiarzabal ambaye amepata ulemavu wa kukatika vidole kutokana na barafu katika milima mbalimbali aliyopanda amesema changamoto aliyokutana nayo wakati wa kupanda mlima ni kuzoea hali ya hewa ya mlima ambayo imekuwa ikibadilika kila mara.

Mkurugenzi wa kampuni ya Safari Bike Africa iliyoratibu changamoto ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kutumia Baiskeli kwa wageni hao,Mario Martos amesema kampuni yake imekusudia kuleta mabadiliko katika sekta ya utalii kwa kufanikisha safari za watalii wa kutumia baiskeli.

Shirika la Hifdhi za Taifa (TANAPA) limejipanga kuhakikisha usalama wa hali ya juu kwa wageni watakaofanya aina hii mpya ya utalii katika Hifadhi zake kwa kuwa na taahadhari sambamba na waongoza wageni waliobobea katika kazi ya Utalii.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni