Na Charles
Ndagulla,Moshi
OFISI ya
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali(CAG),imeibua madudu
yanayosababisha mabonde ya maji kukosa mabilioni ya fedha yatokanayo na mapato
kutoka kwa watumiaji wa maji nchini.
Miongoni mwa
madudu hayo ni kutokuwepo na udhibiti kwa watumiaji wa maji hatua ambayo
imesababisha baadhi ya watumiaji wa maji kuzidisha viwango vya uchukuaji wa
maji tofauti na ilivyoainishwa kwenye
vibali vyao.
Hayo yamo
kwenye mada iliyowasilishwa na mkaguzi ufanisi kutoka ofisi ya CAG,Rebecca
Mahenge kwenye warsha ya siku moja iliyolenga kujadili ripoti ya CAG toleo la
Mwananchi kwa mwaka wa fedha uliomalizika machi 31 mwaka huu 2017.
Warsha hiyo
ilifanyika mjini Moshi hivi karibuni na kushirikisha asasi zisizo za kiserikali kutoka
mikoa ya Manyara,Arusha,Kilimanjaro na Tanga pamoja na wanahabari wa mkoa wa
Kilimanjaro.
Madhumuni ya
ukaguzi wa ufanisi kwa mujibu wa mkaguzi huyo ni kutoa tathimini ya
kiwango ambacho thamani ya fedha yaani
uwekevu,tija na ufanisi huzingatiwa na taasisi za serikali zinapotumia
raslimali katika kutekeleza majukumu yake.
Alisema
kuwa,mamlaka ya maji safi na uondoshaji maji taja Jijini
Mwanza(MWAUWASA)ilizodisha maji kwa aslimia 70 baada ya kutumia lita za ujazo
90,000 kwa siku badala ya lita za ujazo 50,000 kwa siku.
Amesema
kitendo hicho kiliikosesha mapato Bodi ya Bonde la maji ziwa Victoria ya
shilingi Milioni 41 kama malipo ya ziada kutoka kwa watumiaji waliozidisha
viwango vya maji.
Ripoti hiyo
ambayo imo kwenye kitabu kidogo imebainisha kuwa,Bonde la mto Wami/Ruvu
limepoteza mapato yanayokadiliwa kufikia shilingi Milioni 814 kutokana na
visima vilivyochimbwa bila kufuata
utaratibu rasmi katika wilaya ya Ilala mkoa wa Dar es salaam na hivyo kutotambuliwa na Bodi ya maji ya
Bonde la mto Ruvu.
Mkaguzi huyo
wa ufanisi amesema kuwa kwa mujibu wa
ukaguzi uliofanywa na ofisi ya CAG,umebaini
kuwa kati ya visima 2,888 vilivyopo wilaya ya Ilala,ni visima 262 pekee ndio
vipo kwenye orodha ya usajili.
Amesema
mabonde manne yalikosa shilingi Bilioni mbili sawa na aslimia 40 ya kiasi cha
shilingi bilioni tano walizotakiwa kukusanya katika kipindi cha miaka mitano
cha 2011-2012 hadi 2015/2016.
Ukaguzi huo
ambao ulihusu usimamizi na udhibiti wa uchukuaji wa maji kutoka vyanzo vya maji,
ulihusisha mabonde manne ambayo ni bonde la mto Pangani,Bonde la ziwa
Victoria,bonde la Mto Wami/Ruvu na bonde la kati.
Amesema
kuwa,udhaifu katika ukusanyaji wa mapato umesababisha wenye vibali vya kuchukua
maji katika mabonde hayo kutokufuata sheria na makubaliano waliyoingia kati yao
na mamlaka za mabonde.
“Kumekuwepo
na udhaifu katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na ada wanazolipa wenye
vibali vya kuchukua maji katika mabonde,hali hii imechangia bodi za mabonde
kukosa fedha za kutekeleza majukumu yake.”,amesema.
Aidha
imebainika katika ukaguzi huo kuwa,sera ya maji ya mwaka 2009 na sheria namba
11 ya mwaka 2009 inayohusu usimamizi wa Raslimali za maji ambayo inaelekeza
uzingatiaji wa uwepo wa maji na akiba ya maji kwa ajili ya
mazingira,haizingatiwi katika utoaji wa vibali vya maji.
Ripoti hiyo ikapendekeza wizara ya maji na
umwagiliaji kuyaagiza mabonde ya maji kuzingatia matumizi endelevu katika vyanzo vya maji ikiwamo kuhakikisha kunakuwepo mpango
wa pamoja wa usimamizi wa raslimali za maji unaotumika katika mabonde yote.
Pia
ikapendekezwa kuimarishwa kwa udhibiti
katika ukusanyaji wa mapato pamoja na wachukuaji wa maji wasio na vibali na
wale wanaozidisha viwango vilivyoainishwa katika vibali vyao.
Lengo la
ukaguzi huo wa CAG ni kubaini ukubwa wa
tatizo la uhaba wa maji unaotokana na uharibifu wa vyanzo vya maji hivyo kusababisha
migogoro kwa watumiaji wa maji.
Katika
ukaguzi huo pia mapungufu kadhaa yalijitokeza ikiwamo kutokuwepo na mipango
jumuifu wa usimamizi wa raslimali za maji katika mabonde hayo kwa
kuwashirikisha wadau wote.
Hali hiyo
imetajwa kusababisha utoaji wa vibali pasipo kuzingatia kiasi cha maji
kinachopatikana katika mabonde husika kutokana na kutokuwepo kwa udhibiti kwa
watumiaji wa maji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni