Alhamisi, 29 Machi 2018

LIPENI ANKRA ZA MAJI KWA WAKATI,DC KIPPI WARIOBA AWAASA WATEJA MUWSA


 
   Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na uondoshaji wa majitaka Moshi Mjini(MUWSA),Joyce Msiru akitoa taarifa ya utendaji kazi wa mamlaka hiyo katika uzinduzi wa wiki ya maji hvi karibini mjini moshi.                
  

MKUU wa Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, Kippi Warioba amewataka Wananchi kulipa ankra za maji kwa wakati, ili huduma hiyo izidi kuwa endelevu, hali ambayo itawezesha pia kuwahudumia watu wengine kwa pamoja.

Warioba  alitoa kauli hiyo hivi karibuni  kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya  Maji ambayo kimkoa yalifanyika mjini moshi  katika viwanja vya Mamlaka ya Majisafi na Uondoshai wa maji taka moshi mjini (MUWSA).

Alisema kuwa ili MUWSA iweze kuendelea kutoa huduma bora ya maji kwa wananchi wa moshi ni vyema Wananchi wakawa na utayari wa kulipia ankra hizo kwa wakati.

“Niwaase Wananchi wenzangu kulipia ankra zenu za maji kwa wakati ili kuifanya huduma ya maji itolewayo na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira MUWSA, kuwa endelevu,”alisema Warioba.

Aidha mkuu huyo wa wilaya aliwataka Wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji, ili maji hayo yaendelea kuwapo wakati wote kwenye vyanzo vya maji vilivyopo bila kupungua.

“Nachukua nafasi hii kuwaasa wale wote wanaofanya shughuli za uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji kuacha mara moja kufanya uharibifu huo,”alisema.
MKuu wa wilaya ya Moshi,Kippi Warioba(wa pili kutoka kulia)akikata utepe kuzindua huduma mpya ya kulipia ankara za maji ijulikanayo kama NMB Mobile katika uzinduzi wa wiki ya maji iliyofanyika hivi karibuni mjini Moshi.

Aliongeza kuwa “Naomba nitoe agizo kali kwa yeyote atakayepatikana anafanya shughuli za uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji, hatua kali zichukuliwe dhidi yake, na wale wote watakaokwenda kinyume na katazo la sheria hizi, waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria,”alisema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya sheria ya rasilimali za maji namba 11 ya mwaka 2009 kifungu cha 34, sambamba na sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 57, vyote kwa pamoja vinapinga  kufanyika kwa  shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kwenye vyanzo vya maji, mabwawa, mito, maziwa, chemichemi pamoja na kwenye visima.

Nae Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na ondoshaji wa majitaka(MUWSA) Joyce Msiru, alisema kuwa Mamlaka hiyo inaendelea kuhamasisha na kuwaelimisha Wananchi kushiriki kikamilifu  katika matumizi ya majisafi na usafi wa mazingira, ikiambatana na kulipia ankra za matumizi ya majisafi na maji taka kwa wakati.

“Mamlaka inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya maji kuelimisha jamii juu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji na uendeshaji endelevu wa miradi ya maji, ili kuhakikisha kizazi kijacho kinapata rasilimali ya majisafi kwa uhakika na ubora unaotakiwa,”alisema Msiru. 


Jumanne, 27 Machi 2018

KICHAA CHA MBWA CHABISHA HODI K'NJARO,CHAUA WATATU,MAKUMI WAJERUHIWA


 NA CHARLES NDAGULLA,MOSHI

MKOA  wa Kilimanjaro,umekumbwa na tishio la ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambako mpaka sasa watu watatu wamekufa kutokana na kung’atwa na mbwa wanaoaminika kuwa na ugonjwa huo wakiwamo watoto wawili na mama mmoja .

Mbali na watu hao kufariki dunia katika halmashauri ya wilaya ya Moshi,watu 64 wameripotiwa kujeruhiwa na mbwa hao wenye ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika Vijiji vya TPC,Mawala,Oria,Mabogini na Ngasini.

Waliofariki dunia kwa kung’atwa na mbwa hao wametajwa kuwa ni Lulu Zephania(4),Grace Benny (5) mwanafunzi wa shule ya awali katika shule ya msingi Mawala na Naomi Mmanga(34) wote wakazi wa Kijiji cha Mawala.

Kwa mujibu wa Dk.Walter Marandu,daktari wa mifugo katika Halmashauri ya wilaya ya Moshi ,watu hao walishambuliwa na mbwa mmoja kati ya februari mosi na februari 5 mwaka huu na kukimbizwa katika Zanahati ya mawala kwa matibabu.

Akizungumza na Ndagullablog,Marandu  amesema kuwa baada ya hali zao kuendelea kuwa mbaya walihamishiwa katika  Hospitali ya TPC inayomilikiwa na Kiwanda cha sukari cha TPC kabla ya kupelekwa katika Hospital ya rufaa ya KCMC ambako mauti yaliwakuta.

Dk. Marandu amebainisha kuwa,tayari oparesheni kubwa ya kuwaangamiza mbwa hao inaendelea katika maeneo mbali mbali yaliyoripotiwa kukumbwa na ugonjwa huo.

Amesema mpaka sasa mbwa zaidi ya 100 wanaodaiwa kuwa na kichaa cha mbwa wameuawa katika oparesheni hiyo katika vijiji vya Mawala, Mikocheni, Msarikie na Mtakuja.

Kwa mujibu wa Dk.Marandu,watu 64 waliong’atwa na mbwa hao ni katika kipindi cha kuanzia januari hadi mwezi machi mwaka huu na kwamba tatizo hilo la kuwepo na mbwa wenye kichaa cha mbwa ni kubwa huku  wengi wa mbwa wenye ugonjwa huo  ni wale wanaozagaa mitaani .

Amesema tayari Halmashauri imeanza kutoa elimu kwa wananchi juu ya kukabiliana na mbwa hao kwa kutoa gari la matangazo ambalo limekuwa likizunguka katika maeneo mbali mbali ya vijiji kutoa tahadhari hiyo.

“Timu yetu ya wataalamu ipo vijiji pamoja na gari la matangazo,tunatoa matangazo makanisani na misikitini juu ya kuwepo na mbwa wenye kichaa cha mbwa na namna ya wanachi kuchukua hatua”,amesema.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji cha Mawala,David Laizer,amezungumza na Ndagullablog na kueleza kuwa tayari wamewaua mbwa 19 katika kijiji hicho tangu kuripotiwa kwa mlipuko wa ugonjwa huo .


Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Moshi,Michael Kilawila amezungumza na Ndagullablog kuhusiana na kuibuka kwa ugonjwa huo na kueleza kuwa tayari zoezi la kuwapa chanjo mbwa hao limeanza.

Amesema lengo la chanjo hiyo ni kuhakikisha mbwa hao hawaendelei kuleta madhara kwa binadamu huku chanjo hiyo ikienda sanjari na kutolewa kwa elimu kwa wannchi juu ya kujilinda na mbwa hao.

“Tunawaomba wenye mbwa wao kuhakikisha kuwa mbwa wao wanapatiwa chanjo zinazositahili kuanzia chanjo ya kichaa cha mbwa, pamoja na magonjwa mengine ili kuepusha watu wasiendelee kupata madhara zaidi.

Moshi mjini nako hali tete.

Wakati hali ikiwa hivyo katika Halmshauri ya wilaya ya Moshi Vijijini,tatizo hilo pia limeripotiwa katika maeneo kadhaa ya mji wa Moshi ambako watu 13 wamelazwa katika Hospital teule ya St.Joseph ,Hospital ya Rufaa ya KCMC na kituo cha Afya cha Pasua baada ya kudaiwa kung’atwa na mbwa hao.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,Michael Mwandezi amedhibitisha kuwepo na tishio la mbwa kung’ata watu katika manispaa hiyo alipozungumza na wanahabari ofisini kwake wiki iliyopita.

Amesema mbali na watu hao kulazwa kutokana na kushambuliwa na mbwa hao,hadi sasa zaidi ya watu 90 wameripotiwa kung’atwa na mbwa ndani ya manispaa ya Moshi katika kipindi cha kuanzia januari hadi machi mwaka huu.

“Ni kweli  manispaa yetu imekubwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa  na hivi ninavyozungumza tunao  wagonjwa ambao wameng’atwa na mbwa hao na baadhi yao  wamefariki dunia japo kwa sasa sina tawimu sahihi ya idadi ya waliokufa   na pia  wako wanaoendelea kupatiwa matibabu katika hosptali zetu”amesema

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo,Hospital teule ya Mtakatifu Joseph imepokea wagonjwa wanne wakati Hospital ya rufaa ya KCMC inayoendeshwa na Shirika la Msamalia Mwema(GSF)imepokea wagonjwa saba na kituo cha Afya cha pasua kinao wagonjwa wawili.

Amesema jitihada mbali mbali zimechukuliwa kukabilina na tishio la mbwa hao ikiwamo kuendesha oparesheni ya kuwaua mbwa wote wanaoonekana wakilanda landa mitaani.

  ”Tumeshaanza kutoa  matangazo kwa wananchi na tumewataka kutoa taarifa endapo watawaona mbwa  wakilanda landa mitaani na pia tumetoa maelekezo kwa wamiliki wa mbwa kuchukua tahadhari ikiwamo kuwapa chanjo mbwa  ”amesema

Mganga  Mkuu wa Manispaa hiyo,  Soka Mwakapalala amesema baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika  Hospitali za KCMC na Mtakatifu Joseph  hali zao ni mbaya  kutokana na baadhi yao kuripotiwa kupatwa na tatioz la kubweka kama mbwa.

Dk. Mwakapalala amesema kuwa mpaka sasa watu 91 wameripotiwak ung’atwa nam bwa kati ya januari na machi mwaka huu huku akieleza kuwa  virusi vya kichaa cha mbwa hushambulia sana mishipa ya fahamu na dalili kubwa ni mtu Kubweka kama mbwa  na  mwisho mtu  huyo hupoteza fahamu na kufariki.

“Asilimia 99 ya wagonjwa walioang’atwa na mbwa hufariki dunia hivyo kunahitajika tahadhari kubwa sana na tunawaomba wananchi pindi wanaposhambuliwa na mbwa ni mhimu kwenda haraka kupata matibabu ndani ya saa 24”amesema.

Mpaka sasa Manispaa ya Moshi imeendesha oparesheni na kuwaua mbwa 700 kwa kuwapiga risasi huku mbwa 709 wkaipatiwa chanjo.

Kwa mujibu wa Dk. Mwakapalala, katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2016 watu zaidi ya 1,000 waling’atwa na mbwa  ambapo mwaka 2016 walikuwa 434, mwaka 2017 watu 564 na katika kipindi cha kuanzia January hadi Machi mwaka huu ni watu 91.

Jumatatu, 26 Machi 2018

WAFUNGWA UGANDA WAHITIMU SHAHADA YA SHERIA WAKIWA GEREZANI


   
 Pascal Kakuru,Suzzan Kigula na Moses Ekwam,wakipokea shahada za digree ya sheria huku wakiwa wamevalia sare nyeusi za kuhitimu .

Wafungwa watatu (pichani juu)waliosomea gerezani wamehitimu  shahada za digrii katika sheria, ikiwa ni mara ya kwanza kwa wafungwa nchini Uganda kufuzu shahada ya uanasheria.

Mpango huo unaofanikishwa na Mradi wa wafungwa barani Afrika kwa ushirikiano na chuo kikuu cha London  unanuia kuwapa wafungwa fursa ya kushiriki kikamilifu katika taratibu za kutafuta haki.

Kuhitimu kwa watatu hao kutoka Gereza Kuu la Luzira kumetazamwa kama ishara ya mwamko mpya katika mfumo wa marekebisho magerezani Uganda.

Pascal Kakuru, Suzzan Kigula na Moses Ekwam walipokea shahada za digree huku wakiwa wamevalia sare nyeusi za kuhitimu.

Moses Ekwam mmoja wa waliohitimu alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano lakini alihudumu miaka minne baada ya kupatwa bila hatia.

Kwa miaka hiyo minne alipokuwa gerezani alianza kusomea somo la sheria na hivi sasa Ekwam ni mwendesha mashtaka wa jeshi la Uganda.

"Mimi nilikuja hapa nikaona mimi kukaa hapa kuangalia mpira niliona shule iko ndani kwa hivyo nikaamua kujiunga na shule A level nikapita vizuri 2010 hadi sasa hivi  niko wakili," aliambia BBC.
 


Mwenzake Pascal alikuwa akitumikia kifungo kwa makosa ya uhaini na hivi sasa anaelekea kumaliza kifungo chake baada ya kupata msamaha na sasa anasema analenga kutumia utaalamu wake katika sheria.

"Ninao mpango wa kuzungumzia wale watu wanaoteseka wale watoto, kinamama, wafungwa wakimbizi ni watu hodari sana huwezi kuwaongelea wawe kama wanaharakati watu kama hao.


Kutakuwa na ulimwengu vitu kadhaa vya watu kama hao kwa hivyo nina mpango wa kuwazungumzia mahali popote wapo si kwa nchi ya Uganda peke yake bali ulimwengu mzima popote nitakapopata nafasi ya kuwasaidia watu kama hao. "

Katika ripoti ya hivi karibuni Jarida la Afrika la masuala ya uhalifu na haki, idara ya magereza nchini Uganda imewekwa katika nafasi ya kwanza barani Afrika kwenye suala la mageuzi.

Hata hivyo bado kuna changamoto katika kuzingatia haki za wafungwa.
Owinyi Dollo ni naibu wa jaji mkuu nchini Uganda:

"Unaanza kujiuliza kweli kama hukumu ya kifo inapaswa kuwa katika sheria zetu, unahoji kwa sababu mtu ambaye alivunja sheria jana anaweza kubadirika na kuwa mtu mwenye ushawishi mwema leo.

Kwa kuhitimu wafungwa hao watatu wanafuata nyayo za rais wa zamani wa Afrika kusini Nelson Mandela aliyejiimarisha kitaaluma wakati akiwa gerezani jambo linalowapa matumaini wafungwa wengi na pia kuongeza mskumo wa mageuzi zaidi magerezani.

Nchini Kenya, wafungwa wamewahi kusomea sheria na kuhitimu na baadhi hata kuwasaidia wenzao kupata uhuru.

Peter Ouko, mmoja wao, kwa sasa ni balozi wa shirika la Africa Prisons Project.

Alikuwa amehukumiwa kifo na kuwa mfungwa kwa miaka kumi na minane kabla ya kupunguziwa kifungo na kuwa kifungo cha maisha na kisha kuachiliwa huru kwa msamaha wa rais,alipatikana na kosa la kumuua mkewe.       
 Wafungwa katika gereza Kuu la Luzira nchini Uganda akishuhudia wenzao wakitunukiwa vyeti baada ya kuhitimu shahada ya Sheria wakiwa grezani hivi karibuni.

Alhamisi, 22 Machi 2018

UFA MKUBWA WAIBUKA BONDE LA UFA NA KUTISHIA UWEZEKANO WA TANZANIA NA KENYA KUTENGANA


     

Kuibuka kwa ufa mkubwa katika eneo la Suswa katika Bonde la Ufa kusini magharibi mwa nchi ya  Kenya kumezua wasiwasi kuhusu uthabiti wa eneo la Afrika Mashariki kijiolojia.

Wataalamu wanasema kutokea kwa ufa huo katika jimbo la Nakuru ni shughuli ya kijiolojia inayochukua muda mrefu ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda.

Hilo limezua hatari ya kuanza kutokea tena kwa mitetemeko ya ardhi na milipuko ya volkano.

Wanajiolojia wanasema baada ya mamilioni ya miaka, bara la Afrika litapasuka na kuwa vipande viwili.

Sehemu ya mpasuko itakuwa kwenye Bonde la Ufa jambo ambalo linazua uwezekano wa Kenya na Tanzania, pamoja na mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, kujitenga na bara la Afrika.

Mwanajiolojia David Adede ameambia BBC kwamba ufa huo ni sehemu ya kutengana kwa vipande viwili vikubwa vya bara Afrika ambako kutasababisha bara Afrika kutengana na kuwa mabara mawili.

Amesema shughuli hiyo imekuwa ikiendelea kwa muda lakini dalili zake zilikuwa zinafichwa na majivu ya volkano ambayo polepole yamekuwa yakiziba ufa kila unapotokea.


"Maji ya mvua yamesomba majivu hayo pamoja na mchanga na kuufanya ufa huo kuonekana zaidi," amesema.

Anasema vipande hivyo vimekuwa vikitengana "katika kasi ya sentimita mbili kila mwaka."

Kipande kilicho na sehemu kubwa ya bara hufahamika kama Kipande cha Nubia na kipande cha pili hufahamika kama Kipande cha Somalia.

Dkt James Hammond kutoka  Idara ya Sayansi na Uhandisi wa Dunia kutoka chuo cha Imperial College London alinukuliwa na jarida la mtandaoni la Mail & Guardian akisema: 

"Katika miaka milioni kadha ijayo, shughuli hii itakamilika na kuigawa Afrika mara mbili, na kuunda bahari mpya hapo katikati na bara jingine. Ukitumia jiografia ya sasa, bara hilo jipya litashirikisha Somalia, nusu ya Ethiopia, Kenya na Tanzania." 

Baadhi ya wanajiolojia wanakadiria kwamba huenda mpasuko huu ukayabeba pia mataifa ya Uganda, Rwanda, Burundi na maeneo ya Malawi na Msumbiji.

Mwanajilojia Dereje Ayalew kutoka Chuo Kikuu cha Addis Ababa Ethiopia ameliambia jarida hilo kwamba dalili za kutokea kwa bahari zimeanza kuonekana katika maeneo ya jangwani ya Ethiopia, eneo la Afar ambalo pia linahusisha baadhi ya maeneo ya Eritrea na Djibouti.

Mwaka 2005, alisema tayari nyufa nyingi zimeanza kutokea na ardhi imebonyea kwa hadi mira 100.

Ufa huo ulianza kuonekana wiki moja iliyopita baada ya mvua kubwa kunyesha na barabara ya Mai Mahiu kwenda Narok ikakatika eneo lenye ufa huo.

Awali, wengi waliamini ufa huo uliotokea Jumanne wiki iliyopita eneo la Karima ambalo linapatikana kilomita sita kutoka mji wa Mai Mahiu ulitokana na mvua kubwa.


Ufa huo uliokuwa umeikata barabara hiyo ulikuwa umeenea umbali wa mita 700.

Maafisa wa Mamlaka ya Taifa ya Barabara Kenya (KeNHA) wakishirikiana na mkandarasi kutoka China anayejenga reli ya kisasa, walifika eneo hilo na kuziba ufa.

Baada ya uchunguzi, ilibainika kwamba ulitokana na shughuli ya kijiolojia chini ya ardhi ambayo ilihusisha mvutano wa vipande vikubwa vya ardhi.

Siku chache baadaye Jumapili, ufa huo uliendelea kupanuka na kuathiri barabara hiyo tena jambo lililosababisha magari yenye kubeba mizigo mizito kutoweza kupita na tayari umeanza kuathiri nyumba za wakazi.

"Mkandarasi na kundi la wahandisi wamewekwa hapo kwa sasa na watasalia kuendelea kufuatilia yanayojiri kutokana na shughuli za kivolkano ambazo zilisababisha ufa huo," alisema naibu mkurugenzi wa mawasiliano wa KeNHA Charles Njogu baada ya ukarabati huo mara ya kwanza.

 Adede amesema hatua ya kuziba ufa huo kwa sasa itasaidia kwa muda mfupi tu na ufa huo umepitia katika baadhi ya nyumba na mashamba ya watu.
 Eliud Njoroge,mmoja wa raia wa kenya walioathiriwa na ufa huo

Mmoja wa walioathirika ni  kikongwe wa maka 77,Eliud Njoroge,ambaye ameishi katika eneo hilo  kwa zaidi ya miaka 20,amesema amelazimika kuiboa nyuba yake na sasa anaishi  anishi kama 'mkimbizi' kwa jirani yake.
   

Mwandishi wa BBC aliyetembelea eneo hilo Gladys Njoroge anasema katika baadhi ya maeneo, ufa huo una upana wa mita 20 na kina cha hadi futi 50.

Wataalamu wametahadharisha kwamba nyufa zaidi zinaweza kuendelea kuonekana katika baadhi ya maeneo ya Bonde la Ufa.

Mwandishi wa BBC Ferdinand Omondi anasema viongozi wa eneo lililoathirika wamewahimiza wakazi wanaoishi karibu na maeneo yaliyotokea ufa huo kuhama, lakini baadhi yao akiwamo  Njoroge hawawezi kuhamia mbali.


Chanzo: BBC Swahili