Na Charles Ndagulla,Moshi.
NAIBU Waziri wa Kilimo,Dk.Mary Mwanjelwa,ameitaka bodi ya Kahawa
Tanzania(TCB) kutoa taarifa ni kwa nini kahawa ya Tanzania imekosa bie nzuri
kweneo soko la dunia huku kahawa hiyo ikitajwa kuwa na ubora wa hali ya juu.
Dk.Mwajelwa alikuwa mkoani
Kilimanjaro hivi karibuni kwa ziara ya sku moja ambako alipata fursa ya
kutembelea makao makuu ya Bdi hiyo yaliyopo mjini moshi na kupata taarifa za utekelezaji wa shughuli za bodi hiyo.
Amesema bei ya kahawa ikiwa nzuri maisha ya wakulima wa
zao hilo yatakuwa mazuri lakini bei hiyo ikiyumba kwenye soko la dunia hata
hapa nchini bei ya zao hilo itakuwa mbaya.
“Lakini lazima pia tuangalie kwa makini
aina ya uvundikaji wa kahawa na uandaaji usiozingatia ubora unaweza kuwa
chanzo cha kahawa yetu kukosa bei nzuri,kwa hiyo ninyi kama bodi ni mhimu
mkatuletea taarifa ni kwa nini bei ya kahawa yetu imeshuka kwenye soko la
dunia”,amesema.
Dk.Mwanjelwa aliitaka bodi hiyo kuwa
na mikakati ya dhati ya kulipeleka mbele zao la kahawa na kuwa na heshima na
thamani kama ilivyo kwa zao la korosho
na kuhoji kama kahawa ya Tanzania ina ubora wa juu ni kwa nini haipati bei
nzuri kwenye soko la dunia.
Aliitaka bodi hiyo kutochelewesha
malipo ya wakulima pindi kahawa yao inapouzwa mnadani na kuonya kuwa wakulima
wasipolipwa malipo yao kwa wakati wanaweza wakajenga chuki dhidi ya serikali
yao.
“Awamu hii ya tano ni lazima kila
mtumishi ajiongeze,wakati wa kufanyakazi kwa mazoea umepitwa na wakati,ninyi
bodi ya kahawa mmepewa mamlaka ya kusimamia zao la kahawa sasa naomba msisubiri
kuamshwa”,alionya.
Katika taarifa yake kwa naibu waziri
huyo,kaimu mkurugenzi wa bodi ya kahawa,Primus Kimaryo alisema kuwa,katika
msimu wa 2016/2017 wakulima waliouza kahawa yao wakati bei ikiwa nzuri sokoni
walipata wastani wa shilingi 5,000.
Alisema wastani wa bei kwa msimu ni
shilingi 4,000 kwa kahawa ya Arabika huku wakulima wanaozalisha kahawa aina ya
Robusta walilipwa wastani wa shilingi 1,200 hadi 1,400 kwak ilo ya maganda.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo(kulia)akimweleza jambo Naibu Waziri wa Kilimo,Dk.Mary Mwanjelwa(kushoto)ambaye alifanya ziara ya siku moja katika makao makuu ya Bodi hiyo mjini Moshi hivi karibuni.
“Msimu huu 2017/2018 bei ya kahawa
imeshuka kutokana na kushuka kwa bei ya kahawa katika soko la dunia,bei ya
mkulima imekuwa ni ya wastani kutokana na ushindani unaotokana na kiwango
kidogo cha uzalishaji “,alisema.
Hata hivyo Kimaryo alisema kuwa
kuyumba kwa uzalishaji na ubora kunaathiri bei ya mkulima huku soko la mnada
likimikiwa na makampuni machache ya nje pamoja na vyama vya ushirika na vikundi
vya wkulima kutotumia fursa ya uongezaji thamani wa zao.
Kuhusu changamoto za masoko,kaimu
mkurugenzi huyo amesema soko la DE ambalo lilianzishwa kwa ajili ya kumsaidia
mkulima kwa kuuza kahawa za ubora wa juu,linatumiwa kwa kiasi kikubwa na
makampuni yanayonunua kahawa vijijini.
Amesema wakulima wazalishaji hawanufaiki
ipasavyo na soko hilo na kwmaba dirisha hilo siyo mbadala wa mnada huku vyama
vya msingi vya ushirika vikishindwa kuwasaidia ipasavyo wakulima kutokana na
kukumbwa na matatizo ya uendeshaji.
“Mheshimiwa naibu waziri,pia zipo
changamoto za uchanganyaji wa kahawa zenye ubora tofauti,kutegemea soko la nje
kwa aslimia tisini huku matumizi ya CPU yakiwa chini pamoja na upatikanaji wa
magunia ya kahawa kutokuwa na uhakika”,amesema.
HALI
YA UZALISHAJI WA KAHAWA NCHINI
Kuhusu hali ya uzalishaji wa kahawa
nchini,kaimu mkurugenzi huyo alimweleza naibu waziri kuwa mwaka 2011 wadau wa
kahawa waliandaa na kupitisha
mkakati wa miaka kumi wa maendeleo ya kahawa .
Alisema lengo kuu la mkakati huo
ilikuwa ni kuendeleza zao hilo kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kahawa na
kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 80,000 mwaka huu na tani 100,000 ifikapo
mwaka 2021 lakini alikiri kuwa lengo hilo halijafikiwa.
Alisema kutokana na kukwama kwa
lengo hilo,mkakati huo umefanyiwa marejeo ya muda wa kati na mshauri mwelekezi
aliyefanya kazi hiyo ameshakamilisha kazi yake .
Lengo jingine la mkakati huo ilikuwa ni kuongeza
uzalishaji,tija na ubora wa kahawa na kuboresha mapato katika mnyororo wote wa
thamani hususani wakulima wa kahawa na kuwezesha kahawa ya Tanzania
kupata bei nzuri kwenye soko la dunia.
Alitaja changamoto nyingine
zilizokwaza mkakati huo kuwa ni pamoja na tija ndogo ya uzalishaji
inayochangiwa na matumizi kidogo ya pembejeo hususani mbolea .
Sababu nyingine zilizokwaza mkakati
huo zinatajwa kuwa ni kasi ndogo ya kupokea matokoeo ya utafiti,mabadiliko ya
tabianchi yanayaodaiwa kusababisha mvua zisizo na mpangilio pamoja na uwekezaji
mdogo ikilinganishwa na malengo ya mkakati huo.
Uchunguzi wa jamhuri umebaini
kuwa,katika misimu saba iliyopita uzalishaji wa zao la kahawa nchini umekuwa
ukipanda na kushuka huku baadhi ya wakulima wakidaiwa kulipa kisogo zao hilo na
kugeukia mazao mseto kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na bei
ndogo.
Katika msimu wa 2010/2011 uzalishaji
wa kahawa ulikuwa tani 56,790.0 lakini msimu uliofuata wa 2011/2012 uzalishaji
ulishuka kwa kasi ya kutisha na kufikia tani 33,086.7 na ulipanda tena msimu wa
2012/2013 na kufikia tani 71,319.1.
Msimu wa 2013/2014 tani 48,761.9
zilizalishwa na tani hizo zilishuka tena msimu wa 2014/2015 na kufikia 42,768.0
na kupanda tena katika msimu wa 2015/2016 hadi tani 60,188.0 kabla ya
kuporomoka msimu wa 2016/2017 hadi tani 46,963.0.
Kaimu mkurugenzi huyo wa Bodi ya
kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo anasema uzalishaji wa kahawa katika msimu wa
2017/2018 unatarajiwa kushuka kutoka tani 46,963.msimu uliopita hadi
kufikia tani 43,000.
Amesema changamoto nyingine
inayochangia kushuka kwa uzalishaji ni pamoja uwekezaji kidogo kwenye
uzalishaji kutoka taasisi za fedha na wakulima wengi kutotumia kikamilifu
mashine za kati za kumenyea kahawa.
Kuhusu soko la nje,Italia imezipiku
nchini za Japan,Ujerumani,Marekani na Ubeligiji kutokana na kuongoza kununua
kahawa ya Tanzania kwa aslimia 25.18 ikifuatiwa na Japan(16.89%),Ujeruman(11.32%),Marekani(10.86%)
huku Ubeligiji ikishika nafasi ya tano kwa aslimia 9.41.
Wakati nchi hizo zikichuana kwenye
tano bora ya kununua kahawa ya Tanzania,nchi tano zimeibuka kama masoko mapya
ya kahawa ya Tanzania ambazo ni China,India,Urusi,Afrika Kusini na Australia.