Viongozi waandamizi wa serikali wametakiwa
kudumisha na kulinda amani ya nchi kwa kuruhusu uhuru wa kutoa maoni na
kuhimiza uvumilivu wa kisiasa miongoni mwa jamii.
Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na
watumishi wa Mungu wakati wa kusherekea siku kuu ya kuzaliwa kwa Yesu
(Christmas) ambayo husheherekewa Desemba 25 kila mwaka na wakristo wote
duniani.
Askofu Mkuu wa kanisa la Full Gospel Bible
Fellowship, Zachary Kakobe akihubiri katika ibada ya Krismasi jijini Dar es
Salaam, amesema viongozi wa serikali wanapaswa kutafakari misingi ya amani
iliyowekwa na waasisi wa taifa kwa kuheshimu utawala wa sheria na kujiepusha na
matendo yote yanayoweza kuitumbukiza nchi katika machafuko.
“Leo ni siku ya watawala wa Tanzania kutubu,
tumeanza kuona misingi ya amani ya nchi yetu ikitikiswa, amani iliyojengwa kwa
gharama kubwa na waasisi wetu; tumeanza kuona nchi hii ni ya chama kimoja, na
huu ni uovu”, amesema Askofu Kakobe.
Amesema misingi ya demokrasia ni pamoja na
kuruhusu wananchi kutoa maoni yanayolenga kuboresha mstakabali wa maisha yao.
Pia viongozi wanapaswa kukubali lawama na
mawazo tofauti na kuiga mfano wa Yesu Kristo ambaye alistahimili
matukano na maudhi kutoka kwa watu ambao walikuwa hawaikubali huduma yake
akiwa duniani.
“Mungu ana nguvu kuliko majeshi yote ya
nchi, lakini anatukanwa na bado hatumii majeshi yake, hata wewe unaweza ukawa
mvumilivu”, amesema.
Ameongeza kuwa nchi ya Tanzania iko kwenye
mfumo wa vyama vingi ambao unaruhusu vyama vyote kufanya shughuli zao bila kuingiliwa
na mamlaka husika na kuwataka watawala kuheshimu sheria zilizopo ili kujiweka
katika nafasi nzuri ya kutokuruhusu migogoro ya kisiasa inayoweza kuvuruga
amani ya nchi.
“Mungu mwenyewe anaheshimu sheria basi kama
na sisi tumeweka sheria tunapaswa kuheshimu sheria tulizo jiwekea wenyewe”,
amesema
Askofu Kakobe aliwaasa watawala kutoirudisha
nchi kwenye mfumo wa chama kimoja unaopingana na misingi ya kujieleza kwa
uwazi.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa
Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo akihubiri wakati
wa mkesha wa Krismasi katika Parokia ya Mtakatifu Maurus iliyopo Kurasini
amesema ili kudumisha misingi ya amani, wananchi wafanye kazi kwa bidii na
kujiletea maendeleo.
“Wakati umefika watu kufanya kazi usiku na
mchana, hilo likifanyika nchi itaendelea kuwa na amani. Muda wote uwe wa
kufanya kazi, tupumzike kidogo kwa ajili ya kupata usingizi”, amesema Askofu
Pengo.
Amebainisha kuwa amani ya nchi haijengwi na
viongozi waliopo madarakani bali na wananchi wenyewe kwa kufanya kazi na
kuachana na uvivu na malalamiko.
Pia amewataka wananchi kuwaombea viongozi ili
waongoze kwa hofu ya Mungu na kulifikisha taifa kwenye kilele cha maendeleo
yaliyokusudiwa.
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la
Zanzibar Mhashamu Augustino Shao amesema ipo haja kwa serikali na vyama
vya siasa kuelewa dhana ya demokrasia kutokana na mchango wake katika maendeleo
ya taifa.
pichani ni Askofu Mkuu Jimbo katoliki zanzibar,mhashamu Augustino Shao
“Kwa kiasi kikubwa vyama hivi vimeleta mwanga
na uwazi serikalini,chaguzi ndogo za madiwani huko bara ni ishara tosha kwamba
hatujafahamu maana ya demokrasia yaani kutofautiana lakini bado kubaki wamoja”,
amesema Askofu Shao.
Sherehe ya Krismasi
Krismas ni sherehe ambayo huwaunganisha
wakristo wote duniani kuazimisha siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo mwokozi wa
ulimwengu ambayo hufanyika Disemba 25 kila mwaka.
Siku
hii imekuwa ikiwakutanisha wakristo mbalimbali katika nyumba za ibada na
kutafakari maisha yao ya kiroho.
Lakini viongozi wa dini wanaitumia kutoa
matamko mbalimbali yanayolenga kuishauri na kuionya jamii juu ya mwenendo
usiofaa.
Misa ya kitaifa ilifanyika katika Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Joseph Minara Miwili lilipo Zanzibar ambapo wakristo na
viongozi mbalimbali wa serikali walijumuika pamoja katika kumbukumbu hiyo
muhimu duniani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni