Na Sitta Tumma, Mwanza
"TUNAMPONGEZA sana Mtukufu
Prince Karim Aga Khan na taasisi zake zote, kwa namna anavyowekeza miradi
mbalimbali ya maendeleo Tanzania.
"Kiongozi huyu kwanza ni mcha
Mungu, anapenda kuona jamii inapata maendeleo, amani na upendo kwa watu
wote."
Hii ni kauli ya Mwenyekiti Mwenza wa
Kamati ya Amani, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Mkoa wa Mwanza,
Askofu Charles Sekelwa, aliyoitoa mbele ya ujumbe wa kamati hiyo.
Kamati hiyo ya Amani, hivi karibuni
ilitembelea makumbusho ya Mtukufu Prince Aga Khan, yaliyopo jijini Mwanza,
ikiwa ni maadhimisho ya kusherehekea miaka 60 ya uongozi wake.
Maadhimisho hayo ya miaka 60 ya
Uimamu wa Aga Khan, yanakuja huku kiongozi huyo akiendelea kusifika duniani,
kutokana na dhamira yake ya kuiwezesha jamii kuwa na maisha bora! Ndiyo.
Katika ziara hiyo ya Wajumbe wa
Kamati ya Amani, walijionea historia ya kiongozi huyo wa kiroho wa Madhehebu ya
Kiislamu ya Shia Ismailia.
Pamoja na mambo mengine, viongozi wa
kamati hiyo walieleza kufurahishwa na uongozi wa kiongozi wa Aga Khan duniani.
Wenyeviti wa Kamati hiyo, Sheikh
Hassan Kabeke na mwenzake, Askofu Charles Sekelwa, wanasema taasisi hiyo
inayosimamia dhehebu la Ismailia inastahili kuigwa na jamii yote ulimwenguni.
"Kwanza ziara yetu kwenye
makumbusho haya imetupa elimu kubwa.
"Tumejifunza namna ya kuwa
kiongozi bora kwa waumini na kushiriki kwenye maendeleo.
"Mafanikio ya Mtukufu Aga Khan
yanatokana na uongozi wake kupenda watu, amani na maendeleo ya nchi na
mataifa," anasema Sheikh Kabeke.
Viongozi hao wanasema uongozi wa Aga
Khan umetamalaki katika nyanja ya amani, upendo na maendeleo kwa jamii.
Viongozi hao wanasema kuwa, taasisi
na viongozi wote wa madhehebu ya dini hawana budi kuiga uongozi na uwekezaji
miradi ya maendeleo, unaofanywa na Aga Khan kwa jamii ulimwenguni.
Naye Katibu wa Baraza la Waislamu
Mkoa wa Mwanza ( Bakwata), Sheikh
Mohamed Balla, alisisitiza pia suala la amani
na uwekezaji wa miradi ya kisekta Tanzania.
"Tumeona Mtukufu Aga Khan
anavyosaidia kuleta maendeleo katika nchi yetu. Jamii yote inapaswa kuiga mfano
mwema wa kiongozi huyo.
"Tunafurahi huyu kiongozi
anavyohimiza na kupenda amani duniani.
Amani ni kitu muhimu sana, tuilinde kwa
gharama zote," anasema Halima Jarufu, Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa
Mwanza.
AGA KHAN NI NANI?
Rais John Magufuli akimpokea Imamu wa waislamu wa Shia Ismailia Duniani,Mtukufu Aga Khan Ikulu Jijini Dar es salaam hivi karibuni,mtukufu Aga Khan alikuwa nchini kwa ziara ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais Magufuli.
Mtukufu Prince Aga Khan, alianza
kuwa Imamu wa Madhehebu ya Kiislamu ya Shia Ismailia, Julai 11,1957, akiwa
kijana mwenye umri wa miaka 20.
Alichukuwa nafasi hiyo kubwa kiimani
kutoka kwa babu yake, Sir Sultan Mohamed Shah Aga Khan.
Aga Khan ni kiongozi nayesifika
duniani kote, kutokana na huduma zake anazozitoa kwa jamii ya kimataifa!
Ni Imamu wa 49 wa Madhehebu hayo ya
Kiislamu ya Shia Ismailia.
Inaelezwa ana nasaba ya moja kwa
moja na Mtume Muhammad.
Tangu ashike nafasi ya Uimamu mwaka
1957, Prince Karim Aga Khan, amejielekeza katika ustawi wa Jumuiya ya Ismailia,
Jumuiya ya Kiislamu kwa upana wake, pamoja na jamii yote kwa ujumla.
Kiongozi huyu anasisitiza mtazamo wa
Kiislamu ni kama fikra, imani ya kiroho inayofundisha huruma, uvumilivu na
kutetea utu wa mtu.
Katika kizazi cha hivi karibuni,
familia ya Aga Khan imekuwa ikishiriki kutoa huduma za kijamii katika nyanja
mbalimbali za kimataifa.
Mfano, babu yake Aga Khan amewahi
kuwa Rais wa League of Nations.
Baba yake na Prince Aly Khan,
amehudumu nafasi ya Balozi wa Pakistan, katika Umoja wa Mataifa (UN).
Vivyo hivyo baba yake mdogo,
marehemu Prince Sadruddin Aga Khan, alikuwa Mratibu wa Shirika la UN
linaloshughulikia Wakimbizi.
Alikuwa akisaidia Afghanistan na
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, katika mipaka ya nchi za Iraq na Uturuki.
Aidha, amekuwa akifanya kazi na
Serikali tofauti kila moja ikiwa na matarajio yake.
Mtukufu Aga Khan amekuwa akilinda,
kutunza na kuzingatia siasa zisizoegemea upande wowote.
Amekuwa akiwekeza miradi mbalimbali
ya maendeleo nchini, ikiwamo sekta ya afya, elimu na masuala ya amani.
Maadhimisho hayo ya miaka 60 ya
Mtukufu Aga Khan yanasherehekewa kwa muda wa mwaka mmoja, kuanzia Julai 11,2017
hadi Julai 11 mwakani.
Kwamba, kiongozi huyo anatarajiwa
kuzuru nchi 35 duniani, kisha kufungua na kuweka mawe ya msingi ya miradi
mbalimbali ya maendeleo, ambapo atakutana na wanajumuiya ya Dini ya Ismailia
kwa nchi hizo.
Pamoja na hayo, taasisi hiyo
imejikita pia kuwekeza kwenye Sekta ya Elimu, ambapo imejenga shule mbalimbali
za msingi na sekondari.
Taasisi hiyo ya Aga Khan inayomiliki
shule mbalimbali ikiwamo ya Aga
Khan Mzizima Sekondari, pia ina walimu 900
Visiwani Zanzibar.
Maimamu wa Wanizari walianza kutumia
cheo cha Aga Khan wakati wa karne ya 19 ambako Hasan Ali Shah aliyehesabiwa
kama imamu wa 46 wa Kiismaili alipewa cheo hiki na mfalme au shah wa Uajemi.
AGA KHAN
1: Aga Khan I - Hasan
Ali Shah Mehalatee (1800–1881), Imamu wa 46 wa Kiismaili (1817–1881).
2: Aga Khan II - Ali
Shah (~1830–1885), Imamu wa 47 wa Kiismaili (12 Aprili 1881–1885).
3: Aga Khan III - Prince
Sultan Mohammed, (1877–1957), Imamu wa 48 wa Kiismaili (17 Agosti 1885–1957).
4: Aga Khan IV - Prince
Karim Al Husseini (b. 1936),Imamu wa 49 wa Kiismaili (tangu 11 Julai 1957)
UWEKEZAJI
Katika kusimamia misingi yake,
taasisi hiyo ya Maendeleo ya Aga Khan (AKDN) imejikita kusaidia upatikanaji wa
maendeleo ya jamii, kwa kuwekeza miradi ya afya na elimu nchini.
Kwamba, imetenga dola za Kicanada
milioni 15, kuboresha hospitali za wilaya zilizopo mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mpango huo umelenga kusaidia jamii
kupata huduma bora zaidi za kiafya, zikiwamo vipimo.
Taarifa ya Aga Khan inasema kuwa,
mbali na taasisi hiyo kuwa mdau mkubwa wa maendeleo duniani kote, inahitaji
kuona Watanzania wakiishi salama kiafya, kielimu, upendo na utulivu.
"Tayari tumefungua kituo cha
afya Buzuruga Mwanza na Kahama Mkoa wa Shinyanga. Desemba 2017 tutafungua
Tabora na Bukoba
"Mwaka 2018 tutafungua pia
huduma za afya Bunda Mkoa wa Mara.
Mwaka 2019 tutafungua Simiyu na Kigoma
," anasema Altaf Hiran Mansoor, Rais wa Aga Khan Kanda ya Ziwa na
kuongeza:
"Tayari programu hii ya
maboresho ya hospitali za wilaya za Serikali, inashafanyiwa tathmini."
CHUO KIKUU
Katika kupigania maendeleo, Aga Khan
University
inakusudia kujenga Chuo Kikuu cha Afya na Elimu nchini, kitakachokuwa cha pili duniani.
inakusudia kujenga Chuo Kikuu cha Afya na Elimu nchini, kitakachokuwa cha pili duniani.
Hivi karibu, Serikali ya Rais Dk.
John Magufuli, ilikaririwa ikisema chuo hicho kitajengwa Arusha-Tanzania.
Chuo cha kwanza dunini kipo nchini
Pakistan. Kitagharimu zaidi ya dola za Kimarekani milioni 300, sawa na Sh.
Bilioni 660 za Kitanzania.
Taratibu za ujenzi wake zinatarajiwa
kuanza miezi sita ijayo kuanzia sasa. Kukamilika kwake kitabadili sura ya
Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Taarifa zinasema kwamba, Chuo Kikuu
hicho kitapokea wanafunzi si tu Tanzania, bali kutoka Afrika Mashariki, SADC na
duniani kote.
Aga Khan imekuwa ikihudumia
maendeleo ya jamii kwa nchi 35 duniani, zioizopo Asia Kusini, Asia ya Kati,
Mashariki ya Kati, Ulaya, Amerika Kaskazini na Bara la Afrika.
HOSPITAL
Mbali na chuo hicho kikuu, Taasisi
hiyo ya Aga Khan pia imenuia kujenga hospitali kubwa kwa mikoa ya Kanda ya
Ziwa.
Mansoor anasema hospitali hiyo
itakayojengwa Mkoa wa Mwanza, itagharimu dola za Kimarekani milioni 5.5 ,
sawa na Sh. Bilioni 12 za Kitanzania.
"Hospitali yetu ya Dar es Salaam
watu zaidi ya 4,000 wanatibiwa kwa gharama nafuu kila mwaka," anasema Rais
wa Taasisi ya Aga Khan Kanda ya Ziwa, Altaf Hiran Mansoor.
Baadhi ya wagonjwa wanaopata huduma
katika Hospitali ya Aga Khan jijini Mwanza, wanaeleza kufurahishwa na huduma
bora zinazotolewa hopitalini hapo.
"Ukweli Hospitali ya Aga Khan
ina huduma nzuri sana, bei zake nafuu na huduma ni bora.
"Mgonjwa unafika unapokelewa
vizuri hadi unajisikia raha," anasema Asha Haruna, mkazi wa Mabatini
jijini hapa.
Mzee Joshua John (78) yeye anasema:
"Familia hata wajukuu zangu nilishaelekeza watibiwe Hospitali za Aga Khan
popote watakapokuwa. Huduma zao nzuri sana."
Anasema kuwa, hivi sasa hospitali
hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa 160-180 kwa siku moja, tofauti ilivyokuwa Kituo
cha Afya.
Mtukufu Aga Khan(kulia)akizungumza na Waziri wa Elimu,Profesa Joyce Ndalichako baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam hivi karibuni,Aga Khan alikuwa nchini kwa mwaliko wa Rais John magufuli(picha zote kwa hisani ya Ikulu) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni