Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza(pichani na mkewe)
amezindua kampeni ya kufanyika kwa kura ya maamuzi ambayo inatazamwa na jaribio
la kutaka kusalia madarakani hadi 2034.
Shirika la habari la AFP linasema
mpango huo unahusisha kuidhinishwa kwa rasimu ya katiba ambayo itamuwezesha
kuwania urais kwa mihula miwili zaidi ya miaka saba kila muhula.
Muhula wa sasa wa Bw Nkurunziza
unafikia kikomo 2020.
Rais huyo aliwaambia wafuasi wake
Jumanne wiki hii katika kijiji cha Gitega kwamba wale wanaopinga juhudi zake "kwa
maneno au kwa vitendo" watakuwa wameuvuka "mstari mwekundu".
Kampeni hiyo imeanzishwa baada ya
serikali kuzindua juhudi za kuchangisha fedha za maandalizi ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2020.
Shirika la habari la AFP linasema
mchango huo, ambao serikali inasema ni wa hiari, umeshutumiwa na makundi ya
kutetea haki za kibinadamu ambayo yamesema ni kama "wizi kwa mpango".
Viongozi wa upinzani walio
uhamishoni wanasema kura hiyo ya maoni itakuwa kama "mazishi" kwa
mwafaka wa amani uliotiwa saini mwaka 2000 nchini humo.
Mkataba huo wa amani ulisaidia
kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 13 na kusababisha
vifo vya watu 300,000.
Burundi ilitumbukia kwenye mzozo
mwingine wa kisiasa mwaka 2015 wakati Rais Nkurunziza alipokataa kung'atuka
baada ya kumaliza muhula wake na akaamua kuwania tena urais.
Mwaka huo pia kulitekelezwa jaribio la kuipindua serikali ya Bw Nkurunziza ambalo halikufanikiwa.
Mzozo huo ulisababisha mashambulio
ya mara kwa mara ambayo yamechangia vifo vya watu karibu 2,000 na wengine
maelfu kutoroka makwao na kukimbilia nchi jirani ikiwamo Tanzania.
Mazungumzo ambayo yamekuwa
yakiendelea kati ya serikali na makundi ya upinzani yalisambaratika wiki
iliyopita.
Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania ,Benjamin Mkapa aliyekuwa
anafanikisha mazungumzo hayo alisema hakukuwa na "makubaliano yoyote,
maazimio yoyote au stakabadhi yoyote ya kuwafungamanisha wadau".
FAHAMU KUHUSU JAMHURI YA BURUNDI
Milioni 10.4 Idadi ya watu nchini Burundi - sawa na
Ubelgiji
Kilomita
mraba 27,816 Ukubwa wa nchi ya Burundi - sawa na Haiti
Miaka
50 Muda wa kuishi kwa wanaume
Miaka
50 Muda wa kuishi kwa wanawake
$900
GDP - sawa na Liberia
Chanzo:BBC Swahili.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni