MAOFISA watatu wa Chama Cha walimu
cha Akiba na Mikopo(SACCOS) Manispaa ya Moshi,wamefikishwa mahakamani
wakikabiliwa na mashitaka 285 ya kushughi nyaraka na kuiibia saccos hiyo zaidi
ya shilingi milioni 50.
Maofisa hao ni Gerald Thomas Msacky
aliyekuwa Ofisa mikopo,Peter Thadeus Ndalianarua ambaye alikuwa mhasibu na
Rehema Lucas Mlay aliyekuwa karani wa fedha.
Walifikishwa makahamani hapo chini
ya ulinzi wa maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini
(TAKUKURU), mkoani Kilimanjaro na kusomewa mashitaka hayo mbele ya hakimu Mkazi mfawidhi ,Aidan Mwilapwa.
Katika kesi hiyo namba 22 ya mwaka
2017 ,washitakiwa walisomewa mashitaka hayo na mawakili na wanasheria kutoka Takukuru,
Suzan Kimaro akisaidiana na Barry Galinoma.
Wakisoma hati ya mashitaka waendesha
mashitaka hao walidai kuwa, washitakiwa hao kwa pamoja walitenda makosa hayo ya
ubadhirifu na ufujaji wa fedha za chama hicho cha kuweka na kukopa, huku pia
wakishitakiwa kwa makosa manne ya
kughushi nyaraka za malipo.
Mshitakiwa wa kwanza katika kesi
hiyo,Peter Thadeus Ndelianarua ambaye alikuwa mhasibu wa chama hicho na mshitakiwa
wa tatu Rehema Lucas Mlay aliyekuwa karani wa fedha wa chama hicho, kwa pamoja
wanakabiliwa na mashitaka 142.
Kwa upande wa mshitakiwa wa
pili,Gerald Thomas Msacky ambaye alikuwa ni ofisa mikopo wa SACCOS hiyo,yeye
anakabiliwa na mashitaka 282 ambayo yanahusu
ubadhilifu wa fedha za chama hicho pamoja na kughushi nyaraka za malipo.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka
washitakiwa hao kwa nyakati tofauti tofauti kati ya januari na desemba mwaka
2012 kwa kutumia nyaraka za kughushi malipo waliweza kufuja fedha za chama
hicho cha kuweka na kukopa zaidi ya shilingi milioni 50.
Washitakiwa hao ambao wanashitakiwa chini ya
kifungu cha 28 kifungu kidogo cha 2 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa
sheria namba 11 ya mwaka 2007 katika makosa 281 ya ubadhirifu wa fedha.
Pia washitakiwa hao wanashitakiwa
chini ya vifungu namba 333, 335(a), na 337 vya kanuni ya adhabu 16 kama
ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, ambapo
makosa 4 ya kughushi nyaraka wanayotuhumiwa nayo.
Washitakiwa hao walikana mashitaka
yao yote na wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza mashariti ya dhamana
yaliyowata kila mmoja kuwa na wadhamini wawili waliosaini dhamana ya maneno
kiasi cha shilingi milioni 6 kila mmoja,kesi hiyo imeahirishwa hadi desemba 28
mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni