Jumatano, 27 Desemba 2017

DK.MWANJELWA ATAKA MAELEZO KUSHUKA KWA BEI YA KAHAWA YA TANZANIA SOKO LA DUNIA



 Na Charles Ndagulla,Moshi.

NAIBU Waziri wa Kilimo,Dk.Mary  Mwanjelwa,ameitaka bodi ya Kahawa Tanzania(TCB) kutoa taarifa ni kwa nini kahawa ya Tanzania imekosa bie nzuri kweneo soko la dunia huku kahawa hiyo ikitajwa kuwa na ubora wa hali ya juu.

Dk.Mwajelwa alikuwa mkoani Kilimanjaro hivi karibuni kwa ziara ya sku moja ambako alipata fursa ya kutembelea makao makuu ya Bdi hiyo yaliyopo mjini moshi na kupata taarifa  za utekelezaji wa shughuli za bodi hiyo.

Amesema bei  ya kahawa ikiwa nzuri maisha ya wakulima wa zao hilo yatakuwa mazuri lakini bei hiyo ikiyumba kwenye soko la dunia hata hapa nchini bei ya zao hilo itakuwa mbaya.

“Lakini lazima pia tuangalie kwa makini aina ya uvundikaji wa kahawa na uandaaji usiozingatia ubora unaweza kuwa chanzo cha kahawa yetu kukosa bei nzuri,kwa hiyo ninyi kama bodi ni mhimu mkatuletea taarifa ni kwa nini bei ya kahawa yetu imeshuka kwenye soko la dunia”,amesema.

Dk.Mwanjelwa aliitaka bodi hiyo kuwa na mikakati ya dhati ya kulipeleka mbele zao la kahawa na kuwa na heshima na thamani  kama ilivyo kwa zao la korosho na kuhoji kama kahawa ya Tanzania ina ubora wa juu ni kwa nini haipati bei nzuri kwenye soko la dunia.

Aliitaka bodi hiyo kutochelewesha malipo ya wakulima pindi kahawa yao inapouzwa mnadani na kuonya kuwa wakulima wasipolipwa malipo yao kwa wakati wanaweza wakajenga chuki dhidi ya serikali yao.

“Awamu hii ya tano ni lazima kila mtumishi ajiongeze,wakati wa kufanyakazi kwa mazoea umepitwa na wakati,ninyi bodi ya kahawa mmepewa mamlaka ya kusimamia zao la kahawa sasa naomba msisubiri kuamshwa”,alionya.

Katika taarifa yake kwa naibu waziri huyo,kaimu mkurugenzi wa bodi ya kahawa,Primus Kimaryo alisema kuwa,katika msimu wa 2016/2017 wakulima waliouza kahawa yao wakati bei ikiwa nzuri sokoni walipata wastani wa shilingi 5,000.

Alisema wastani wa bei kwa msimu ni shilingi 4,000 kwa kahawa ya Arabika huku wakulima wanaozalisha kahawa aina ya Robusta walilipwa wastani wa shilingi 1,200 hadi 1,400 kwak ilo ya maganda.
 Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo(kulia)akimweleza jambo Naibu Waziri wa Kilimo,Dk.Mary Mwanjelwa(kushoto)ambaye alifanya ziara ya siku moja katika makao makuu ya Bodi hiyo mjini Moshi hivi karibuni.

“Msimu huu 2017/2018 bei ya kahawa imeshuka kutokana na kushuka kwa bei ya kahawa katika soko la dunia,bei ya mkulima imekuwa ni ya wastani kutokana na ushindani unaotokana na kiwango kidogo cha uzalishaji “,alisema.

Hata hivyo Kimaryo alisema kuwa kuyumba kwa uzalishaji na ubora kunaathiri bei ya mkulima huku soko la mnada likimikiwa na makampuni machache ya nje pamoja na vyama vya ushirika na vikundi vya wkulima kutotumia fursa ya uongezaji thamani wa zao.

Kuhusu changamoto za masoko,kaimu mkurugenzi huyo amesema soko la DE ambalo lilianzishwa kwa ajili ya kumsaidia mkulima kwa kuuza kahawa za ubora wa juu,linatumiwa kwa kiasi kikubwa na makampuni yanayonunua kahawa vijijini.

Amesema wakulima wazalishaji hawanufaiki ipasavyo na soko hilo na kwmaba dirisha hilo siyo mbadala wa mnada huku vyama vya msingi vya ushirika vikishindwa kuwasaidia ipasavyo wakulima kutokana na kukumbwa na matatizo ya uendeshaji.

“Mheshimiwa naibu waziri,pia zipo changamoto za uchanganyaji wa kahawa zenye ubora tofauti,kutegemea soko la nje kwa aslimia tisini huku matumizi ya CPU yakiwa chini pamoja na upatikanaji wa magunia ya kahawa kutokuwa na uhakika”,amesema.


HALI YA UZALISHAJI WA KAHAWA NCHINI 

Kuhusu hali ya uzalishaji wa kahawa nchini,kaimu mkurugenzi huyo alimweleza naibu waziri kuwa mwaka 2011 wadau wa kahawa waliandaa na kupitisha  mkakati  wa miaka  kumi wa maendeleo ya kahawa .

Alisema lengo kuu la mkakati huo ilikuwa ni kuendeleza zao hilo kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kahawa na kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 80,000 mwaka huu na tani 100,000 ifikapo mwaka 2021 lakini alikiri kuwa lengo hilo halijafikiwa.

Alisema kutokana na kukwama kwa lengo hilo,mkakati huo umefanyiwa marejeo ya muda wa kati na mshauri mwelekezi aliyefanya kazi hiyo ameshakamilisha kazi yake .
 
Lengo jingine la  mkakati huo ilikuwa ni  kuongeza uzalishaji,tija na ubora wa kahawa na kuboresha mapato katika mnyororo wote wa thamani hususani wakulima wa kahawa  na  kuwezesha kahawa ya Tanzania kupata bei nzuri kwenye soko la dunia.

Alitaja changamoto nyingine zilizokwaza  mkakati huo  kuwa ni pamoja na tija ndogo ya uzalishaji inayochangiwa na matumizi kidogo ya pembejeo hususani mbolea .


Sababu nyingine zilizokwaza mkakati huo zinatajwa kuwa ni kasi ndogo ya kupokea matokoeo ya utafiti,mabadiliko ya tabianchi yanayaodaiwa kusababisha mvua zisizo na mpangilio pamoja na uwekezaji mdogo ikilinganishwa na malengo ya mkakati huo.

Uchunguzi wa jamhuri umebaini kuwa,katika misimu saba iliyopita uzalishaji wa zao la kahawa nchini umekuwa ukipanda na kushuka huku baadhi ya wakulima wakidaiwa kulipa kisogo zao hilo na kugeukia mazao mseto kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na bei ndogo.

Katika msimu wa 2010/2011 uzalishaji wa kahawa ulikuwa tani 56,790.0 lakini msimu uliofuata wa 2011/2012 uzalishaji ulishuka kwa kasi ya kutisha na kufikia tani 33,086.7 na ulipanda tena msimu wa 2012/2013 na kufikia tani 71,319.1.

Msimu wa 2013/2014 tani 48,761.9 zilizalishwa na tani hizo zilishuka tena msimu wa 2014/2015 na kufikia 42,768.0 na kupanda tena katika msimu wa 2015/2016 hadi tani 60,188.0 kabla ya kuporomoka msimu wa 2016/2017 hadi tani 46,963.0.

Kaimu mkurugenzi huyo wa Bodi ya kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo anasema uzalishaji wa kahawa katika msimu wa 2017/2018 unatarajiwa kushuka kutoka tani 46,963.msimu uliopita  hadi kufikia tani 43,000.

Amesema changamoto nyingine inayochangia kushuka kwa uzalishaji ni pamoja uwekezaji kidogo kwenye uzalishaji kutoka taasisi za fedha na wakulima wengi kutotumia kikamilifu mashine za kati za kumenyea kahawa.


Kuhusu soko la nje,Italia imezipiku nchini za Japan,Ujerumani,Marekani na Ubeligiji kutokana na kuongoza kununua kahawa ya Tanzania kwa aslimia 25.18 ikifuatiwa na Japan(16.89%),Ujeruman(11.32%),Marekani(10.86%) huku Ubeligiji ikishika nafasi ya tano kwa aslimia 9.41.


Wakati nchi hizo zikichuana kwenye tano bora ya kununua kahawa ya Tanzania,nchi tano zimeibuka kama masoko mapya ya kahawa ya Tanzania ambazo ni China,India,Urusi,Afrika Kusini na Australia.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni