Jumamosi, 30 Desemba 2017

UJENZI WA NYUMBA SASA KWA KIBALI,WATAKAOPUUZA KUKIONA



Na Kija Elias, Hai.

Baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, limepitisha sheria ndogo ndogo zikiwemo sheria za vibali vya ujenzi vinayomtaka kila mwananchi ambaye anataka kujenga lazima awe na kibali cha ujenzi huo. 

Sheria hiyo imepitishwa jana, kufuatia agizo lililotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambalo alilitoa hivi karibuni la kuwataka viongozi wa Halmashauri za wilaya,miji Majiji nchini, kuharakisha utoaji wa vibali vya ujenzi na kuachana na urasimu ambao ulikuwa ukisababisha kuwepo kwa ujenzi holela. 

Akisoma sheria hizo kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Afisa Ardhi wa wilaya hiyo Jacob Muhumba, alisema kuwa mtu yeyote atakaye jenga bila kuwa na kibali cha ujenzi sheria hiyo imeweka adhabu kali ikiwa ni pamoja na kusitisha ujenzi wake na kufikishwa katika vyombo vya dola. 

“Sheria hii inamtaka kila mtu anayetaka kujenga ni lazima awe na kibali cha ujenzi, hatutamruhusu mtu kujenga bila kuwa na kibali, na kila mtu atakayekuwa anaomba kibali cha ujenzi atalazimika kulipia gharama  kwa ajili ya kupata kibali hicho,”alisema Muhumba. 

“Tulikuwa hatuna sheria ya vibali vya ujenzi tangu zamani, lakini pia tulikuwa hatutozi gharama yeyote ile, hivyo mwananchi alikuwa akijijengea tu bila kufuata utaratibu hali ambayo imechangia kuwepo kwa makazi holela,”alisema. 

Aidha alifafanua kuwa gharama hizo za kupata kibali cha ujenzi kitategemea na kile mtu anachotaka kujenga , ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi, maghala, viwanja vya ndege na majengo ya biashara . 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Helgha Mchomvu alisema kuwa baraza hilo limelazimika kuipitisha  sheria hiyo ili kuepusha ujenzi holela ambao umekuwa ukifanyika na hivyo kuufanya mji wa Bomang’omba kutokuwa katika mpangilio mzuri. 

Katika hatua nyingine halmashauri hiyo ya wilaya ya Hai,imeshindwa kufikia lengo la kukusanya mapato ya shilingi Bilioni 2.5 kutokana na baadhi ya vyanzo vya mapato vya halmashauri hiyo kuchukuliwa na serikali Kuu.
  

“Ukusanyaji wa mapato umeshuka kutoka bilioni 2.5 hadi kufikia bilioni 2.1 hii imechangiwa na serikali kuu kuchukua vyanzo vyetu ambavyo tulikuwa tukikusanya, hivyo kupitishwa kwa sheria ya kuwa na kibali cha ujenzi itasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato,”alisema mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Wakizungumzia hatua ya kuwepo na sheria ya vibali katika ujenzi wa nyumba baadhi ya wakazi wa  mji wa Boma ng’ombe, kuhusu  wamesema kuwa itasaidia sana kwani kumekuwepo na ujenzi holela ambao unachangia kuharibu mandhari ya mji huo.

Gidion Lucas na Issaya Fabiani, walisema kumekuwepo na ucheleweshaji mkubwa wa kupata vibali vya ujenzi unaosababishwa na wahusika wenyewe na hivyo kuchangia wananchi kujenga kiholela bila kufuata utaratibu, kutokana na kuchoka kusubiri  kwa muda mrefu ili waweze kupata vibali vya ujenzi.



Alhamisi, 28 Desemba 2017

MTUMISHI WA MFUKO WA PENSHENI KWA WATUMISHI WA UMMA PPF ALIYENASWA NA SHEHENA YA DAWA ZA KULEVYA AENDELEA KUSOTA RUMANDE

Mtuhumiwa wa dawa za Kulevya aina ya Mirungi,Anitha Osward ambaye ni mtumishi wa Mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa umma(P P F) mkoani Kilimanjaro akiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kukamatwa akituhumiwa kusafrisha shehena ya dawa za kulevya,alikamatwa Desemba 19,2017 eneo la Majengo kwa Mtei mjini Moshi.
 Anitha Osward mkazi wa karanga Manispaa ya Moshi ,mtuhumiwa wa dawa za kulevya akiwa haamini kilichotokea baada ya kukamatwa na makachero wa polisi akituhumiwa kujihusisha na usafrishaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi.
 Shehena ya mirungi ikiwa kituo cha polisi baada ya kukamatwa ikisafrishwa ndani ya gari aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674 DLB linaloaminika kumilikiwa na mtumishi wa mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa umma(P P F),Anitha Osward.
 Shehena ya Mirungi ikiwa ndani ya gari lenye namba za usajili T674 DLB aina ya Toyota Sienta baada ya kukamatwa na polisi hivi karibuni eneo la Majengo Kwa Mtei nje kidogo ya mji wa moshi.
 Gari aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674 DLB likivutwa baada ya kupata ajari eneo la Majengo kwa Mtei mjini Moshi,gari hilo lilikamatwa na polisi likiwa na hsehena ya dawa la kulevya aina ya Mirungi.
 Gari aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T674 DLB likiwa kituo cha polisi mjini moshi baada ya kukamatwa likiwa na kilo 216 na gramu 370 za dawa kulevya aina ya mirungi .
 Kama inavyyonekana nyuma ya buti ya gari lenye namba za usajili T674 DLB aina ya Toyota Sienta ni shehena ya dawa za kulevya aina ya mirungi baada ya kukamatwa na polisi hivi karibuni ikisafrishwa na mtumishi wa shirika la umma(P P F),Anitha Osward.




 TAARIFA YA JESHI LA POLISI KILIMANJARO JUU YA KUKAMATWA KWA SHEHENA YA DAWA ZA KULEVYA IKISAFRISHWA NA MTUMISSHI WA MFUKO WA PENSHENI KWA WATUMISHI WA UMMA(P P F) ANITHA OSWARD.


JESHI la polisi mkoani Kilimanjaro, linamshikilia mfanyakazi mmoja wa mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma(PPF) kwa tuhuma za kujihusiha na usafirishaji wa dawa za kulevya. 


Mtumishi huyo,Anitha Osward(32)alikamatwa desemba 19 mwaka jana akiwa na shehena ya madawa ya kulevya aina ya mirungi aliyokuwa akiisafrisha kwa kutumia gari lake dogo aya ya Toyota Sienta lenye namba za usjaili T674DLB.

 Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro,Hamis Issah,mtuhumiwa huyo ambaye bado anashikiliwa na jeshi la polisi mpaka sasa,alikamatwa na askari waliokuwa doria.

“Askari wakiwa doria walimkamata Anitha Oswald, ambaye ni mkazi wa Karanga, Manispaa ya Moshi, akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 216 na gramu 370”, alisema kamanda Issa. 

Kamanda Issa alisema Anitha Oswald alikamatwa eneo la Majengo kwa Mtei Disemba 19, mwaka jana, akiwa anatokea Njia Panda ya Himo kuchukua mzigo huo. 

Aidha kamanda Issa alisema kwamba usafirishaji wa dawa za kulevya bado ni changamoto kubwa ambapo alielezea kusikitishwa na tabia ya baadhi ya watumishi wa Umma kujihusisha na usafirishaji huo.

“Jeshi la polisi mkoani hapa liko makini, operesheni inaendelea na hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atabainika kujihusisha na biashara hii”, alisema.

Hata hivyo kamanda aliongeza kusema kwamba jeshi hilo la polisi mkoni kilimanjaro, bado linaendelea kumtafuta dereva wa gari hilo, ambaye alikimbia baada ya kulitelekeza gari alilokuwa akiliendesha baada ya kugonga mti katika jitihada za kuwakimbia polisi.


 imeandaliwa na Charles Ndagulla,Moshi










Jumatano, 27 Desemba 2017

DK.MWANJELWA ATAKA MAELEZO KUSHUKA KWA BEI YA KAHAWA YA TANZANIA SOKO LA DUNIA



 Na Charles Ndagulla,Moshi.

NAIBU Waziri wa Kilimo,Dk.Mary  Mwanjelwa,ameitaka bodi ya Kahawa Tanzania(TCB) kutoa taarifa ni kwa nini kahawa ya Tanzania imekosa bie nzuri kweneo soko la dunia huku kahawa hiyo ikitajwa kuwa na ubora wa hali ya juu.

Dk.Mwajelwa alikuwa mkoani Kilimanjaro hivi karibuni kwa ziara ya sku moja ambako alipata fursa ya kutembelea makao makuu ya Bdi hiyo yaliyopo mjini moshi na kupata taarifa  za utekelezaji wa shughuli za bodi hiyo.

Amesema bei  ya kahawa ikiwa nzuri maisha ya wakulima wa zao hilo yatakuwa mazuri lakini bei hiyo ikiyumba kwenye soko la dunia hata hapa nchini bei ya zao hilo itakuwa mbaya.

“Lakini lazima pia tuangalie kwa makini aina ya uvundikaji wa kahawa na uandaaji usiozingatia ubora unaweza kuwa chanzo cha kahawa yetu kukosa bei nzuri,kwa hiyo ninyi kama bodi ni mhimu mkatuletea taarifa ni kwa nini bei ya kahawa yetu imeshuka kwenye soko la dunia”,amesema.

Dk.Mwanjelwa aliitaka bodi hiyo kuwa na mikakati ya dhati ya kulipeleka mbele zao la kahawa na kuwa na heshima na thamani  kama ilivyo kwa zao la korosho na kuhoji kama kahawa ya Tanzania ina ubora wa juu ni kwa nini haipati bei nzuri kwenye soko la dunia.

Aliitaka bodi hiyo kutochelewesha malipo ya wakulima pindi kahawa yao inapouzwa mnadani na kuonya kuwa wakulima wasipolipwa malipo yao kwa wakati wanaweza wakajenga chuki dhidi ya serikali yao.

“Awamu hii ya tano ni lazima kila mtumishi ajiongeze,wakati wa kufanyakazi kwa mazoea umepitwa na wakati,ninyi bodi ya kahawa mmepewa mamlaka ya kusimamia zao la kahawa sasa naomba msisubiri kuamshwa”,alionya.

Katika taarifa yake kwa naibu waziri huyo,kaimu mkurugenzi wa bodi ya kahawa,Primus Kimaryo alisema kuwa,katika msimu wa 2016/2017 wakulima waliouza kahawa yao wakati bei ikiwa nzuri sokoni walipata wastani wa shilingi 5,000.

Alisema wastani wa bei kwa msimu ni shilingi 4,000 kwa kahawa ya Arabika huku wakulima wanaozalisha kahawa aina ya Robusta walilipwa wastani wa shilingi 1,200 hadi 1,400 kwak ilo ya maganda.
 Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo(kulia)akimweleza jambo Naibu Waziri wa Kilimo,Dk.Mary Mwanjelwa(kushoto)ambaye alifanya ziara ya siku moja katika makao makuu ya Bodi hiyo mjini Moshi hivi karibuni.

“Msimu huu 2017/2018 bei ya kahawa imeshuka kutokana na kushuka kwa bei ya kahawa katika soko la dunia,bei ya mkulima imekuwa ni ya wastani kutokana na ushindani unaotokana na kiwango kidogo cha uzalishaji “,alisema.

Hata hivyo Kimaryo alisema kuwa kuyumba kwa uzalishaji na ubora kunaathiri bei ya mkulima huku soko la mnada likimikiwa na makampuni machache ya nje pamoja na vyama vya ushirika na vikundi vya wkulima kutotumia fursa ya uongezaji thamani wa zao.

Kuhusu changamoto za masoko,kaimu mkurugenzi huyo amesema soko la DE ambalo lilianzishwa kwa ajili ya kumsaidia mkulima kwa kuuza kahawa za ubora wa juu,linatumiwa kwa kiasi kikubwa na makampuni yanayonunua kahawa vijijini.

Amesema wakulima wazalishaji hawanufaiki ipasavyo na soko hilo na kwmaba dirisha hilo siyo mbadala wa mnada huku vyama vya msingi vya ushirika vikishindwa kuwasaidia ipasavyo wakulima kutokana na kukumbwa na matatizo ya uendeshaji.

“Mheshimiwa naibu waziri,pia zipo changamoto za uchanganyaji wa kahawa zenye ubora tofauti,kutegemea soko la nje kwa aslimia tisini huku matumizi ya CPU yakiwa chini pamoja na upatikanaji wa magunia ya kahawa kutokuwa na uhakika”,amesema.


HALI YA UZALISHAJI WA KAHAWA NCHINI 

Kuhusu hali ya uzalishaji wa kahawa nchini,kaimu mkurugenzi huyo alimweleza naibu waziri kuwa mwaka 2011 wadau wa kahawa waliandaa na kupitisha  mkakati  wa miaka  kumi wa maendeleo ya kahawa .

Alisema lengo kuu la mkakati huo ilikuwa ni kuendeleza zao hilo kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kahawa na kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 80,000 mwaka huu na tani 100,000 ifikapo mwaka 2021 lakini alikiri kuwa lengo hilo halijafikiwa.

Alisema kutokana na kukwama kwa lengo hilo,mkakati huo umefanyiwa marejeo ya muda wa kati na mshauri mwelekezi aliyefanya kazi hiyo ameshakamilisha kazi yake .
 
Lengo jingine la  mkakati huo ilikuwa ni  kuongeza uzalishaji,tija na ubora wa kahawa na kuboresha mapato katika mnyororo wote wa thamani hususani wakulima wa kahawa  na  kuwezesha kahawa ya Tanzania kupata bei nzuri kwenye soko la dunia.

Alitaja changamoto nyingine zilizokwaza  mkakati huo  kuwa ni pamoja na tija ndogo ya uzalishaji inayochangiwa na matumizi kidogo ya pembejeo hususani mbolea .


Sababu nyingine zilizokwaza mkakati huo zinatajwa kuwa ni kasi ndogo ya kupokea matokoeo ya utafiti,mabadiliko ya tabianchi yanayaodaiwa kusababisha mvua zisizo na mpangilio pamoja na uwekezaji mdogo ikilinganishwa na malengo ya mkakati huo.

Uchunguzi wa jamhuri umebaini kuwa,katika misimu saba iliyopita uzalishaji wa zao la kahawa nchini umekuwa ukipanda na kushuka huku baadhi ya wakulima wakidaiwa kulipa kisogo zao hilo na kugeukia mazao mseto kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na bei ndogo.

Katika msimu wa 2010/2011 uzalishaji wa kahawa ulikuwa tani 56,790.0 lakini msimu uliofuata wa 2011/2012 uzalishaji ulishuka kwa kasi ya kutisha na kufikia tani 33,086.7 na ulipanda tena msimu wa 2012/2013 na kufikia tani 71,319.1.

Msimu wa 2013/2014 tani 48,761.9 zilizalishwa na tani hizo zilishuka tena msimu wa 2014/2015 na kufikia 42,768.0 na kupanda tena katika msimu wa 2015/2016 hadi tani 60,188.0 kabla ya kuporomoka msimu wa 2016/2017 hadi tani 46,963.0.

Kaimu mkurugenzi huyo wa Bodi ya kahawa nchini(TCB),Primus Kimaryo anasema uzalishaji wa kahawa katika msimu wa 2017/2018 unatarajiwa kushuka kutoka tani 46,963.msimu uliopita  hadi kufikia tani 43,000.

Amesema changamoto nyingine inayochangia kushuka kwa uzalishaji ni pamoja uwekezaji kidogo kwenye uzalishaji kutoka taasisi za fedha na wakulima wengi kutotumia kikamilifu mashine za kati za kumenyea kahawa.


Kuhusu soko la nje,Italia imezipiku nchini za Japan,Ujerumani,Marekani na Ubeligiji kutokana na kuongoza kununua kahawa ya Tanzania kwa aslimia 25.18 ikifuatiwa na Japan(16.89%),Ujeruman(11.32%),Marekani(10.86%) huku Ubeligiji ikishika nafasi ya tano kwa aslimia 9.41.


Wakati nchi hizo zikichuana kwenye tano bora ya kununua kahawa ya Tanzania,nchi tano zimeibuka kama masoko mapya ya kahawa ya Tanzania ambazo ni China,India,Urusi,Afrika Kusini na Australia.




Jumanne, 26 Desemba 2017

VIONGOZI WA DINI WAHIMIZA WATAWALA KULINDA MISINGI YA DEMOKRASIA NCHINI

Viongozi waandamizi wa serikali wametakiwa kudumisha na kulinda amani  ya nchi kwa kuruhusu uhuru wa kutoa maoni na kuhimiza uvumilivu wa kisiasa miongoni mwa jamii. 

Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na watumishi wa Mungu wakati wa kusherekea siku kuu ya kuzaliwa kwa Yesu (Christmas) ambayo  husheherekewa  Desemba 25 kila mwaka na wakristo wote duniani.

Askofu Mkuu wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe akihubiri katika ibada ya Krismasi jijini Dar es Salaam, amesema viongozi wa serikali wanapaswa kutafakari misingi ya amani iliyowekwa na waasisi wa taifa kwa kuheshimu utawala wa sheria na kujiepusha na matendo yote yanayoweza kuitumbukiza nchi katika machafuko.

“Leo ni siku ya watawala wa Tanzania kutubu, tumeanza kuona misingi ya amani ya nchi yetu ikitikiswa, amani iliyojengwa kwa gharama kubwa na waasisi wetu; tumeanza kuona nchi hii ni ya chama kimoja, na huu ni uovu”, amesema Askofu Kakobe.

Amesema misingi ya demokrasia ni pamoja na kuruhusu wananchi kutoa maoni yanayolenga kuboresha mstakabali wa maisha yao.

Pia viongozi wanapaswa kukubali lawama na mawazo tofauti na kuiga mfano wa  Yesu  Kristo ambaye alistahimili matukano na maudhi kutoka kwa  watu ambao walikuwa hawaikubali huduma yake akiwa duniani.

“Mungu  ana nguvu kuliko majeshi yote ya nchi, lakini anatukanwa na bado hatumii majeshi yake, hata wewe unaweza ukawa mvumilivu”, amesema.

Ameongeza kuwa nchi ya Tanzania iko kwenye mfumo wa vyama vingi ambao unaruhusu vyama vyote kufanya shughuli zao bila kuingiliwa na mamlaka husika na kuwataka watawala kuheshimu sheria zilizopo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutokuruhusu migogoro ya kisiasa inayoweza kuvuruga amani ya nchi.

“Mungu mwenyewe anaheshimu sheria basi kama na sisi tumeweka sheria tunapaswa kuheshimu sheria tulizo jiwekea wenyewe”, amesema

Askofu Kakobe aliwaasa watawala kutoirudisha nchi kwenye mfumo wa chama kimoja unaopingana na misingi ya kujieleza kwa uwazi.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo akihubiri wakati wa mkesha wa Krismasi katika Parokia ya Mtakatifu Maurus iliyopo Kurasini amesema ili kudumisha misingi ya amani, wananchi wafanye kazi kwa bidii na kujiletea maendeleo.

“Wakati umefika watu kufanya kazi usiku na mchana, hilo likifanyika nchi itaendelea kuwa na amani. Muda wote uwe wa kufanya kazi, tupumzike kidogo kwa ajili ya kupata usingizi”, amesema Askofu Pengo.

Amebainisha kuwa amani ya nchi haijengwi na viongozi waliopo madarakani bali na wananchi wenyewe kwa kufanya kazi na kuachana na uvivu na malalamiko.

Pia amewataka wananchi kuwaombea viongozi ili waongoze kwa hofu ya Mungu na kulifikisha taifa kwenye kilele cha maendeleo yaliyokusudiwa.

Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar Mhashamu Augustino Shao amesema ipo haja kwa serikali na vyama vya siasa kuelewa dhana ya demokrasia kutokana na mchango wake katika maendeleo ya taifa.
 pichani ni Askofu Mkuu Jimbo katoliki zanzibar,mhashamu Augustino Shao

“Kwa kiasi kikubwa vyama hivi vimeleta mwanga na uwazi serikalini,chaguzi ndogo za madiwani huko bara ni ishara tosha kwamba hatujafahamu maana ya demokrasia yaani kutofautiana lakini bado kubaki wamoja”, amesema Askofu Shao.

Sherehe ya Krismasi

Krismas ni sherehe ambayo huwaunganisha wakristo wote duniani kuazimisha siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo mwokozi wa ulimwengu ambayo hufanyika Disemba 25 kila mwaka.
  
Siku hii imekuwa ikiwakutanisha wakristo mbalimbali katika nyumba za ibada na kutafakari maisha yao ya kiroho.

Lakini viongozi wa dini wanaitumia kutoa matamko mbalimbali yanayolenga kuishauri na kuionya jamii juu ya mwenendo usiofaa.

Misa ya kitaifa ilifanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Minara Miwili lilipo Zanzibar ambapo wakristo na viongozi mbalimbali wa serikali walijumuika pamoja katika kumbukumbu hiyo muhimu duniani.

Jumamosi, 23 Desemba 2017

UKOSEFU WA ELIMU YA MATUNZO UNAVYOCHOCHEA KANSA YA NGOZI KWA 'ALBINO'



“Nina ndoto kwamba siku moja nchini Tanzania, watu wenye albinism watachukua nafasi yao inayostahili katika ngazi za jamii.
 "Na kwamba siku  za ubaguzi dhidi ya watu wenye ‘albinism’  zitakuwa kumbukumbuiliyofifia.”

Hii ni nukuu ya muasisi wa shirika la Under The Same Sun, Peter Ash aliyoitoa mwaka 2009 kutambua umuhimu wa watu wenye ulemavu wa ngozi katika jamii.

Ulemavu wa ngozi (Albinism) ni hali isiyoambukiza inayotokana na vinasaba vya
kurithi na hutokea dunia nzima.


 Ili mtoto azaliwe akiwa na ulemavu wa ngozi ni lazima baba na mama wawe na vinasaba hivyo  na matokeo yake ni  ukosefu wa rangi kwenye nywele, ngozi na macho ambao vile vile unasababisha uoni hafifu na kudhurika kwa urahisi na mionzi ya jua na mwanga mkali.

Mtu mwenye albino huwa na urithi kutoka kwa wazazi wake ikiwa watakuwa na jeni zenye tabia bainishi za albino kabla ya kuzaliwa mtoto mwenye albino.

Wazazi wanapokuwa na tabia bainishi za albino kuna uwezekano wa asilimia 25 ya kila ujauzito kuwa mtoto atazaliwa na albino. Albino wanazaliwa na ngozi nyeupe na matatizo ya uoni wa macho.
  
Watafiti wa afya wanasema kuna aina nyingi za ulemavu wa ngozi lakini ulemavu unaoathiri ngozi, macho na nywele unajulikana kama ‘Oculocutaneous Albinism (OCA)’ na aina ulemavu unaojitokeza sana katika nchi ya Tanzania.

 Pia zipo aina nyingine za ulemavu wa ngozi (OCA) ambazo ni OCA2, OCA3 na OCA4 baadhi ya aina hizi zimegawanyika katika aina nyingine ndogo ndogo kutokana na aina ya tofauti ya kiwango cha rangi alichonacho mtu.

Tatizo la ngozi ni changamoto kubwa kwa watu wenye ualbino  kwa sababu ngozi zao ni tofauti na binadamu wa kawaida hivyo huitaji mafuta ya kuilainisha ngozi na kupaka mafuta ya kujikinga na mionzi ya jua.

Gharama ya mafuta haya ya kujikinga ni ghali kulinganisha na hali ya kimaisha waliyonayo Albino wengi Tanzania, huuzwa kati ya sh. 40,000 na 50,000 bei ambayo wengi hushindwa kumudu na hivyo kuendelea kuteseka na kutengwa na jamii.

Juhudi zimefanyika na mashirika yasiyo ya kiserikali kuagiza mafuta hayo kwa wingi kutoka nchi za nje lakini yakifika bandarini hutozwa kodi kubwa ambayo inazidi gharama ya kununulia bidhaa hiyo.

 Mafuta hayo huzuiliwa mda mrefu bandarini na wakati mwingine huaribika kwa sababu ya kuisha kwa mda wa matumizi.  

Kutokana na changamoto hizo za usafirishaji, hospitali ya KCMC Moshi iliamua kujitolea kutengeneza mafuta hayo hapa nchini ili kurahisisha upatikanaji wake.

Changamoto inabaki katika usambazaji, mafuta ya kulainisha ngozi huzalishwa kwa wingi lakini usambazaji wake hauridhishi kwa kuwa mafuta haya hayawafikii watu wenye ulemavu wa ngozi walio pembezoni mwa nchi.

Pia ukosefu wa elimu miongoni mwa watu kuhusiana na jinsi ya kuwatunza Albino imekuwa sababu ya kuendeleza tatizo la ngozi kwa watu wenye ualbino. 

Kukosekana kwa umakini kumewafanya kuwa katika hatari ya kupatwa na saratani ya ngozi na kupoteza maisha yao.

Taarifa za shirika la Under the Sum Sun zinaonyesha zaidi ya asilimia 90 ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania hufariki dunia wakiwa na umri wa miaka 30 kutokana na maradhi ya saratani ya ngozi yanayosababishwa na kutojikinga dhidi ya mionzi mikali ya jua.

Serikali kupitia mamlaka zake inashauriwa kutazama afya za watu wenye ulemavu kwa jicho la huruma na kuwasaidia waishi vizuri kama binadamu wengine.
  
Njia pekee ni kulipa nguvu baraza la watu wenye ulemavu wa ngozi ambalo liliundwa mwaka 2007 lakini halijaanza kufanya kazi.

Baraza hilo likikamilika litakuwa chombo muhimu kwa watu hao kupaza sauti zao ikiwemo mstakabali wa afya zao.

Ruzuku inayotolewa kwa vyama vya walemavu kikiwemo chama cha Albino Tanzania haitoshi kutekeleza majukumu  ya msingi ikilinganishwa na mazingira yasiyoridhisha waliyonayo walemavu.

Kila chama cha walemavu hupata ruzuku ya shilingi milioni mbili kila mwaka, fedha hizi ni chache na serikali itafakari suala hili na kutengeneza mpango mkakati wa kuvisaidia vyama vya walemavu.

 Mabadiliko ya sera na sheria ni muhimu katika kuwahakikishia watu wenye ulemavu usala na afya bora.