Jumanne, 16 Desemba 2014

BENKI YA USHIRIKA K’NJARO YACHUNGULIA KABURI

Benki kuu ya Tanzania(BoT) imesitisha baadhi ya huduma za biashara kwa benki ya Ushirika Kilimanjaro(KCBL) kutokona na mtaji wa benki hiyo kuwa chini ya sh, bilioni 2  na hivyo kuwa  katika hatari ya kukosa sifa kwa mujibu wa sheria ya  benki kuu ya mwaka 2006.

Kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi iliyowasilishwa katika mkutano mkuu wa 20 wa wanahisa wa benki hiyo uliofanyika hivi karibuni mjini hapa inaonyesha kuwa,kwa sasa benki hiyo ina mtaji  wa sh,Milioni 195,111,000 tu hali ambayo wakaguzi hao wameonya kuwa inaweza kuathiri uwepo wa benki hiyo.

Aidha taarifa hiyo imeonya kuwa,mikopo inayotolewa kwa wateja imekuwa hairejeshwi kila  mwezi kwa  mujibu wa mikataba iliyowekwa hali iliyopelekea kufutwa kwa mikopo mibaya yenye thamani ya sh,Milioni 255,611,441 kwenye vitabu baada ya kupata kibali kutoka bodi ya uongozi.

Wakati kiasi hicho kikubwa cha fedha kikufutwa,benki hiyo ilifanikiwa kukusanya kiasi kidogo cha fedha cha sh,Milioni 62.073,000 huku taarifa hiyo ya ukaguzi ikigundua kuwapo kwa tengo la ziada la mikopo mibaya la sh,33,740,683 likipitishwa kwenye vitabu.       

Taarifa hiyo ya ukaguzi imeendelea kufichua kuwa,kuongezeka kwa matumizi yasiyo na riba kunachangia benki kutokuendelea vizuri na kusababisha hasara ya sh,milioni 343,260,000 katika mwaka husika na kuongeza jumla ya  hasara kutoka sh,Bilioni  1.169,834,000  mwaka 2012    hadi sh,Bilioni 1.513,094,000 mwaka jana.

Hata hivyo menejimenti ya benki hiyo imejibu hoja hizo za ukaguzi na kuelezea kuwa itaongeza biashara kwa sh,Bilioni 1.5 ambayo itazalisha mapato ya sh,Milioni 150 ili kuongeza faida bila kuonyesha mchanganuo jinsi itakavyoongeza biashara hiyo.

Katika hatua nyingine,benki hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha inarejesha mabilioni ya shilingi yaliyotolewa na benki hiyo kwa wateja mbalimbali kama mikopo kutokana na kuwapo na mwitikio mdogo katika ujereshaji wake.              
Taarifa ya meneja wa benki hiyo,Elizabert Makwabe kwa mkutano mkuu wa wanahisa hao imeeleza kuwa,hadi kufikia septemba 30 mwaka huu jumla ya sh,Bilioni 4.333,036,114 zilikuwa zimetolewa kama mikopo kwa wateja mbalimbali.

Inaeleza kuwa aslimia 63.3 ya mikopo hiyo ilielekezwa katika sekta ya kilimo ambayo ni kiasi cha sh,Bilioni 2.758,217,111 na kwamba ni sh,Milioni 370,258,855 tu zilizokuwa zimekusanywa katika kipindi cha kuanzia januari hadi septemba mwaka huu.

Meneja huyo amelalamika kuwa,baadhi ya wateja wanatumia njia mbalimbali ili wachelewe kulipa na wakati mwingine wanatumia kauli za matusi pale inapolazimika madeni  yasiyolipwa yakusanywe.

Alitoa wito kwa wale wote ambao hawajarejesha au marejesho yao hayaendi vizuri,kuchukua hatua za makusudi na kulipa madeni yao na kwamba bila kufanya hivyo benki italazimika kutenga matengo kwa ajili ya madeni mabaya hali itakayoathiri mtaji wa benki hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni