Jumapili, 28 Desemba 2014

KIONGOZI WA AL-SHABAAB AKAMATWA



Kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab nchini Somalia, Zakariyah Ismail Ahmend Hersi, amekamatwa na polisi baada ya kujisalimisha jana Jumamosi.

Afisa mmoja wa idara ya ujasusi amesema Hersi alijisalimisha kwa polisi katika mkoa wa Gedo, baada ya kile kinachoonekana ni uwezekano wa kuzuka mzozo ndani ya kundi hilo.

Huenda Hersi anatofautiana na wapiganaji watiifu kwa kiongozi wa Al-Shabaab, hayati Abdi Godane, aliyeuawa katika shambulio la anga lililofanywa na Marekani mwanzoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, afisa wa kijeshi wa ukanda huo, Jama Muse, amesema Hersi alikuwa anasimamia masuala ya kijasusi na fedha na pia alikuwa ni mmoja kati ya makamanda waandamizi wa Al-Shabaab.

Ingawa jeshi la Somalia lilimuweka katika orodha ya mawakala wa Al-Shabaab, haijafahamika wazi iwapo Hersi bado alikuwa ana nguvu ndani ya kundi hilo la kigaidi katika miezi michache iliyopita. Inawezekana kuwa Hersi alikuwa miongoni mwa kundi la makamanda waliotofautiana na Godane kabla ya kifo chake.

CHANZO: DW

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni