Ijumaa, 12 Desemba 2014

MWANAFUNZI WA KIDATO CHA KWANZA MAJENGO SECONDARY ATOWEKA KUSIKOJULIKANA



M
wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari majengo,Said Seleman (14) mkazi wa mtaa wa Arabika kata ya Majengo Manispaa ya Moshi, ametoweka nyumbani kwao kwa zaidi ya miezi miwili sasa huku familia yake ikipoteza matumaini ya kumpata kutokana na kutoonekana kila kona wanayomsaka.

Kwa mujibu wa mama mzazi wa mwanafunzi huyo,salama saidi,kijana huyo alitoroka nyumbani kwao Oktoba nane mwaka huu wakati mama yake akijiandaa kwenda na mwanafunzi huyo shuleni kwao kutokana na kutuhumiwa kutenda utovu wa nidhamu.

Akizungumza na blog hii, mama huyo alisema tangu siku hiyo wamekuwa katika harakati za kumtafuta mwanaye bila kafanikio na kuomba watu wenye mapenzi mema ambao watafanikiwa kumuona mwanaye watoe taarifa kituo chochote cha polisi au wampige simu yake ya kiganjani namba 0754 03 63 12.

Kwa mujibu wa mama mzazi wa mwanafunzi huyo, mwanaye alikuwa akituhumiwa kujihusisha na wizi wa mabegi ya wanafunzi wenzake na kwenda kuyauza na kisha kugawana fedha na wanafunzi wenzake na baada ya arobaini yake kufika siri ikafichuka na kubanwa ili ataje washirika wake.

Pia alisema, sakata hili lilifikishwa nyumbani kwao na mama huyo akashauri likazungumzwe kwa uwazi shuleni na ndipo kijana huyo alioingiwa na hofu na kisha kutimka kutokana na kuonywa na wenzake kuwa akikamatwa ni marufuku kuwataja washirika wake.

Tayari mama huyo ametoa taarifa za kupotelewa na mwanaye katika kituo cha polisi majengo ambako jarada limefunguliwa na kupewa namba MAJ/RB/3513/2014.

Hima hima wananchi kwa atakayemuona mwanafunzi huyo atoe taarifa zitakazosaidi kupatikana kwake kwani kwa kitendo chake cha kutoroka nyumbani amekosa fursa ya kufanya mtihani wa kidato cha kwanza na hivyo kuwa katika hatari ya kukosa nafasi ya kusonga mbele  kwa kidato cha pili

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni