Ijumaa, 12 Desemba 2014

MOTO WATEKETEZA MADUKA 6, BASI LA ABIRIA; MOSHI



Mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 zimeteketea kwa moto yakiwemo maduka sita na basi dogo la abiria lililokuwa gereji kwa ajili ya matengenezo katika tukio lililotokea mjini Moshi hapa mkoani Kilimanjaro.

Mashuhuda wa tukio hilo lililotokea katika mtaa wa Bakwata-Sido katika Manispaa ya Moshi walisema moto ulianza majira ya saa 6:30 usiku wa kuamkia leo, ukianzia katika kibanda cha kuchaji betri za magari.

“Kuna kibanda cha kuchaji betri za magari katika gereji ya vijana ambako betri zilikuwa zikichajiwa humo ambako shoti ya umeme ilitokea na kulikuwa na oil zilizokuwa zimetapakaa chini hivyo cheche za moto ziliruka na kusababisha mlipuko huu,” alisema shuhuda mmoja.

Mmiliki wa mojawapo ya maduka aliyetambulisha kwa jina la Justo Elias Mboho alisema taarifa za kulipuka kwa maduka katika mtaa ulio na shughuli nyingi za ufundi magari na uuzaji wa mitungi ya gesi alizipata usiku na kwamba kila kitu kimeteketea kwa moto.

“Sikuwa na jinsi nilipoambiwa kwamba mali zote zimeteketea kwa moto hivyo nikaona hakuna haja ya usiku huo kuja katika eneo la tukio hadi asubuhi ambako kila kitu kimeteketea… mali zenye thamani ya shilingi milioni 5 katika duka langu zimeteketea zote,” alisema Mboho.

Aidha mmiliki mwingine aliyejifahamika kwa jina la Living Mrema alisema duka lake lilikuwa na vifaa vyenye thamani ya  shilingi milioni 20 viliteketea kwa moto na kuongeza kwamba kwa ujumla wa maduka yote sita zaidi ya shilingi milioni 90 zimeteketea kwa moto.

Katika tukio hilo mashuhuda waliongeza kusema gari la zimamoto la Manispaa ya Moshi liliishiwa maji hivyo kuomba msaada wa zimamoto ya Kiwanda cha Sukari (TPC) ambao walifika na kuambulia kuzima moto tu kutokana na umbali hadi eneo la tukio.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Korongoni, Said Mwamba alilitupia lawama Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, kikosi cha Zimamoto-Kilimanjaro na Manispaa ya Moshi kutokana na uzembe wa matukio kadhaa ya moto.

“Niliamshwa usiku na vijana kwamba moto unawake katika mtaa wa Bakwata-Sido, nikapiga simu jeshi la polisi simu zilikuwa zikiita bila kupokelewa na nyingine kuzimwa kinyume na maadili ya kazi yenyewe, zimamoto nao waliishiwa maji huku Manispaa nilishawaambia mapema kwamba uuzwaji wa gesi katika eneo hili ambalo ni makazi ya watu ni hatari,” alisema Diwani Mwamba

Diwani huyo aliongeza kuwa chanzo ni mrundikano  wa vifaa vya gereji ya karibu (Vijana Garage) bila kufanyiwa usafi na kuwekwa kwa utaratibu  hali ambayo ingeweza kuleta maafa zaidi katika eneo hilo.

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
CHANZO: JAIZMELALEO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni