Jumamosi, 16 Desemba 2017

"MAFURIKO" SHULENI YANAVYOKWAMISHA WANAFUNZI KUELIMIKA



Wananchi wakielemishwa wakaelimika ni faida kwa taifa. Kuelimika kunategemea  ubora wa elimu inayotolewa ambayo hupimwa kwa vigezo mbalimbali, ikiwemo ujuzi na maarifa wanayopata wanafunzi wakiwa shuleni kusaida kutatua changamoto zilizopo katika jamii. 

Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wa elimu imefanya juhudi mbalimbali za kuwaelimisha watoto ikiwemo kupunguza gharama za masomo na kuamua kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari. hali hiyo imechochea ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa kila mwaka.  

Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la elimu (UNESCO) zinaonyesha hadi kufikia mwaka 2015 uandikishaji wanafunzi katika shule za msingi umefikia asilimia 91 katika nchi zinazoendelea zikiwemo zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

 Takwimu hizi zinadhihirisha kuwa juhudi mbalimbali zinafanyika kuwapeleka watoto shule.

Changamoto iliyopo ni uandikishaji hauendani na uboreshaji wa miundombinu ya shule, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ambapo shule nyingi za serikali zina idadi kubwa ya wanafunzi ikilinganishwa na idadi ya walimu na madarasa yaliyopo. 

Mathalani shule ya msingi Gamondo A iliyopo Wilaya ya Bariadi ina wanafunzi 2,334 akiwa na vyumba 9 vya madarasa ambapo ina upungufu wa vyumba 43 ili kukidhi mahitaji yote.

 Kwa wastani darasa moja lina zaidi ya wanafunzi 150.
Kulingana na uwiano uliowekwa na Wizara ya Nchi Ofisi ya Raid Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)  darasa 1 kwa wanafunzi 40 (1:40).

Muongozo  huo wa TAMISEMI bado haujatekelezwa kikamilifu katika maeneo mbalimbali ya nchi likiwemo jiji la Dar es Salaam ambalo idadi ya wakazi inaongezeka kwa kasi na kuleta changamoto katika mipango ya Halmashauri kujenga shule.

Mkoa wa Dar es salaam pekee una jumla ya shule za msingi 663 kati ya hizo 377 za serikali na 286 zisizo za serikali. Pia una jumla ya shule za sekondari 324 ambapo za Serikali 138 na 186 zisizo za serikali. 

Idadi ya shule za sekondari ni mara mbili ya shule za msingi, jambo huzidisha msongamano wa wanafunzi katika shule hizo.

Kwa mazingira ya kawaida ufanisi wa ufundishaji utakuwa chini na wanafunzi hawawezi kupata matokeo mazuri katika masomo yao, kwa sababu walimu hawawezi kuwafikia wanafunzi wote kwa wakati na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata maarifa sahihi.  
Licha ya upungufu wa madarasa, shule nyingi za Dar as Salaam zimejengwa pembezoni, ambapo wanafunzi hutumia zaidi ya saa moja kuzifikia shule hizo.

Abuu Juma, mwanafunzi wa shule ya sekondari Kambangwa iliyopo Wilaya Kinondoni anasema anaishi Bunju B na hulazimika kuifuata shule hiyo ambayo iko umbali wa kilomita 29 toka nyumbani.

Huamka mapema ili kukabiliana na foleni lakini akifika shuleni anakuwa amechoka na uwezo wa kufuatilia masomo hupungua.

Mikakati ya serikali kutatua changamoto za elimu

Kwa kuliona hilo serikali  kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi,  Profesa,  Joyce  Ndalichako wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2017/2018 aliahidi kuinua kiwango cha elimu .

 “Wizara yangu imeendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika kuratibu uboreshaji wa miundombinu kwenye Shule za Msingi na Sekondari",

 "Wizara yangu imeratibu ujenzi wa miundombinu katika Shule 274 (Msingi 142 na Sekondari 132) katika Halmashauri 119 ambapo ujenzi wa jumla ya Madarasa 1,081, Vyoo 2,802, Mabweni 200, Mabwalo 9 Majengo ya Utawala 6, na nyumba za walimu 11 pamoja na uchimbaji wa visima vya maji katika Shule 4 umefanyika.

“Ujenzi huu ulitumia njia ya Force Account kupitia Kamati za Shule ambayo imesaidia kupunguza gharama za ujenzi na kuongeza 17 ufanisi katika ukamilishaji wa ujenzi” 

Serikali ilitazame suala la ubora wa elimu na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu kwa sababu imesaini mikataba ya kimataifa katika sekta ya elimu ikiwemo Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ya 2030 ambapo nchi wahisani zinatakiwa kutekeleza lengo la 4 la kuweka mazingira mazuri yatakayosaidia wanafunzi wa kike na wa kiume kupata elimu bora inayolenga kuwajengea uwezo wa kujitegemea na  kujiajiri katika shughuli mbalimbali za ufundi na ujasiriamali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni