Alhamisi, 14 Desemba 2017

URAFI WA MADARAKA: RAIS WA BURUNDI AZINDUA KAMPENI YA KUBAKI MADARAKANI HADI 2034



Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza(pichani na mkewe) amezindua kampeni ya kufanyika kwa kura ya maamuzi ambayo inatazamwa na jaribio la kutaka kusalia madarakani hadi 2034.

Shirika la habari la AFP linasema mpango huo unahusisha kuidhinishwa kwa rasimu ya katiba ambayo itamuwezesha kuwania urais kwa mihula miwili zaidi ya miaka saba kila muhula.

Muhula wa sasa wa Bw Nkurunziza unafikia kikomo 2020.

Rais huyo aliwaambia wafuasi wake Jumanne wiki hii  katika kijiji cha Gitega kwamba wale wanaopinga juhudi zake "kwa maneno au kwa vitendo" watakuwa wameuvuka "mstari mwekundu".

Kampeni hiyo imeanzishwa baada ya serikali kuzindua juhudi za kuchangisha fedha za maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Shirika la habari la AFP linasema mchango huo, ambao serikali inasema ni wa hiari, umeshutumiwa na makundi ya kutetea haki za kibinadamu ambayo yamesema ni kama "wizi kwa mpango".

Viongozi wa upinzani walio uhamishoni wanasema kura hiyo ya maoni itakuwa kama "mazishi" kwa mwafaka wa amani uliotiwa saini mwaka 2000 nchini humo.

Mkataba huo wa amani ulisaidia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 13 na kusababisha vifo vya watu 300,000.

Burundi ilitumbukia kwenye mzozo mwingine wa kisiasa mwaka 2015 wakati Rais Nkurunziza alipokataa kung'atuka baada ya kumaliza muhula wake na akaamua kuwania tena urais.
 
Mwaka huo pia kulitekelezwa jaribio la kuipindua serikali ya Bw Nkurunziza ambalo halikufanikiwa.

Mzozo huo ulisababisha mashambulio ya mara kwa mara ambayo yamechangia vifo vya watu karibu 2,000 na wengine maelfu kutoroka makwao na kukimbilia nchi jirani ikiwamo Tanzania.

Mazungumzo ambayo yamekuwa yakiendelea kati ya serikali na makundi ya upinzani yalisambaratika wiki iliyopita.

Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa  Tanzania ,Benjamin Mkapa aliyekuwa anafanikisha mazungumzo hayo alisema hakukuwa na "makubaliano yoyote, maazimio yoyote au stakabadhi yoyote ya kuwafungamanisha wadau".
     
FAHAMU KUHUSU JAMHURI YA BURUNDI

     Milioni 10.4 Idadi ya watu nchini Burundi - sawa na Ubelgiji

Kilomita mraba 27,816 Ukubwa wa nchi ya Burundi - sawa na Haiti

Miaka 50 Muda wa kuishi kwa wanaume

Miaka 50 Muda wa kuishi kwa wanawake

$900 GDP - sawa na Liberia 

Chanzo:BBC Swahili.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni