Jumamosi, 30 Desemba 2017

UJENZI WA NYUMBA SASA KWA KIBALI,WATAKAOPUUZA KUKIONA



Na Kija Elias, Hai.

Baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, limepitisha sheria ndogo ndogo zikiwemo sheria za vibali vya ujenzi vinayomtaka kila mwananchi ambaye anataka kujenga lazima awe na kibali cha ujenzi huo. 

Sheria hiyo imepitishwa jana, kufuatia agizo lililotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambalo alilitoa hivi karibuni la kuwataka viongozi wa Halmashauri za wilaya,miji Majiji nchini, kuharakisha utoaji wa vibali vya ujenzi na kuachana na urasimu ambao ulikuwa ukisababisha kuwepo kwa ujenzi holela. 

Akisoma sheria hizo kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Afisa Ardhi wa wilaya hiyo Jacob Muhumba, alisema kuwa mtu yeyote atakaye jenga bila kuwa na kibali cha ujenzi sheria hiyo imeweka adhabu kali ikiwa ni pamoja na kusitisha ujenzi wake na kufikishwa katika vyombo vya dola. 

“Sheria hii inamtaka kila mtu anayetaka kujenga ni lazima awe na kibali cha ujenzi, hatutamruhusu mtu kujenga bila kuwa na kibali, na kila mtu atakayekuwa anaomba kibali cha ujenzi atalazimika kulipia gharama  kwa ajili ya kupata kibali hicho,”alisema Muhumba. 

“Tulikuwa hatuna sheria ya vibali vya ujenzi tangu zamani, lakini pia tulikuwa hatutozi gharama yeyote ile, hivyo mwananchi alikuwa akijijengea tu bila kufuata utaratibu hali ambayo imechangia kuwepo kwa makazi holela,”alisema. 

Aidha alifafanua kuwa gharama hizo za kupata kibali cha ujenzi kitategemea na kile mtu anachotaka kujenga , ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi, maghala, viwanja vya ndege na majengo ya biashara . 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Helgha Mchomvu alisema kuwa baraza hilo limelazimika kuipitisha  sheria hiyo ili kuepusha ujenzi holela ambao umekuwa ukifanyika na hivyo kuufanya mji wa Bomang’omba kutokuwa katika mpangilio mzuri. 

Katika hatua nyingine halmashauri hiyo ya wilaya ya Hai,imeshindwa kufikia lengo la kukusanya mapato ya shilingi Bilioni 2.5 kutokana na baadhi ya vyanzo vya mapato vya halmashauri hiyo kuchukuliwa na serikali Kuu.
  

“Ukusanyaji wa mapato umeshuka kutoka bilioni 2.5 hadi kufikia bilioni 2.1 hii imechangiwa na serikali kuu kuchukua vyanzo vyetu ambavyo tulikuwa tukikusanya, hivyo kupitishwa kwa sheria ya kuwa na kibali cha ujenzi itasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato,”alisema mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Wakizungumzia hatua ya kuwepo na sheria ya vibali katika ujenzi wa nyumba baadhi ya wakazi wa  mji wa Boma ng’ombe, kuhusu  wamesema kuwa itasaidia sana kwani kumekuwepo na ujenzi holela ambao unachangia kuharibu mandhari ya mji huo.

Gidion Lucas na Issaya Fabiani, walisema kumekuwepo na ucheleweshaji mkubwa wa kupata vibali vya ujenzi unaosababishwa na wahusika wenyewe na hivyo kuchangia wananchi kujenga kiholela bila kufuata utaratibu, kutokana na kuchoka kusubiri  kwa muda mrefu ili waweze kupata vibali vya ujenzi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni