Ijumaa, 1 Desemba 2017

MASOKO YATAJWA UNYANYASAJI KIJINSIA WANAWAKE JIJINI MWANZA



Na Sitta Tumma, Mwanza

IMEELEZWA kwamba asilimia 88.9 ya lugha inayotumiwa kwenye mikusanyiko ya watu, katika maeneo ya masoko jijini Mwanza ni matusi na ukatili dhidi ya wanawake.

Hali hiyo inatokana na jamii kuendekeza ukatili wa kijinsia, jambo linalotakiwa kukomeshwa kwa wahusika wa vitendo hivyo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa Mradi wa Shirika la EfG, Ikupa Mwakisu, katika hitimisho la kampeni ya kuzuia ukatili kwa wanawake masokoni, iliyofanyika Soko la Kirumba Manispaa ya Ilemela jijini hapa.

Shirika hilo la kirai limekuwa likitekeleza kampeni yake ya kuzuia ukatili kwa wanawake, kwenye masoko ya Mkuyuni, Mlango Mmoja, Igogo, Soko Kuu Wilaya ya Nyamagana, Kirumba na Soko la Kimataifa la Mwaloni, katika Wilaya ya Ilemela.

Kwa mujibu wa Ikupa, ukatili dhidi ya wanawake umekuwa ukirudisha nyuma jitihada za maendeleo kwa jamii husika, hivyo ni vema ukakomehwa.

"Mwaka 2014-2015 Shirika la EfG lilifanya utafiti kwenye masoko jijini Mwanza. Utafiti huu ulilenga kutambua changamoto na mazingira ya wanawake wafanyabiashara ngazi ya wilaya na mkoa.

"Utafiti ulibaini mambo mengi yakiwamo ya kisheria na ukatili wa kijinsia. Kwenye masoko ukatili wa lugha chafu unaongoza kwa asilimia 88.9," alisema Ikupa.

Alitoa wito kwa viongozi wa ngazi zote wakiwamo wa kisiasa na jamii kwa ujumla, kuchukuwa hatua za kisheria kwa watu wanaoendekeza ukatili juu ya wanawake.

Alisema Shirika la EfG limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kupunguza tatizo hilo katika eneo la mradi jijini Mwanza, ingawa elimu zaidi bado inahitajika kwa jamii.

"Tunapambana kuondoa vikwazo vya kiuchumi kwa wanawake masokoni, vinavyotokana na ukatili wa lugha na vinginevyo.

"Tumejikita kutoa elimu kwa viongozi masokoni na jamii. Tunawajengea uwezo wa kuchukuwa hatua na kutoa ushahidi mahakamani kuhusu kesi za ukatili kwa wanawake," aliongeza Ikupa.

Baadhi ya wanawake wanaofanyakazi kwenye masoko hayo sita yanayosimamiwa na EfG walisema, hivi sasa vitendo vya ukatili vimepungua ikilinganishwa na awali.

"Zamani ukiingia sokoni wanaume wanashika shika makalio ya wanawake. Unasikia mwanamke anatukanwa matusi ya nguoni bila kujali.

"Lakini kwa sasa tumeshaelimishwa na hawa EfG, akinishika tu matiti au makalio ndani. Siku hizi ushenzi huo haupo tena," alisema Eliza Marwa, kutoka Soko la Kirumba.

Diwani wa Kata ya Kirumba, Alex Ngusa, maarufu kwa jina la 'The Home Boy' aliitaka jamii yote kuacha vitendo vya kikatili kwa wanawake na watoto, ili kukwepa mkono wa heria.

Kwa mujibu wa Diwani Ngusa, lugha chafu, vipigo na masengenyo kwa wanajamii hayafai, bali kuheshimu utu wa mtu ni muhimu zaidi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni