Jumatatu, 18 Desemba 2017

MTUKUFU AGA KHAN ANAVYOLETA NEEMA KWA WATANZANIA



Na Sitta Tumma, Mwanza

"TUNAMPONGEZA sana Mtukufu Prince Karim Aga Khan na taasisi zake zote, kwa namna anavyowekeza miradi mbalimbali ya maendeleo Tanzania.

"Kiongozi huyu kwanza ni mcha Mungu, anapenda kuona jamii inapata maendeleo, amani na upendo kwa watu wote."

Hii ni kauli ya Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani, ambaye pia ni 
Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Mkoa wa Mwanza, Askofu Charles Sekelwa, aliyoitoa mbele ya ujumbe wa kamati hiyo.

Kamati hiyo ya Amani, hivi karibuni ilitembelea makumbusho ya Mtukufu Prince Aga Khan, yaliyopo jijini Mwanza, ikiwa ni maadhimisho ya kusherehekea miaka 60 ya uongozi wake.

Maadhimisho hayo ya miaka 60 ya Uimamu wa Aga Khan, yanakuja huku kiongozi huyo akiendelea kusifika duniani, kutokana na dhamira yake ya kuiwezesha jamii kuwa na maisha bora! Ndiyo.

Katika ziara hiyo ya Wajumbe wa Kamati ya Amani, walijionea historia ya kiongozi huyo wa kiroho wa Madhehebu ya Kiislamu ya Shia Ismailia.

Pamoja na mambo mengine, viongozi wa kamati hiyo walieleza kufurahishwa na uongozi wa kiongozi wa Aga Khan duniani.

Wenyeviti wa Kamati hiyo, Sheikh Hassan Kabeke na mwenzake, Askofu Charles Sekelwa, wanasema taasisi hiyo inayosimamia dhehebu la Ismailia inastahili kuigwa na jamii yote ulimwenguni.

"Kwanza ziara yetu kwenye makumbusho haya imetupa elimu kubwa.

"Tumejifunza namna ya kuwa kiongozi bora kwa waumini na kushiriki kwenye maendeleo.

"Mafanikio ya Mtukufu Aga Khan yanatokana na uongozi wake kupenda watu, amani na maendeleo ya nchi na mataifa," anasema Sheikh Kabeke.

Viongozi hao wanasema uongozi wa Aga Khan umetamalaki katika nyanja ya amani, upendo na maendeleo kwa jamii.

Viongozi hao wanasema kuwa, taasisi na viongozi wote wa madhehebu ya dini hawana budi kuiga uongozi na uwekezaji miradi ya maendeleo, unaofanywa na Aga Khan kwa jamii ulimwenguni.

Naye Katibu wa Baraza la Waislamu Mkoa wa Mwanza ( Bakwata), Sheikh 
Mohamed Balla, alisisitiza pia suala la amani na uwekezaji wa miradi ya kisekta Tanzania.

"Tumeona Mtukufu Aga Khan anavyosaidia kuleta maendeleo katika nchi yetu. Jamii yote inapaswa kuiga mfano mwema wa kiongozi huyo.

"Tunafurahi huyu kiongozi anavyohimiza na kupenda amani duniani. 

Amani ni kitu muhimu sana, tuilinde kwa gharama zote," anasema Halima Jarufu, Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza.
              
                    AGA KHAN NI NANI?
 Rais John Magufuli akimpokea Imamu wa waislamu wa Shia Ismailia Duniani,Mtukufu Aga Khan Ikulu Jijini Dar es salaam  hivi karibuni,mtukufu Aga Khan alikuwa nchini kwa ziara  ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais Magufuli.

Mtukufu Prince Aga Khan, alianza kuwa Imamu wa Madhehebu ya Kiislamu ya Shia Ismailia, Julai 11,1957, akiwa kijana mwenye umri wa miaka 20.

Alichukuwa nafasi hiyo kubwa kiimani kutoka kwa babu yake, Sir Sultan Mohamed Shah Aga Khan.

Aga Khan ni kiongozi nayesifika duniani kote, kutokana na huduma zake anazozitoa kwa jamii ya kimataifa!

Ni Imamu wa 49 wa Madhehebu hayo ya Kiislamu ya Shia Ismailia.
Inaelezwa ana nasaba ya moja kwa moja na Mtume Muhammad.

Tangu ashike nafasi ya Uimamu mwaka 1957, Prince Karim Aga Khan, amejielekeza katika ustawi wa Jumuiya ya Ismailia, Jumuiya ya Kiislamu kwa upana wake, pamoja na jamii yote kwa ujumla.

Kiongozi huyu anasisitiza mtazamo wa Kiislamu ni kama fikra, imani ya kiroho inayofundisha huruma, uvumilivu na kutetea utu wa mtu.

Katika kizazi cha hivi karibuni, familia ya Aga Khan imekuwa ikishiriki kutoa huduma za kijamii katika nyanja mbalimbali za kimataifa.

Mfano, babu yake Aga Khan amewahi kuwa Rais wa League of Nations.
Baba yake na Prince Aly Khan, amehudumu nafasi ya Balozi wa Pakistan, katika Umoja wa Mataifa (UN).

Vivyo hivyo baba yake mdogo, marehemu Prince Sadruddin Aga Khan, alikuwa Mratibu wa Shirika la UN linaloshughulikia Wakimbizi.

Alikuwa akisaidia Afghanistan na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, katika mipaka ya nchi za Iraq na Uturuki.

Aidha, amekuwa akifanya kazi na Serikali tofauti kila moja ikiwa na matarajio yake.

Mtukufu Aga Khan amekuwa akilinda, kutunza na kuzingatia siasa zisizoegemea upande wowote.

Amekuwa akiwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, ikiwamo sekta ya afya, elimu na masuala ya amani.

Maadhimisho hayo ya miaka 60 ya Mtukufu Aga Khan yanasherehekewa kwa muda wa mwaka mmoja, kuanzia Julai 11,2017 hadi Julai 11 mwakani.

Kwamba, kiongozi huyo anatarajiwa kuzuru nchi 35 duniani, kisha kufungua na kuweka mawe ya msingi ya miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo atakutana na wanajumuiya ya Dini ya Ismailia kwa nchi hizo.

Pamoja na hayo, taasisi hiyo imejikita pia kuwekeza kwenye Sekta ya Elimu, ambapo imejenga shule mbalimbali za msingi na sekondari.

Taasisi hiyo ya Aga Khan inayomiliki shule mbalimbali ikiwamo ya Aga 
Khan Mzizima Sekondari, pia ina walimu 900 Visiwani Zanzibar.

Maimamu wa Wanizari walianza kutumia cheo cha Aga Khan wakati wa karne ya 19 ambako Hasan Ali Shah aliyehesabiwa kama imamu wa 46 wa Kiismaili alipewa cheo hiki na mfalme au shah wa Uajemi.
               
             AGA KHAN

1:   Aga Khan I - Hasan Ali Shah Mehalatee (1800–1881), Imamu wa 46 wa Kiismaili (1817–1881).

2:   Aga Khan II - Ali Shah (~1830–1885), Imamu wa 47 wa Kiismaili (12 Aprili 1881–1885).

3:   Aga Khan III - Prince Sultan Mohammed, (1877–1957), Imamu wa 48 wa Kiismaili (17 Agosti 1885–1957).

4:   Aga Khan IV - Prince Karim Al Husseini (b. 1936),Imamu wa 49 wa Kiismaili (tangu 11 Julai 1957)
                   
              UWEKEZAJI
Katika kusimamia misingi yake, taasisi hiyo ya Maendeleo ya Aga Khan (AKDN) imejikita kusaidia upatikanaji wa maendeleo ya jamii, kwa kuwekeza miradi ya afya na elimu nchini.

Kwamba, imetenga dola za Kicanada milioni 15, kuboresha hospitali za wilaya zilizopo mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mpango huo umelenga kusaidia jamii kupata huduma bora zaidi za kiafya, zikiwamo vipimo.

Taarifa ya Aga Khan inasema kuwa, mbali na taasisi hiyo kuwa mdau mkubwa wa maendeleo duniani kote, inahitaji kuona Watanzania wakiishi salama kiafya, kielimu, upendo na utulivu.

"Tayari tumefungua kituo cha afya Buzuruga Mwanza na Kahama Mkoa wa Shinyanga. Desemba 2017 tutafungua Tabora na Bukoba
"Mwaka 2018 tutafungua pia huduma za afya Bunda Mkoa wa Mara. 

Mwaka 2019 tutafungua Simiyu na Kigoma ," anasema Altaf Hiran Mansoor, Rais wa Aga Khan Kanda ya Ziwa na kuongeza:

"Tayari programu hii ya maboresho ya hospitali za wilaya za Serikali, inashafanyiwa tathmini."
                   
    CHUO KIKUU


Katika kupigania maendeleo, Aga Khan University
inakusudia kujenga Chuo Kikuu cha Afya na Elimu nchini, kitakachokuwa cha pili duniani.

Hivi karibu, Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, ilikaririwa ikisema chuo hicho kitajengwa Arusha-Tanzania.

Chuo cha kwanza dunini kipo nchini Pakistan. Kitagharimu zaidi ya dola za Kimarekani milioni 300, sawa na Sh. Bilioni 660 za Kitanzania.

Taratibu za ujenzi wake zinatarajiwa kuanza miezi sita ijayo kuanzia sasa. Kukamilika kwake kitabadili sura ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Taarifa zinasema kwamba, Chuo Kikuu hicho kitapokea wanafunzi si tu Tanzania, bali kutoka Afrika Mashariki, SADC na duniani kote.

Aga Khan imekuwa ikihudumia maendeleo ya jamii kwa nchi 35 duniani, zioizopo Asia Kusini, Asia ya Kati, Mashariki ya Kati, Ulaya, Amerika Kaskazini na Bara la Afrika.
                   
                     HOSPITAL


Mbali na chuo hicho kikuu, Taasisi hiyo ya Aga Khan pia imenuia kujenga hospitali kubwa kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mansoor anasema hospitali hiyo itakayojengwa Mkoa wa Mwanza, itagharimu dola za Kimarekani milioni  5.5 , sawa na Sh. Bilioni 12 za Kitanzania.

"Hospitali yetu ya Dar es Salaam watu zaidi ya 4,000 wanatibiwa kwa gharama nafuu kila mwaka," anasema Rais wa Taasisi ya Aga Khan Kanda ya Ziwa, Altaf Hiran Mansoor.

Baadhi ya wagonjwa wanaopata huduma katika Hospitali ya Aga Khan jijini Mwanza, wanaeleza kufurahishwa na huduma bora zinazotolewa hopitalini hapo.

"Ukweli Hospitali ya Aga Khan ina huduma nzuri sana, bei zake nafuu na huduma ni bora.

"Mgonjwa unafika unapokelewa vizuri hadi unajisikia raha," anasema Asha Haruna, mkazi wa Mabatini jijini hapa.

Mzee Joshua John (78) yeye anasema: "Familia hata wajukuu zangu nilishaelekeza watibiwe Hospitali za Aga Khan popote watakapokuwa. Huduma zao nzuri sana."

Anasema kuwa, hivi sasa hospitali hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa 160-180 kwa siku moja, tofauti ilivyokuwa Kituo cha Afya.

Awali kikiwa Kituo cha Afya, Aga Khan ilikuwa inapokea takribani wagonjwa 130 kwa siku moja, ambapo kwa sasa kuna ongezeko la wagonjwa hadi 160 kwa siku.



Mtukufu Aga Khan(kulia)akizungumza na Waziri wa Elimu,Profesa Joyce Ndalichako baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam hivi karibuni,Aga Khan alikuwa nchini kwa mwaliko wa Rais John magufuli(picha zote kwa hisani ya Ikulu)







Top of Form
Bottom of Form



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni