Jumanne, 12 Desemba 2017

MMILIKI WA SHULE YA SEKONDARI YA SCOLASTICA AANGUA KILIO KIZIMBANI

Mmiliki wa Shule ya sekondari ya Scolastica iliyopo Himo Mkoani Kilimanjaro,Edward Shayo akipelekwa kizimbani kwa ajili ya kusomewa shitaka la mauji ya mwanafunzi wa shule hiyo,Humphrey Makundi,kesi hiyo imeahirishwa hadi desemba 22 mwaka huu
 Mmiliki wa shule ya sekondari ya Scolastica iliyopo Himo Mkoani Kilimanjaro,Edward Shayo na washitakiwa wenzake,Hamis Chacha na Laban Nabiswa wakiongozwa na polisi kwenda kizimbani tayari kusomewa shitaka la mauaji ya kukusidia ya mwanafunzi wa shule hiyo,Humphrey Makundi,kesi hiyo itatajwa tena desemba 22 mwaka huu

 AANGUA KILIO KIZIMBANI


Na Charles Ndagulla,Moshi

MMILIKI wa shule binafsi ya sekondari ya Scolastica iliyopo katika Mji wa Himo mkoani Kilimanjaro,Edward Shayo jana aliangua kilio mahakamani baada ya kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa shule hiyo inayomkabili yeye na wenzake wawili kupigwa kalenda

Shayo ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo amekuwa haamini kilichotokea kwani tangu  aliposomewa shitaka la mauaji ya kukusidia kwa mara ya kwanza Novemba 27 mwaka huu,amekuwa katika hali ya majonzi huku akitoa raia kwa ndugu zake kumwombea.

Mbali na Shayo,washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ni Hamis Chacha ambaye ni mlinzi wa shule hiyo pamoja na Makamu mkuu wa shule hiyo,Laban Nabiswa .

Wote kwa pamoja wanashitakiwa kwa kosa moja la mauaji ya kukusidia dhidi ya aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo,Marehemu Humphrey  Makundi(16) anayedaiwa kuuawa Novemba 6 mwaka huu na mwili wake kutupwa mto Wona jirani na shule hiyo. 

Walisomewa shitaka hilo na wakili wa serikali Cassim Nasri akisaidiwa na wakili wa Serikali Faygrace Sadallah mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya Julieth Mawole .

Akisoma hati ya mashitaka,wakili Nasri alidai kuwa,mnamo Novemba 6 mwaka huu huko maeneo ya  Himo wilaya ya Moshi,washitakiwa kwa pamoja walimuua kwa makusudi mtu mmoja aitwaye Humphrey Makundi.

Baada ya kusomewa shitaka hilo,washitakiwa hao hawakautakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji hadi mahakama kuu.

Washitakiwa walipelekwa mahabusu kwenye gereza kuu la mkoa,Karanga na kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Decemba 22 mwaka huu huku vilio vikitawala mara baada ya washitakiwa hao kusomewa shitaka lao.
 
DONDOO ZA TUKIO LILIVYOKUWA

1.Novemba 6 mwaka huu mwanafunzi huyo alidaiwa kutoweka shuleni hapo

2.Novemba 10 mwaka huu mwili wake uliokotwa ndani ya Mto Wona na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa,Mawenzi

3.Novemba 12 mwili wa marehemu ulizikwa na Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga baada ya kutojitokeza ndugu wa kuutambua 

4.Novemba 17 mwaka huu mahakama ya hakimu mkazi mjini moshi ilitoa kibali cha mwili huo kufukuliwa baada ya ndugu wa marehemu kubaini kuwa mwili uliozikwa katika makaburi hayo ni wa mtoto wao.

MWILI WAFANYIWA UCHUNGUZI

Mwili wa marehemu Humphrey ulifanyiwa uchunguzi na madaktari katika Hospital ya rufaa ya KCMC na kushuhudiwa na Baba mzazi wa marehemu na katika uchunguzi huo,ikibainika marehemu alikatwa na kitu chenye ncha kali kiunoni,mgongoni,kwenye mapaja na mbavu mbili zilivunjika.

Baba mzazi huyo akawaeleza wanahabari kuwa kulingana na majibu ya uchunguzi huo ni ukweli ulio wazi kuwa,mwanaye aliuawa na kwamba kifo chake kinatia shaka na kuvitaka vyombo vya uchunguzi kuwasaka wahusika wa mauaji ya mtoto wake mpendwa.

SHULE WASUSIA MAZISHI

Katika  hali ya kusikitisha na kushangaza,uongozi wa shule hiyo,ulisusia mazishi ya mwanafunzi huyo yaliyofanyika DEesemba 2 mwaka huu katika Kijiji cha Komakundi wilaya ya Moshi Vijijini.

Uongozi wa shule hiyo haukuweza kutuma mwakilishi katika mazishi hayo ambayo yaliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mgh’wira huku ibaada ya mazishi ikiongozwa na msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma ,Mchungaji Samwel Mshana.






 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni