Ijumaa, 1 Desemba 2017

VIGOGO SACCOS YA WALIMU MOSHI MJINI KIZIMBANI KWA MAKOSA 285



 MAOFISA watatu wa Chama Cha walimu cha Akiba na Mikopo(SACCOS) Manispaa ya Moshi,wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka 285 ya kushughi nyaraka na kuiibia saccos hiyo zaidi ya shilingi milioni 50.

Maofisa hao ni Gerald Thomas Msacky aliyekuwa Ofisa mikopo,Peter Thadeus Ndalianarua ambaye alikuwa mhasibu na Rehema Lucas Mlay aliyekuwa karani wa fedha.

Walifikishwa makahamani hapo chini ya ulinzi wa maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), mkoani Kilimanjaro na kusomewa mashitaka hayo mbele  ya hakimu Mkazi mfawidhi ,Aidan Mwilapwa. 

Katika kesi hiyo namba 22 ya mwaka 2017 ,washitakiwa walisomewa mashitaka hayo na mawakili na wanasheria kutoka Takukuru, Suzan Kimaro akisaidiana na Barry Galinoma.

Wakisoma hati ya mashitaka waendesha mashitaka hao walidai kuwa, washitakiwa hao kwa pamoja walitenda makosa hayo ya ubadhirifu na ufujaji wa fedha za chama hicho cha kuweka na kukopa, huku pia wakishitakiwa kwa makosa manne  ya kughushi nyaraka za malipo.

Mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo,Peter Thadeus Ndelianarua ambaye alikuwa mhasibu wa chama hicho na mshitakiwa wa tatu Rehema Lucas Mlay aliyekuwa karani wa fedha wa chama hicho, kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 142.

Kwa upande wa mshitakiwa wa pili,Gerald Thomas Msacky ambaye alikuwa ni ofisa mikopo wa SACCOS hiyo,yeye anakabiliwa na mashitaka 282 ambayo yanahusu  ubadhilifu wa fedha za chama hicho pamoja na kughushi nyaraka za malipo.
  
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka washitakiwa hao kwa nyakati tofauti tofauti kati ya januari na desemba mwaka 2012 kwa kutumia nyaraka za kughushi malipo waliweza kufuja fedha za chama hicho cha kuweka na kukopa zaidi ya shilingi milioni 50.

 Washitakiwa hao ambao wanashitakiwa chini ya kifungu cha 28 kifungu kidogo cha 2 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sheria namba 11 ya mwaka 2007 katika makosa 281 ya ubadhirifu wa fedha.

Pia washitakiwa hao wanashitakiwa chini ya vifungu namba 333, 335(a), na 337 vya kanuni ya adhabu 16 kama ilivyofanyiwa  marejeo mwaka 2002, ambapo makosa 4 ya kughushi nyaraka wanayotuhumiwa nayo.

Washitakiwa hao walikana mashitaka yao yote na wapo nje kwa   dhamana baada ya kutimiza mashariti ya dhamana yaliyowata kila mmoja kuwa na wadhamini wawili waliosaini dhamana ya maneno kiasi cha shilingi milioni 6 kila mmoja,kesi hiyo imeahirishwa hadi desemba 28 mwaka huu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni