Jumanne, 19 Desemba 2017

MKURUGENZI HALMASHAURI YA MJI WA BARIADI KIZIMBANI MOSHI



VIGOGO watatu waliokuwa watumishi katika Halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro,wameburuzwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka manne yakiwamo ya kughushi nyaraka,wizi na ubadhilifu wa fedha za umma.

Walioburuzwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, Melkizedeck Humbe ,aliyekuwa mweka hazina wa halmashauri hiyo,Thadeus Meela na aliyekuwa karani wa fedha wa Halmashauri hiyo,Valentina Mollel.

Kabla ya kuhamishiwa mkoani Simiyu,Humbe alikuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hai na Meela alikuwa mweka hazina kabla ya kumishiwa wilaya ya Ruangwa  na baadaye wilaya ya Pangani mkoani Tanga.

Walifikishwa mbele ya hakimu mfawidhi mahakama ya wilaya ya Hai,Arnold Kirekiano na kusomewa mashitaka na wakili na mwendesha mashitaka wa Takukuru,Suzan Kimaro.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani hapo ,washitakiwa hao wameshitakwia kwa makosa ya wizi na ubadhilifu wa fedha wa zaidi ya shilingi Milioni 27. 

Washitakiwa hao wanadaiwa kuandaa nyaraka za uongoza malipo ya   mishahara kwenda Hazina wakiomba fedha za mishahara huku wakitambua kuwa wameingiza majina ya watumishi hewa waliokuwa wamekwisha kuacha kazi katika Halmashauri ya Hai kwa sababu mbalimbali. 

Mwendesha mashitaka huyo wa takukuru aliiambia mahakama kuwa, baada ya kutumiwa fedha hizo waliandaa nyaraka za malipo (payment voucher), yenye namba 2015-000204 ya  Julai 08 mwaka 2014, na madokezo kumdanganya mwajiri kwa kuonyesha kuwa fedha hizo wanazirejesha kwa Katibu mkuu Hazina kama ulivyo utaratibu wa mishahara isiyo na wenyewe.

Pamoja na nyaraka hizo kuonyesha wanarejesha fedha hizo Hazina, waliandaa hundi ya wazi iliyowawezesha kuchukua fedha taslimu milioni 27.44, toka kwenye akaunti ya Halmashauri ya Hai iliyoko Benki ya NMB tawi la Hai na kuzifanyia matumizi binafsi kinyume na sheria.

Washitakiwa walikana mashitaka yao na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika na watakaosaini bodi ya shilini Milioni Tano kila mmoja.

Upande wa mashitaka uliiambia mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na washitakIwa hao watarejea tena mahakamani hapo Februari 15 mwaka 2018 ambako watasomewa maelezo ya awali ya kosa.

 Hata hivyo,furaha ya kuachiliwa kwa dhamana kwa washitakiwa wawili,Thadeus Meela na Valentina Mollel ilifutika baada ya kujikuta wakikamtwa tena na maofisa wa Takukuru. 

Baada ya kukamatwa walipelekwa moja kwa moja ofisi za takukuru wilaya ya Hai na taarifa za baadae zimedai kuwa,wawili hao wamepelekwa mahabusu na watafikishwa tena mahakamani desemba 21 mwaka huu kwa tuhuma ziongine za ubadhilifu wa fedha za Halmashauri hiyo.

Katika hatua nyingine , Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu alizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhairishwa kwa kesi hiyo na kutoa  onyo kwa watumishi wa umma ambao wanaendekeza ubadhirifu kupitia nyadhifa walizokabidhiwa wataendelea kuwakamata mmoja baada ya mwingine. 

Makungu ameonya kuwa, Taasisi yake itawasaka watumishi wote waliotenda makosa ya ubadhilifu wa fedha za serikali kokote waliko bila kujali walitenda makosa hayo wakati gani.

“Nirudie tena kutoa wito kwa wananchi wenye taarifa za ubadhirifu, ufisadi na uhujumu uchumi bila kujali kama ni za muda mrefu watuletee kwa kuwa makosa ya jinai huwa hayana ukomo” alisema Makungu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni