Jumatano, 22 Novemba 2017

BENKI YA KCBL YATUMIA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI KUKOPESHA WAKULIMA WA KAHAWA



Na Charles Ndagulla,Moshi

MIKOPO yenye riba kubwa na masharti magumu katika upatikanaji wa mikopo kwenye mabenki mengi hapa nchini imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa wakulima wengi hasa wadogo wadogo hali ambayo imechangia wengi wao kuishi maisha ya dhiki.

Hii inatokana na mabenki mengi kujiendesha kibiashara zaidi kwa kutoza riba kubwa pamoja na masharti magumu katika upatikanaji wa mikopo kwa wakulima ambao wengi hawana mali zinazoweza kuwekwa kama dhamana ya mkopo.

Benki ya ushirika mkoani Kilimanjaro(KCBL)iliyopo mjini moshi imeweza kuliona hilo na kujikita katika utoaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima wadogo wadogo lengo ni kuwawezesha kuboresha maisha yao.

Mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wakulima kukusanya mazao hususani zao la  kahawa kupitia mfumo wa stakabadhi ya mazao  ghalani ambao unatajwa kama mfumo bora na rafiki kwa wakulima wa zao la kahawa .

Benki hii ya ushirika ilisajiliwa kama chama cha ushirika mwaka 1994 kabla ya mwaka 1995 kupata  leseni ya kutoa huduma za kibenki ambako mwaka uliofuata yaani 1996 huduma za kibenki zilianza rasmi.

Meneja Mkuu wa Benki hiyo,Joseph Kingazi anasema mpaka sasa benki hiyo inao wanahisa 245 ambao ni vyama vya ushirika wa mazao (AMCOS),vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo(SACCOS) pamoja na watu binafsi wapatao 307.

Anasema wazo la kuanzishwa kwa benki hiyo kulitokana na mawazo yaliyotolewa na vyama vya ushirika wa mazao(AMCOS)mkoani Kilimanjaro ili kuweza kupata mikopo yenye riba na masharti nafuu katika kukusanya mazao yao.

“Lengo kuu la kuanzishwa kwa benki hii ilikuwa kuwasidia wakulima wadogo wadogo kuweza kupata mikopo yenye riba na masharti nafuu tofauti na mabenki mengine katika ukusanyaji wa mazao hususani zao la kahawa kupitia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani”,anasema kingazi.


Meneja huyo anataja mafanikio sita ambayo benki hiyo imepata tangu kuanzishwa kwake miaka 20 iliyopita ikiwa ni pamoja na kuwafikia wateja zaidi ya 762,177 katika mkoa wa Kilimanjaro na mikoa mingine iliyo jirani na mkoa huo .

Mafanikio menigne ni kuwa benki ya ushirika ya kwanza nchini inayomilikiwa na wazalendo kwa aslimia 100 huku ikitoa mikopo kwa wakulima wa zao la kahawa  yenye thamani ya ya shilingi Bilioni 28 hadi kufikia msimu wa kilimo wa 2016/17.

“KCBL imekuwa mwanzilishi wa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani toka mwaka 1999 na kwa sasa mfumo huu umeweza kuenea na kutumika sehemu mbali mbali hapa nchini  hasa kwenye mazao ya pamba,korosho na mazao mengine”,anasema.

Kwa mujibu wa meneja huyo,uwepo wa benki hiyo umekuwa kimbilio kwa wakulima wengi hatua ambayo imekuwa chachu kwa wakulima hao kuboresha maisha yao huku wanahisa na wateja wa kawaida wakipewa mafunzo mbalimbali kupitia kwa wataalam wa benki hiyo.

Anasema tangu kuanza kwa mfumo wa stakabadhi ya mazo ghalani,KCBL imeweza kumsaidia mkulima kutoka kukopwa mazao yake na kupata malipo kwa wakati huku mfumo huo ukivisaidia vyama vya msingi vya ushirika kujitegemea katika kununua mazao.

“Mfumo huo pia umevisaidia vyama vya msingi vya ushirika kujitengenezea mfuko wake wa ndani kwa ajili ya kununua mazao msimu bubu unapoanza tofauti na miaka ya  nyuma kabla ya mfumo haujaanza”,anasema.

Kwa upande wa wakulima meneja huyo anasema kuwa mfumo huo umechangia kuwahamasisha wakulima kulima kahawa kwa wingi kutokana kutokana na kupata malipo kwa wakati pale anapoleka mazao yake chamani.

Ametaja faida nyingine wanayopata wakulima kutokana na mfumo hiuo wa stakabadhi ya mazao ghalani kuwa ni pamoja na kupanda kwa bei ya kahawa kila msimu,kupanda kwa ubora wa mazao .

“Pia mkulima amefaidika kutokana na kupata faida  kwenye fedha za kigeni (Foreign Exchange Gain) pamoja na kupata  riba nafuu ikilinganishwa na wateja wengine”.anasema.

Anasema mikakati yao ya baadaye katika kuhakikisha wakulima wa zao la kahawa wananufaika na mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ni pamoja na kuuboresha mfumo huo ili wakulima waweze kuutumia vizuri.

Mikakati mingine ni kutoa elimu na semina kwa wakulima kwenye kilimo cha kisasa cha kahawa,elimu juu ya tabia yakujiwekea akiba pamoja na kutoa mafunzo kwa watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika .

Kupitia mfumo huo wa stakabadhi ya mazao ghalani,KCBL imeweza kutoa mikopo kwa ajili ya makusanyo ya kahawa na zaidi ya aslimia 75 ya kahawa yote  ya mkoa wa Kilimanjaro imefadhiliwa na benki hiyo.

Mpaka sasa benki hiyo inatoa huduma zake katika wilaya zote saba za mkoa wa Kilimanjaro ambazo ni Same,Mwanga,Rombo,Moshi Vijijini,Hai Siha na Moshi mjini na mkoa wa Arusha.

“Tunatoa huduma zaidi vijijini kupitia vyama vya msingi vya ushirika na kumfikia mtu/mkulima wa chini kabisa,pia tumefungua kituo cha huduma kwa wateja katika wilaya ya Rombo eneo la Tarakea Kibaoni”,anasema.

Licha ya baadhi ya  benki kuyumba katika utoaji wa mikopo kutokana na serikali kupitisha uamuzi wa kuzihamishia akaunti zote za serikali benki kuu,KCBL haijaguswa na hali hiyo kutokana na kutokuwa na fungu lolote toka serikalini.

Kwa mujibu wa meneja huyo wa benki ya ushirika,benki yake imekuwa ikitegemea akiba za wateja wao katika kufanya biashara ya pesa na kuwatoa hofu wateja wao kuwa benki hiyo haina tatizo katika suala zima la utoaji mikopo.

Kukua kwa tekinolojia ya mawasiliano kumerahisisha benki nyingi kutumia miamala ya fedha kwa ATM na Simu baking na KCBL haijapitwa na mfumo huo kwani kupitia Umoja Switch mtandao huo unazo zadi ya  ATMs 200 kwa nchi nzima kupitia huduma ya ushirika Card.

Mfumo huo na ule wa miamala ya kibenki kupitia simu ya kiganjani kwa mteja mwenye akaunti katika benki hiyo ambayo kujiunga kwake ni bure,ni mfumo unaomwondolea usumbufu mteja kusafiri umbali mrefu kwenda benki.

Meneja huyo anaeleza kuwa changamoto inayowakabili ni mtaji mdogo unaochangiwa na kupanuka  kwa shughuli za kibenki pamoja na gharama kubwa za TEKNOHAMA.

Kijazi anasema mipango yao ya baadaye ni kuongeza kiwango cha faida kutoka kwenye uwekezaji mbalimbali,kuongeza wanahisa wapya na kuongeza wateja wapya ndnai na nje ya mkoa wa Kilimanjaro kupitia vituo vya huduma kwa wateja vya benki hiyo.

“Mipango yetu mingine ni kwenda na teknolojia ya kisasa katika utoaji wa huduma zetu  pamoja na kufungua matawi kwenye baadhi ya wilaya zetu na mikoa jirani kama Arusha,Manyara na Tanga”,anasema meneja huyo.

Kwa upande wake meneja mikopo wa KCBL,Janeth Minja anasema hali ya urejesheji wa mikopo ni nzuri kutokana na wakopaji wengi kurejesha kwa wakati huku benki hiyo ikifanya ufuatiliaji kwa baadhi ya wakopaji ambao hawarejeshi kwa wakati.

Meneja huyo anasema kuwa pamoja na urejeshaji wa mikopo kuwa mzuri ipo changamoto kwa baadhi ya wkopaji kutorejesha mikopo yao kwa wakati na baadhi yao  hukimbilia mahamakani kuweka zuio la kuuzwa kwa mali wanazoweka kama dhamana ya mikopo.

Anasema mkakati wa benki hiyo ni pamoja na kufanya jitihada za kuwafuatilia kwa karibu wateja ambao mikopo yao hailipwi ili kuhakikisha wanalipa kwa wakati na kuondokana na usumbufu kwa kukamatwa kwadhamana zao na kuuzwa.

Minja anafafanua kuwa malengo yao ya muda wa kati na muda mrefu ni kuongeza kiasi cha ukopeshaji  katika sekta mbali mbali ikiwamo kilimo,biashara ndogo na kubwa,ujenzi na sekta ya utalii.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni