Jumamosi, 18 Novemba 2017

HUDUMA DUNI ZA AFYA KICHOCHEO VIFO VYA WATOTO NJITI



Serikali ya Tanzania imeshauriwa kutengeneza mifumo imara ya kitaasisi itakayosimamia utolewaji wa huduma za afya kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ili kupunguza vifo vya watoto hao ambavyo vinaongezeka kila mwaka. 

Kauli hiyo ya wadau wa afya ni mkakati maalumu wa kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, ikizingatiwa kuwa vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (pre-mature babies) vinashika nafasi ya pili baada ya vile vinavyotokana na maambukizi mbalimbali. 

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Kila mwaka duniani kote inakadiliwa watoto milioni 15 wanazaliwa kabla ya muda na idadi hiyo inaongezeka kila mwaka. Mwaka 2015 pekee nchini Tanzania watoto 236,000 walizaliwa kabla ya muda ambapo waliofariki walikuwa 9,400 ndani ya mwezi mmoja tangu kuzaliwa kwao. 

Kutokana na ongezeko la vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya muda, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakusudia kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kwa kuanzisha vitengo maalumu katika hospitali zote nchini ambazo zitakuwa na vifaa vya kisasa na wahudumu waliopitia mafunzo maalumu ya kuwatunza watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Ulisubisya Mpoki amesema wototo wanaozaliwa kabla ya wakati ni matokeo ya kutokuwa na huduma bora za mama na mtoto na uhaba wa watumishi wa afya wenye ujuzi wa kuwahudumia watoto hao pindi wanapozaliwa.

“Taarifa za kitakwimu tulizonazo kwa mwaka 2015 peke yake zinaonyesha Tanzania  hapa tulipata watoto 236,000 ambao walizaliwa kabla ya kutimiza siku 37 za kukaa katika matumbo ya mama zao. Katika hao watoto 9,400 walifariki”, anaeleza Dkt. Mpoki na kuongeza kuwa, 

“Sababu ya kufariki kwao ni watu kutokuwa na ujuzi  wa namna ya kuwahudumia lakini vilevile vifaa vya kutolea huduma na mahali maalumu panapoweza kukidhi mahitaji ya watoto hao ambao walitakiwa kuendelea kubaki katika matumbo ya mama zao lakini kwasababu moja au nyingine wakapata hayo matatizo”. 

Serikali inaandaa mfumo rasmi wa kukabiliana na changamoto ya vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ikiwemo utolewaji wa elimu kwa wafanyakazi wa afya na akina mama juu ya  njia sahihi za kuwatunza watoto hao ili wakue kama watoto wengine. 

“Wataalamu wa sayansi kutoka katika vyuo vikuu walikuwa wanaliaangalia tatizo hili kwa kipindi kirefu, wakagundua kwamba ni lazima tuweke mifumo itakayosaidia kupunguza shida hiyo”, anaeleza Dkt. Mpoki.

Amesema  wanashirikiana na Shirika la Misaada la Ujerumani (GIZ) kufanya tafiti, kutoa mafunzo na kujenga majengo yenye vifaa maalumu vya kuwatunza watoto hao ili kuwaepusha na vifo vinavyozuilika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni