Jumatatu, 20 Novemba 2017

RAIS ROBERT MUGABE KUSHITAKIWA



Mtandao wa Twitter unaofuatilia taarifa za vyombo vya habari nchini Zimbabwe unaripoti kuwa Kiongozi wa chama tawala Cha ZANU PF anaamini mchakato wa kumshtaki Bwana Mugabe utaendelea kama ilivyopangwa Jumanne , wakati ambapo chama bunge linatarajiwa kukaa. 

Hii ni kama muda wa makataa uliowekwa wa kujiuzulu kwake ambao ni leo  Jumatatu saa sita adhuhuri utakwisha kabla Bwana Mugabe hajajiuzulu

Halikuwa tangazo ambalo baadhi ya wazimbabwe walilisubiri, Bwana Mugabe bado ni rais na haijawa wazi ikiwa bunge sasa litaanza mchakato wa kumshitaki.

Watu wa Zimbabwe walikuwa wanatarajia kusikia Mugabe akijiuzulu kulingana na madai yao.

Baadhi ya wale waliokusanyika kufuatilia hotuba yake kwenye vilabu waliiambia BBC kuwa wamekatishwa tamaa na kutojiuzulu kwa rais Mugabe.

Hata hivyo hali  imeendelea kuwa tulivu katika maeneo mengi ya Zimbabwe, huku wengi wakiendelea kusubiri mchakato utakaofuata.

Duru kutoka ndani ya mazungumzo ya hatma ya Mugabe zimeiambia BBC kuwa Mugabe mwenye umri wa miaka 93 alikuwa amekubali kuondoka madarakani , lakini baadae akabadili mawazo yake.

Jeshi linatarajiwa kuwa na mkutano na waandishi wa habari leo Jumatatu  pamoja na Muungano wa Wapiganaji waliopigania Uhuru wa Zimbabwe. 

Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa tangu jeshi lichukue madaraka Jumatano iliyopita, Mugabe hakujiuzulu na alisema kuwa ameazimia kuongoza kongamano lijalo la Zanu-PF.

Hatma yake sasa iko mashakani kwani kulingana na mbunge wa Zanu-PF Terence Mukupe anasema kongamano hilo ni mahala panopofaa kumuidhinisha kiongozi mpya anayependelewa na chama cha Zanu-PF

Chanzo:BBC

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni