Ijumaa, 24 Novemba 2017

EU YAITAKA TANZANIA IJITATHIMN MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA



Umoja wa Ulaya (EU) umeitaka serikali ya Tanzania kuimarisha taasisi za uwajibikaji na uwazi kwa kupanua wigo wa Asasi za Kiraia kufanya kazi na jamii ili ifanikiwe katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwaletea wananchi maendeleo.  

Tamko hilo la EU linakuja siku chache baada ya serikali kuiondoa Tanzania kwenye Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa  (OGP) na kuziagiza Halmashauri za miji kutoshirikiana na Asasi za kiraia mpaka zipate idhini ya Wizara Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). 

Wito huo umetolewa  jijini Dar es Salaam na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Roeland van de Geer wakati akizindua Mradi wa Kutete Haki ya Demokrasia, Uwazi na Uwajibikaji katika jamii, 

Amesema changamoto kubwa inayoikabili Tanzania ni rushwa ambayo imedhoofisha juhudi za serikali kuwaletea wananchi maendeleo. 

“Rushwa inaharibu rasilimali za wananchi na jamii, zaidi kuvunja haki zao za msingi na uhuru. Gharama za kiuchumi ni kubwa lakini gharama za rasilimali watu na jamii ni kubwa zaidi”, amesema Balozi Geer na kuongeza kuwa,

“Rushwa ni adui wa maendeleo na mafanikio. Ni chanzo kikubwa cha umaskini na kikwazo kuushinda. Dawa ni uwazi”. 

Ili kuhakikisha rushwa inatokomezwa katika jamii, ameshauri kuundwa kwa taasisi imara zinazojiendesha kwa uwazi na kuwajibika kwa wananchi ambao ndio wadau muhimu wa shughuli za maendeleo. 

“Kupambana na rushwa ni mapambano yanayohitaji taasisi imara na wananchi makini katika ngazi zote. Lakini rushwa haitokei Tanzania peke yake.  

Rushwa ipo kila sehemu lakini tofauti ni kwamba taasisi zao zina uwezo na utashi wa kupambana nayo”, amesema Balozi.

Ameongeza kuwa rushwa bado ni changamoto katika Umoja wa Ulaya ambapo kila mwaka inaigharimu Euros bilioni 120 kwa mwaka. 

Amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuzijengea uwezo Asasi za Kiraia na wananchi hasa kwenye masula ya demokrasia, uwazi na uwajibikaji wa viongozi katika jamii ili kujenga jamii inayoheshimu misingi ya demokrasia.
 
Uwazi na Uwajibikaji katika Serikali za Mitaa
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa ‘Tuungane Kutete Haki’, Daniel El-Noshokaty amesema ili mapambano ya rushwa yafanikiwe inahitajika nguvu ya pamoja katika ngazi ya serikali ya mitaa ambako uwakilishi wa wananchi unapatikana.

“Rushwa ni kikwazo katika njia ya maendeleo ambayo Tanzania inapita; mapambano yake yanatakiwa kuanzia kwenye mizizi ya taifa. Kwa kufanya hivyo, nchi itakuwa na nafasi nzuri ya kutokomeza rushwa katika ngazi ya juu. Kwa Pamoja Tanzania inaweza ikasimama na kupambana na rushwa”, amesema El-Noshokaty. 

Kulingana na Shirika la Transparency International (2016) inaiweka Tanzania katika nafasi ya 116 katika ya nchi 176 zenye viwango kikubwa cha rushwa duniani. Na sababu kubwa ni kutokuwa na mifumo imara ya kitaasisi inayofanya kazi kwa uhuru na uwazi. 

Licha ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Magufuli kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa, bado rushwa inajitokeza kwa sura tofauti na kuathiri kwa sehemu kubwa upatikanaji wa huduma za kijamii, kudhoofisha mfumo wa utawala na kuzuia mazingira mazuri ya kufanya biashara. 

Ufunguzi huo wa Mradi wa ‘Tuungane Kutetea Haki” ulihudhuliwa na wadau mbalimbalimbali kutoka Asasi za kiraia na viongozi wa serikali, ambapo wote wamesisitiza uwepo wa uwazi katika shughuli za maendeleo na viongozi kuwa tayari kuwajibika kwa wananchi ili kujenga jamii inayoheshimu misingi ya demokrasia.

Mabadiliko ya Sera na Sheria kuchochea Uwazi

 
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa InterStar Consults, Lawrence Kilimwiko amesema Serikali za Mitaa zinaongozwa kwa msukumo wa kisiasa na utashi wa baadhi ya viongozi toka Serikali Kuu ambao wanatumia rasilimali za nchi kwa manufaa binafsi.

Ameitaka jamii kupaza sauti na kudai uwajibikaji na uwazi kwa kupigania mabadiliko ya kisheria na sera ambazo zimekuwa kikwazo kwa maendeleo ya nchi.  

Mradi wa ‘Tuungane Kutetea Haki’ unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya, Konrad-Adenauer-Stiftung (KAS) kwa kushirikiana na taasisi za Actions for Democracy and Local Governance (ADLG) na Civic Education Teachers Association (CETA) ambao utagharimu bilioni 2.5 katika miaka miwili ya utkelezaji wake.

Mradi huo una lengo kupunguza mianya ya rushwa kwa kukuza ushirikiano baina ya Asasi za Kiraia (AZAKI) na Serikali za Mitaa kwa kupanua wigo wa siasa, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ngazi ya Halmashauri. 

Unatekelezwa katika mikoa ya Geita, Simiyu, Ruvuma, Lindi, Mara, Kagera na Pwani ambaopo utafanya kazi sambamba na vyombo vya habari zikiwemo redio za kijamii katika maeneo husika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni