Jumatatu, 27 Novemba 2017

WATUHUMIWA MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SHULE YA SCOLASTICA WAPANDISHWA KIZIMBANI




Na Charles Ndagulla,Moshi

WATU  watatu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwanafunzi Humphrey makundi(16) wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Scolastica iliyopo katika mji mdogo wa Himo,leo wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na shitaka moja la mauaji.

Washitakiwa hao ni pamoja na mmoja wa wakurugenzi wa shule hiyo,Edrwad Shayo,Mwalimu wa shule hiyo Laban Nabiswa pamoja na mlinzi wa shule hiyo,Hamis Chacha.

Walisomewa shitaka hilo na wakili wa serikali Cassim Nasri akisaidiwa na wakili wa Serikali Faygrace Sadallah mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya Julieth Mawole .

Akisoma hati ya mashitaka,wakili Nasri alidai kuwa,mnamo Novemba 6 mwaka huu huko maeneo ya  Himo wilaya ya Moshi,washitakiwa kwa pamoja walimuua kwa makusudi mtu mmoja aitwaye Humphrey Makundi.

Baada ya kusomewa shitaka hilo,washitakiwa hao hawkautakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji hadi mahakama kuu.

Washitakiwa walipelekwa mahabusu kwenye gereza kuu la mkoa,Karanga na kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Decemba nane mwaka huu huku vilio vikitawala mara baada ya washitakiwa hao kusomewa shitaka lao.

Mshitakiwa wa pili na mmoja wa wamiliki wa shule hiyo,Edward Shayo alishindwa kujizuia na kumwaga chozi  muda mfupi  baada ya kutoka mahakamani huku akiwapa wosia ndugu zake akiwataka wamwombee kwani anaamini mungu yupo na atatenda muujiza.

Shayo alifikishwa mahakamani hapo peke yake  saa 5:39 akiwa ndani ya gari la polisi lenye namba za usajili T367 CAF aina ya Toyota landCruser akitokea Hospital ya Rufaa ya KCMC ambako amekuwa akipatiwa matibabu tangu kukamatwa kwake na alipanda kizimbani pamoja na wenzake saa 7 :11 mchana .

DONDOO ZA TUKIO LILIVYOKUWA

1.Novemba 6 mwaka huu mwanafunzi huyo alidaiwa kutoweka shuleni hapo

2.Novemba 10 mwaka huu mwili wake uliokotwa ndani ya Mto Wona na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa,Mawenzi

3.Novemba 12 mwili wa marehemu ulizikwa na Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga baada ya kutojitokeza ndugu wa kuutambua 

4.Novemba 17 mwaka huu mahakama ya hakimu mkazi mjini moshi ilitoa kibali cha mwili huo kufukuliwa baada ya ndugu wa marehemu kubaini kuwa mwili uliozikwa katika makaburi hayo ni wa mtoto wao.

MWILI WAFANYIWA UCHUNGUZI

Mwili wa marehemu Humphrey ulifanyiwa uchunguzi na madaktari katika Hospital ya rufaa ya KCMC na kushuhudiwa na Baba mzazi wa marehemu na katika uchunguzi huo,ikibainika marehemu alikatwa na kitu chenye ncha kali kiunoni,mgongoni,kwenye mapaja na mbavu mbili zilivunjika.

Baba mzazi huyo akawaeleza wanahabari kuwa kulingana na majibu ya uchunguzi huo ni ukweli ulio wazi kuwa,mwanaye aliuawa na kwamba kifo chake kinatia shaka na kuvitaka vyombo vya uchunguzi kuwasaka wahusika wa mauaji ya mtoto wake mpendwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni