Jumatano, 15 Novemba 2017

IDADI YA WANAUME WANAOPIGWA NA WAKE ZAO YAONGEZEKA-TAMWA



Jamii imetakiwa kujenga utamaduni wa kuzungumza na kujadili mambo ya msingi yanayohusu maendeleo ili kuondokana na mifumo kandamizi ya haki za binadamu na kujenga jamii inayoheshimu usawa, upendo na amani.

Inaeleezwa kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji vinaendelea katika ngazi ya familia na jamii kwasababu baadhi ya watu wanaoshuhudia matendo maovu hawatoi taarifa kwa mamlaka husika ili zishughulikiwe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Edda Sanga wakati akizungumza katika Uzinduzi wa Maonesho ya  Miaka 30 ya 
TAMWA amesema jamii bado inakabiliwa na changamoto nyingi za ukatili wa kijinsia ambazo zinatokea katika familia lakini waathirika au watu wanaoshuhudia hawazungumzi hadharani ili kukomesha vitendo hivyo. 

“Huko nyuma tumekuwa kimya sana haya mambo hatuyazungumzi kwa kuogopa kwamba nikiyatoa nje mambo ambayo yanahusu undani wa familia yangu nitaonekana kama vile ninakiuka misingi na haki za ustawi wa kabila langu”, amesema Edda Sanga. 

Licha ya serikali kushirikiana na Asasi za Kiraia kuendelea kutoa elimu na kupambana na vitendo vya kikatili katika jamii, wananchi pia wanawajibika kupaza sauti na kukemea viashiria vyote vinavyokiuka usawa wa kijinsia na haki za wanawake na watoto ambao ndio waathirika wakubwa wa ukatili. 

“Yaliyo mengi yanatokana na tulivyozaliwa na  kulelewa katika mifumo hii ambayo haichangamkii haki za wanawake na watoto mfano mimba za utotoni. Ni vizuri jamii tukakaa tukazungumza. Ni wakati wa kuyatoa nje tuyazungumze ili suluhu apatikane palepale ambapo tukio limetokea”, amesema Edda Sanga. 

Ripoti ya Uchunguzi ya Watu na Afya ya 2010 inaonyesha kuwa asilimia 10 ya wanawake walio na umri wa miaka kati ya 15 mpaka 49 waliripoti kulazimishwa kufanya mapenzi kwa mara kwa kwanza na 48% ya wanawake walioolewa wanapata udhalilishaji wa kingono. 

Pia amewataka wanawake ambao wanashiriki kuwafanyia ukatili wanaume waache kwasababu wanadhalilisha utu wao na kukwamisha harakati za kuleta usawa na haki katika jamii  ikizingatiwa kuwa kila mtu pasipo kujali hali yake ana haki ya kuishi kwa amani na kuwa na ustawi mzuri wa maisha yake. 

“Tunapozungumza masuala hayo na mwanaume tumuhusishe ili na yeye ahamasike sasa kuingia hata kama ni kwa mawazo tu kwasababu haya masuala yanataka tubadilishe namna tunavyofikiri",amesema. 

"Hatuwezi kubadilika kama tunaongea wanawake kwa wanawake ni lazima tuwe na wanaume huo ndio mfumo tunauchukua”, ameeleza Edda Sanga. 

Katika miaka ya hivi karibuni wamejitokeza wanaume ambao wanafanyiwa ukatili na wake zao ikiwemo kupigwa, kutukanwa na hata kunyimwa tendo la ndoa. Lakini muitikio wake sio mkubwa ikilinganishwa na matukio yanayowapata wanawake na watoto. 

Baadhi ya tafiti zinaeleza kuwa asilimia 35 ya wanaume wanapigwa na wake zao ingawa hawasemi kutokana na kuona aibu kwasababu bado mtazamo wa jamii umeegemea kwenye mfumo dume ambao unampa mwanaume nguvu ya kumtawala mwanamke.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni