Jumatatu, 13 Novemba 2017

KIGWANGALA AMVAA NYALANDU,ATAKA ACHUNGUZWE NA TAKUKURU



By Daniel Mjema,Mwananchi

DODOMA.Waziri wa Maliasili na Utalii,Dk.Hamis Kigwangala amemlipua waziri wa zamani wa wizara hiyo,Lazaro Nyalandu akimtuhumu kwa matumizi mabaya ya madaraka.

Akichangia mpango wa wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018,Dk Kigwangala ameiagiza Takukuru na polisi kumchunguza Nyalandu.

Kigwangala amesema Nyalandu aliikosesha serikali mapato ya shilingi Bilioni 32 kwa miaka miwili aliyohudumu katika wizara hiyo kwa  kushindwa kusaini sheria ya tozo kwa hotel za kitalii.

Mbali na tuhuma hizo,pia alimtuhumu kutumia helkopita ya mwekezaji mmoja raia wa kigeni kipindi cha kampeni  zake za kugombea urais 2015,wakati kampuni ya raia huyo ikituhumiwa kwa ujangili.

Hata hivyo wakati Kigwangala akitoa tuhuma hizo,tayari Nyalandu alishasema kuwa tuhuma ambazo zimeanza kuibuliwa mitandaoni dhidi yake si za kweli bali zinalenga tu kumchafua.

Akizungumza na mwananchi hivi karibuni ,alishangaa iweje ziibuliwe sasa zaidi ya miaka miwili tangu aachie uwaziri.

LEMBELI ALIVYOMSHUKIA NYALANDU


Machi 8 mwaka 2015,aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na mazingira,James Lembeli,alimshutumu vikali Nyalandu akimtuhumu  kugeuza  wizara hiyo kama ofisi yake binafsi.

Lembeli alitoa shutuma hizo mkoani Morogoro muda mfupi kabla ya kamati hiyo kupokea taarifa ya uhifadhi kutoka kwa uongozi wa hifahdi ya Taifa ya Mikumi.

Shutuma hizo zilikuja baada ya aliyekuwa mbunge wa  Viti maalumu kwa wakati huo Ester Bulaya kupitia kundi la vijana kutoka mkoa wa Mara(sasa yuko Chadema) kutaka wabunge wapewe nakala ya tangazo la serikali(GN) linalohusiana na tozo mpya kwenye hoteli za kitalii zilizopo kwenye hifadhi za Taifa.

Nyalandu alisaini tangazo hilo la serikali februari 27 mwaka 2015 baada ya kuwapo na msuguano wa muda mrefu na wabunge ambao kwa muda mrefu walikuwa  wakimshutumu kwa  kushindwa kutekeleza amri ya mahakama kuu kuhusiana na tozo hizo mpya.

Lembeli alihoji kitendo cha Nyalandu  kuendesha vikao na wamiliki wa hoteli hizo licha ya mahakama kuamulu wamiliki wa hoteli hizo kulipa tozo mpya kama zilivyopendekezwa na shirika la hifadhi za taifa,Tanapa.

“Uliona wapi maamuzi ya mahakama yanajadiliwa nje ya mahakama,kulikuwa na nini hapo?,tunafahamu kilichokuwa kinaendelea,sisi ndiyo tunaisimamia wizara hii siyo watu wa nje?,alihoji .

Lembeli  alisema kuwa wizara ya maliasili na utalii imekuwa kama ofisi ya mtu binafsi na kuongeza kuwa umefika wakati wabunge wasema hapana, imetosha na hakuna cha utatu mtakatifu katika hilo.

Kwa upande wake Bulaya alitaka wabunge wapewe nakala hiyo ya tangazo la serikali ili waone kama kilichosainiwa kinaendana na yaliyomo kwenye uamuzi wa mahakama na kuonya kuwa bunge lingewaka moto kama Nyalandu alisaini tofauti na uamuzi wa mahakama.

Kutoka na msuguano huo,wajumbe wote wa kamati hiyo walipitisha azimio la kumtaka Nyalandu kuwasilisha nakala hiyo kwa kamati hiyo katika majumuisho ya ziara yao ambayo yalifanyika Jijini mwanza.


 Mgororo huo wa tozo mpya katika hoteli za kitalii zilizopo kwenye hifadhi za tiafa ulikolezwa na hatua ya Nyalandu kugoma kutekeleza maamuzi ya mahakama kuu akidai kuwa kulikuwa na udanganyifu uliofanywa na wataalamu wa Shirika la Hifadhi za taifa,Tanapa.

Katika kujitetea huko,Nyalandu alidai kuwa baadhi ya Hotel hazikujumuishwa katika mchakato wa ulipaji wa tozo hizo mpya na kwamba tozo hizo zingeweza kukusanywa kwa hotel 27 tofauti na hotel 56 zilizopo ndani ya hifadhi hizo.

Mkurugenzi mkuu wa  TANAPA,Allan Kijazi alisema kuwa hatua ya shirika lake kutaka wenye hoteli hizo kulipa tozo mpya ni kutokana na wenye hotel hizo kupandisha gharama za malazi kwa wageni kwa kila kitanda.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo,awali Tanapa ilikuwa ikitoza kati ya dola 4 hadi 8 kwa kitanda kutokana na wageni kutozwa dola kati ya 100 hadi 150 kwa kitanda na wenye hoteli.

Alisema kuwa wenye hoteli hizo walipandisha tozo kwa wageni na kutoza kati ya dola 350 hadi dola 1,000 kwa kitanda hivyo shirika hilo kuamua kupendekeza  tozo mpya za kati vya dola 30 na 70 ambazo wenye hotel hizo walizigomea.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni