Jumatano, 7 Januari 2015

EWURA YASHUSHA BEI ZA MAFUTA



Bei ya mafuta ya petroli, dizeli na ya taa nchini inazidi kushuka kutokana na kuporomoka kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia tangu Juni mwaka jana.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi alisema jana kuwa bei ya rejareja ya petroli kuanzia leo imeshuka kwa Sh74, dizeli kwa Sh62 na mafuta ya taa kwa Sh54.

Bei hizo zinashuka wakati kukiwa na mjadala mkali kuwa bei zilizopo sasa hazisadifu hali halisi ya kuporomoka kwa mafuta ghafi yanayouzwa kwa Dola 50 za Marekani kwa pipa.

Ngamlagosi alisema bei hizo mpya zimekokotolewa kutokana na bei ya mafuta ghafi na kwamba huenda ikapungua zaidi siku zijazo.

Alisema kwa sasa bei ya jumla za nishati hiyo zimepungua ukilinganisha na mwezi uliopita, kwani kwa lita petroli imepungua kwa Sh73.75, dizeli Sh62.08 na mafuta ya taa kwa Sh54.34.

“Be za mafuta safi ya petroli kwa tani katika soko la dunia imepungua kwa Dola 249 za Marekani, dizeli kwa Dola 189 na mafuta ya taa kwa Dola 180.

Kufuatia bei hizo mpya, petroli katika vituo vya Dar es Salaam haitazidi Sh1, 955, dizeli Sh1,846 na mafuta ya taa Sh1,833.

Kutokana na gharama kubwa za usafirishaji, wakazi wa Kyerwa Kagera ndiyo watakaokuwa wakinunua petroli kwa bei ya juu zaidi kwa Sh2,192, dizeli Sh2, 083 na mafuta ya taa Sh2,070.

Ngamlagosi alisema ni vigumu bei iliyopo ikaendana na bei ya sasa katika soko la dunia kwa kuwa mafuta yanayoingia nchini hununuliwa kwa bei ya mwezi mmoja uliopita na kwamba kushuka kwa thamani ya Shilingi kumechangia pia.

“Watu wanatakiwa wafahamu kuwa gharama za kodi hazibadiliki. Pia kuna malipo ya usafirishaji na usambazaji, vyote vinachangia karibu asilimia 40 ya gharama za mafuta.

“Asilimia 60 tu ndiyo inayoathirika na kushuka au kupanda kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia,” alisema.

Mhadhiri wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Goodluck Urassa alisema bei hizo mpya zinaendana na hali halisi ya soko la dunia.


CHANZO: MWANANCHI
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni