Jumamosi, 17 Januari 2015

BILIONI 2 ZATUMIKA KUONDOA ADHA YA BARABABARA MAMBA MYAMBA, MPINJI JIMBONI SAME MASHARIKI



Kiasi cha Shilingi bilioni 2 kimetumika kukamilisha ujenzi wa barabara katika vijiji vya Mamba Myamba na Mpinji  vilivyopo katika Jimbo la Same Mashariki mkoani Kilimanjaro huku wananchi wa kipongeza hatua hiyo.

Wakizungumza walisema tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1961 walikuwa wakiteseka kutokana na kukosekana kwa huduma mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara.

“Tunamshukuru sana Rais Kikwete kwa kutujengea barabara hizi, kwetu sisi wananchi imekuwa faraja kubwa, kukamilika kwa barabara hizi kutafungua fursa nyingi ambazo zitakuwa chachu ya maendeleo katika vijiji vyetu,” walisema wananchi hao.

Mmoja wa wakazi wa Mamba Myamba, Elieti Kikoro alisema walikuwa wakilazimika kubeba mizigo yao kichwani au kwa kutumia wanyama kama punda kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mibovu hususani kipindi cha masika.

Alisema kujengwa kwa barabara hizo kumekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi waishio milimani katika jimbo hilo ambalo hawakutegemea kama siku moja watakuwa na barabara ambayo itawezesha kusafirisha mazao yao.

Diwani wa Kata ya Mamba Myamba, Michael Chikira alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kufungua fursa za kiuchumi na wananchi wataweza kuzalisha kwa wingi zao lao la tangawizi na kuinua pato la taifa.

Alisema barabara hiyo ilianza kujengwa kufuatia ombi lililotolewa kwa Rais Kikwete na Mbunge wa jimbo la Same Mashariki Anne Kilango Malecela, ambao Rais Kikwete aliaahidi kutekeleza ombi hilo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo, Anne Kilango Malecela alisema kujengwa kwa barabara hizo ni msaada mkubwa kwa wananchi waishio maeneo ya milimani katika jimbo hilo. 

Aidha Kilango aliongeza kuwa barabara hizo zenye urefu wa Kilometa 13.8,  zimegharimu kiasi cha shilingi bilioni mbili, na kwamba maeneo zilizopojengwa barabara hizo ni barabara ya Parame Kitubwa-Korogwe Mpinji (Km 8.7), na Kiwandani Manga-Chalinze (Km 4.8).

Maoni 1 :

  1. Tunataka kujua ukubwa wa km za mraba za Tarafa ya Mamba Vunta

    JibuFuta