Jumatatu, 19 Januari 2015

MUWSA ISIWAFUMBIE MACHO WADAIWA HAWA SUGU



Mamlaka  ya maji safi na usafi wa mazingira Mjini Moshi(MUWSA) inahudumia wakazi wapatao 194,756 hii ni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 pamoja na wakaazi wengine 30,000 waliopo maeneo ya wilaya za Hai na Moshi Vijijini.

Kwa sasa Mamlaka hiyo inao wateja wapatao 23,123 ambao wanapata huduma ya maji safi na salama kutoka chemichemi nne na visima virefu vinne ambako uzalishaji wa maji safi na salama unakadiliwa kuwa ni wastani wa mita za ujazo 34,944 kwa siku iikilinganishwa na mahitaji ya mita za ujazo 45,082 kwa siku.

Hali ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa mji wa moshi kwa sasa ni wastani wa saa 18 hadi 24 kutegemea na eneo lilivyo ambapo mamlaka hiyo imeugawa mji wa moshi katika kanda tisa ambazo ni Maili sita, Shanty Town, Soweto,City Centre,Majengo,Bomambuzi,Chekereni na Himo.

Mamlaka hiyo ambayo ni moja ya mamlaka kubwa hapa nchini,imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha huduma  kwa wakazi wa mji wa moshi ikiwamo utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye lengo la kuongeza maji na kuwafikia wateja wengi zaidi.

Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa chanzo kipya  cha maji ya Coffee Curing chenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 700 kwa siku,ujenzi wa chemchem ya mto karanga mradi utakaoongeza mita za ujazo 3,800 kwa siku.

Pamoja na jitihada hizo nzuri za MUWSA katika kuwapatia huduma bora ya maji safi na salama wakazi wa mji wa moshi na maeneo ya mji mdogo ya Himo,zipo changamoto kadhaa zinazoweza kukwaza ndoto hizo.

Moja ya changamoto hizo ni kuwapo na wateja wasiolipia ankara za maji kwa muda mwafaka na hivyo kuwapo na malimbikizo makubwa ya madeni na hawa hatuna budi kuwaita wadaiwa sugu.


Miongoni mwa wadaiwa hawa sugu ni taasisi za serikali ambazo zinadaiwa kiasi cha sh,Milioni 800,fedha hizi ni nyingi sana na endapo zitalipwa zinaweza kutumika kuboresha miundombinu ya maji na wananchi wakapata maji ya uhakika bila ya mgao .

Deni hilo ambalo linatajwa kuendelea kuongezeka limekuwa kikwazo kwa juhudi za Muwsa za kufikisha huduma bora ya maji safi na salama na uondoaji wa maji taka kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo.

Akitoa taarifa  ya utekelezaji wa shughuli za mamlaka hiyo hivi karibuni kwa Naibu Waziri wa maji Amos Makalla,kaimu mwenyekiti wa Bodi hiyo,Elizabert Maro Minde,aliiomba wizara ya maji kuingilia kati deni hilo kwa kuzibana taasisi hizo ili ziweze kulipa madeni yake.

Minde alizitaja Taasisi hizo kuwa ni pamoja na jeshi la polisi,Chuo cha mafunzo ya Taaluma ya jeshi la polisi nchini(MPA) zamani kikiitwa CCP,jeshi la magereza na Idara ya Mahakama na kuongeza kuwa licha ya mamlaka hiyo kujitahidi kukusanya madeni,imefika pahala inashindwa.

Makalla alikuwa katika ziara ya siku mbili mkoani Kilimanjaro ambako pamoja na mambo mengine alizindua chanzo kipya cha maji kilichopo mto karanga ambacho kinazalisha mita za ujazo 3,800 kwa siku na kunufaisha maeneo ya Bomambuzi,Pasua,Matindigani,Kaloleni,Soweto na Kiboriloni.

Mamlaka hiyo ililalamika mbele ya Makalla kwamba Taasisi hizo za serikali hazitoi kipaumbele katika kulipa madeni hayo licha ya ukweli kwamba kila mwaka zimekuwa zikipata fedha kutoka kwenye bajeti za wizara zao kwa ajili ya kulipia huduma za maji na mahitaji mengine.    

Ni kweli kwamba taasisi nyingi za serikali zimekuwa zikilalamikiwa mara kwa mara na watoa huduma kwa kushindwa kulipia huduma wanazopewa na taasisi mbalimbali licha ya kwamba wizara zao hutenga kwenye majeti zake fedha kwa ajili ya taasisi zilizo chini yake.

Malalamiko haya yamekuwa ni ya siku nyingi na sasa yanaonekana kuwa sugu kutokana na taasisi husika kutoona umhimu wa kulipia huduma hizo licha ya kuzihitaji kwa udi na uvumba na hivyo kuibua malumbano baina ya watoa huduma na watumiaji wa huduma.  

Pamoja na mamlaka hiyo kuendelea kuzidai taasisi hizo,walimweleza Makalla kwamba bado wanaendelea kuzipatia huduma ya maji bila kusitisha huduma hizo kwa kile walichodai ni kutokana na mahitaji makubwa ya maji katika maeneo husika ya wadaiwa hao.

Kwanza ni jambo la kuwapongeza MUWSA kwa kuonyesha moyo wa huruma wa taasisi hizo nyeti ambazo kwa hakika zikisitishiwa huduma hiyo panaweza pakatokea mtikisiko mkubwa unaoweza kuchafua hali ya hewa.

Wakati nikiwapongeza mamlaka hiyo kwa kuonyesha uungwana kwa wadaiwa hao sugu,nashindwa kupata jibu la moja kwa moja kwamba ni kweli taasisi hizo hazina uwezo wa kulipia ankara za maji kiasi cha kuonewa huruma ya kutokusitishiwa huduma hiyo?

Swali hili haliwezi kupata majibu kwa sababu wakati MUWSA wakiwaonea huruma wadaiwa hawa wa mamilioni ya fedha,imekuwa mstari wa mbele kuwasitishia huduma wateja wake ambao madeni yao hayafikii hata robo ya fedha wanazozidai taasisi hizi.

Napata wakati mguu kuelewa ni mfumo upi unaotumiwa na mamlaka hiyo kuwasitishia huduma wateja wake wadogo baada ya kuwatumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu zao za kiganjani na kuwapa siku saba wawe wameshalipia ankara zao.

Kama MUWSA wameweza kuwakabili wateja wadogo kwa kuwasitishia huduma za maji kwa kuwatumia ujumbe huo wa simu,wanashindwaje kufanya hivyo kwa wateja hao wakubwa ambao sasa wanaendelea kutumia huduma wasiyoilipia bila hofu wala woga. 

 Ni ajabu na kweli kwa mamlaka kubwa kama hii kuanza kulia lia bila kuchukua hatua za kukabiliana na wadaiwa sugu kama magereza,polisi na Idara ya mahakama ambazo kila mwaka hupokea fedha kwa sababu ya ulipiaji wa ankra za maji,tuwaulize fedha hizo wanazipeleka wapi ?

Minde alilalamika mbele ya Makalla kwamba deni hilo limewarudisha nyuma na wakamuomba kwa dhamana aliyopewa na rais (Jakaya Kikwete)alivalie njuga deni hilo kwa madai kwamba taasisi hizo hazilipi kipaumbele deni hilo kwa sababu eti wanaona mamlaka hiyo ni taasisi ya serikali kama walivyo wao. 

Kiasi hicho cha fedha pia kingetosha kukamilisha miradi mbali mbali ambayo mamlaka hiyo wanaitekeleza kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maji hivyo kutosheleza mahitaji ya wakazi wa mji wa moshi ambako baadhi ya maeneo yamekuwa hayana maji ya uhakika.

Mtazamo wangu ni kwamba MUWSA wachukue hatua sasa dhidi ya wadaiwa hawa sugu ikiwamo kuwasitishia huduma ya maji  badala ya kulia kulia na kuishia kufukuzana na wateja wadogo,kwani waswahili wanasema sheria ni msumeno.
 Kwa maoni: +255752847877

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni